Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 13 January 2015

SHEIN ATIBUA NDOTO ZA LOWASSA, MEMBE

 
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kinadaiwa kuwa na mpango wa kumsimamisha Dk. Ali Mohammed Shein kuwania urais wa Muungano katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Hatua hiyo itatibua ndoto za urais za Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ambao kambi zao zinatajwa kuwa na nguvu ndani ya chama hicho.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya chama hicho vimeeleza kwamba, hatua ya kutaka kumsimamisha Dk. Shein inatokana na Rais huyo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutokuwa na makundi kwenye chama, hivyo kumaliza ‘mnyukano’ unaoendelea wa makada wa chama hicho ambao wanaendelea kumwaga fedha katika mitandao na kambi mbalimbali.
Sababu nyingine ni ile ya CCM kutafuta namna ya kuulinda Muungano, ikiamini kwamba inaweza kupunguza munkari wa Wazanzibari wanaoupinga Muungano huo, hivyo kujihakikishia kura za visiwa vya Unguja na Pemba.
Taarifa hizo zimekuja wakati Kamati Kuu ya CCM ikitarajiwa kuketi kesho Jumanne katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Unguja kujadili na kutathmini hali ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Ikiwa uamuzi huo utafikiwa katika vikao rasmi vya chama, utahitimisha safari ya kwenda Ikulu ya vigogo kadhaa wa chama hicho, akiwemo Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, ambaye licha ya yeye kutotangaza rasmi, lakini ametajwa kwamba amejipanga vilivyo kuhakikisha anaomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo adhimu.
“CCM ina wakati mgumu katika kutafuta mrithi wa Rais Jakaya Kikwete, vigogo wengi wanatajwa na wengine wametangaza nia, lakini suala la Muungano nalo limeleta mtikisiko mkubwa na wanatafuta namna ya kukabiliana na mtikisiko huo.
“Wazanzibari wamekuwa wakilalamika kwamba Muungano hauwasaidii, ndiyo maana kwenye maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walisema wanataka Muungano wa Mkataba, ambao kimsingi hautakuwa na nguvu, hivyo endapo Dk. Shein atateuliwa anaweza kurejesha matumaini,” kimesema chanzo chetu kutoka ndani ya CCM.
Chanzo kingine kimesema, endapo Dk. Shein – rais wa kwanza wa SMZ kutoka Kisiwa cha Pemba – atateuliwa, CCM ina uhakika wa kupata kura za Unguja na Pemba.
Ingawa suala hilo halijawa wazi, lakini kitendo cha vigogo wa CCM wanaotajwa kuwania urais kujikita Zanzibar wakati huu wa vikao vya Kamati Kuu kinaashiria kwamba kuna hofu kubwa ya karata kugeuka wakati wowote ikiwa hawatafanya jitihada za ziada.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, ilielezwa kwamba baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo wamekuwa wakipishana kwa usafiri wa ndege na boti kwenda Zanzibar kutafuta kuungwa mkono na wajumbe wa NEC na waliopo visiwani humo.
Gazeti moja la kila siku liliripoti mwishoni mwa wiki kwamba, vigogo wa urais waliofanya ziara kwa nyakati tofauti hivi karibuni visiwani Zanzibar ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano) Stephen Wasira, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alialikwa kuhudhuria Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) Jumamosi yaliyoandaliwa na Mbunge wa Mpendae na Mafanyabiasha mashuhuri, Salum Turky.
Kadhalika Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa ambaye wakati wa Sikukuu ya Krismasi ya mwaka 2014 alikuwa Zanzibar.
Inaelezwa kwamba suala kubwa ambalo Kamati Kuu italijadili ni kuangalia mwenendo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015 tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, lakini pia suala la akaunti ya Tegeta Escrow.
Makada wa chama hicho wanaowania urais mbali ya Lowassa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ni Bernard Membe – Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa – ambaye yaonekana bado anasubiri kuoteshwa ili atangaze rasmi ingawa taarifa zinasema wafuasi wake wamekuwa wakiendelea na kampeni hadi mitandaoni.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi, Teknolojia January Makamba, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

No comments:

Post a Comment