Na Jovither Kaijage, Mwananchi
Ukerewe. Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu amemsimamisha kazi mjumbe wa kamati ya utendaji ya chama hicho Wilaya ya Ukerewe, Wilbrod Machemli kwa kushindwa kutimiza wajibu wake, ikiwa ni pamoja na kutotangaza ujio wa kiongozi huyo.
Rungu hilo pia limemkuta katibu wa Chadema wilaya hiyo, Libelatus Mlebele ambaye amepewa onyo kali.
Akizungumzia hatua hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Nansio jana, Mwalimu ambaye ameanza ziara mkoani hapa juzi kwa lengo la kuwashukuru wananchi baada ya kukichagua chama hicho katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, alisema hakuridhishwa na maandalizi yaliyofanywa na viongozi hao.
Kutokana na hali hiyo, Mwalimu alimwagiza Mwenyekiti wa wilaya wa chama hicho, Jacobo Munyaga kwa gharama zake amwandalie mkutano mwingine kabla ya mwisho wa mwezi ujao.
Mwalimu pia alitilia shaka matumizi ya fedha yaliyotajwa kutumika kutangaza uwepo wa mkutano wake.
Alisema Chadema hakipo tayari kulinda viongozi wazembe na wasiowajibika na kuwaonya wajumbe wa kamati tendaji hasa katibu ambaye bado yupo katika uangalizi wa miezi sita kwa maelezo kuwa anaweza kuondolewa kazini.
Kabla ya kuchukua uamuzi huo, Mwalimu aliwaita mbele wakazi wanne wa kata za Kakerege, Nansio, Nakatungulu na Kagera ambao walikiri kutosikia matangazo ya ujio wake.
Hatua hiyo aliichukua baada ya kuwasili katika Uwanja wa Mongera wa mjini Nansio saa 9:30 alasiri huku kukiwa na idadi ndogo ya watu ikilinganishwa na ziara zake za nyuma.
Mbali na hilo, pia Mwalimu ametumia mkutano huo kukemea matumizi mabaya ya fedha za serikali yanayofanywa na viongozi waandamizi wakati huduma za kijamii zikizidi kuwa mbaya.
Alisema ziara za mara kwa mara za nje ya nchi zisizo za lazima zinazofanywa na Rais Jakaya Kikwete pamoja na viongozi wengine hazina tija kwa taifa.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Joseph Mkundi akizungumza katika mkutano huo, alisema katika katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wao wamepata mafanikio makubwa.
Alisema mbali na kusimamia vyema matumizi ya fedha za serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pia halmashauri hiyo imekamilisha mipango ya kununua greda moja la kutengeneza barabara lenye thamani ya Sh400 milioni hivi karibuni chama hiko kimeluwa kikipigania kukishinikiza serikali kuwachukulia hatua watuhumiwa wa ufisadi.
Hata hivyo, alisema mbali ya halmashauri hiyo kupata hati safi ya matumizi ya fedha za umma pia hivi karibuni huko jijini Nairobi Kenya, Halmashauri hiyo ilipata tuzo ya kukidhi vigezo vya sheria ya ununuzi ya umma kati ya wilaya 166 za nchi nzima.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment