Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 15 January 2015

KASHFA YA TEGETA ESCROW YAWASUKUMA VIGOGO WAWILI KIZMBANI

Watuhumiwa wa kesi ya kupokea rushwa kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrwo, Rugonzibwa Mujunangoma (kushoto) na Theophil Bakwea  na wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka. Picha na Said Khamis 
Na Tausi Ally, Mwananchi
Dar es Salaam. Miezi michache baada ya kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kutikisa nchi, watumishi wawili waandamizi wa Serikali wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakituhumiwa kupokea rushwa ya mamilioni ya fedha zilizotoka kwenye akaunti hiyo.
Mahakama hiyo ilielezwa jana kuwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliwekewa kiasi cha Sh323 milioni kupitia akaunti yake namba 00120102602001.
Kadhalika, Mahakama ilielezwa kuwa Februari 12, 2014, Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), Wizara ya Nishati na Madini, Theophillo Bwakea alipokea rushwa ya Sh161,700,000 kupitia akaunti yake namba 004101102643901.
“Upelelezi wa kesi umekamilika naomba mahakama izuie akaunti ya mshtakiwa iliyotumika kupokea fedha hizo za escrow na kesi ipangwe kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali,” alisema Leonard Swai ambaye ni Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akisoma hati ya mashtaka katika kesi namba 11 ya mwaka 2015 inayomkabili Mujunangoma, Swai alidai mshtakiwa huyo alifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 15 (1)cha Sheria ya Kupambana na Rushwa, Namba 11 ya mwaka 2007.
Swai alidai kuwa Februari 5, 2014 katika Benki ya Mkombozi iliyopo wilayani Ilala, Dar es Salaam, Mujunangoma akiwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa James Burchard Rugemalira, ambaye ni mshauri huru wa kitaalamu, mkurugenzi wa VIP na mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Mujunangoma alikana na mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha sheria anachoshtakiwa nacho, mshtakiwa huyo hahitaji kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hakimu Emilius Mchauru alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi ya Serikali na kwamba kila mdhamini asaini hati ya maneno ya Sh10 milioni.
Pia, Hakimu Mchauru alimtaka mdhamini ama mshtakiwa mwenyewe, kuwasilisha mahakamani hapo nusu ya fedha taslimu anazodaiwa kuzichukua kama rushwa, ama kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo, baada ya kutolewa kwa masharti hayo, mshtakiwa alipata wadhamini wawili wanaoaminika , kutoa hati mbili za mali isiyohamishika ambazo alidai zina zaidi ya thamani ya fedha iliyomo ndani ya hati ya mashtaka.
Kuhusu kuzuia akaunti ya mshtakiwa, Hakimu Mchauru aliutaka upande wa mashtaka kuwasilisha maombi mahakamani hapo na kuyaambatanisha na hati ya kiapo itakayounga mkono maombi hayo.
Kwa upande wa Bwakea, aliyefunguliwa kesi namba 12 ya 2015, Swai alidai kuwa siku hiyo ya tukio katika benki ya Mkombozi alipokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti yake.
Swai alidai kuwa mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha kama zawadi kwa kushiriki kama mjumbe aliyeandaa sera iliyoruhusu sekta binafsi kuzalisha na kuuza umeme kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Bwakea alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na akaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe ya kusomwa kwa maelezo ya awali.
Hata hivyo, Swai aliiomba mahakama hiyo izuie akaunti ya mshtakiwa iliyotumika kupokea kiasi hicho cha fedha na mahakama iliridhia na kutoa amri ya kuizuia mtu yeyote kutoa ama kuchukua fedha kutoka kwenye akaunti hiyo.
Hakimu Moshi alimtaka mshtakiwa (Bwakea) kuwa na wadhamini wawili, watumishi wa Serikali ambao kila mdhamini asaini hati ya maneno ya Sh25 milioni.
Pia, washtakiwa hao wasitoke nje ya Jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama. Hata hivyo, mshtakiwa (Bwakea) alikamilisha masharti hayo na kuachiwa huru kwa dhamana na kesi hiyom imeahirishwa hadi Januari 29, 2015.
Kashfa hiyo ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyoibuliwa na Bunge iliitikisa nchi na hadi sasa imesababisha kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kwa kupokea Sh1.6 bilioni kutoka akaunti hiyo.
Pia, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alijiuzulu baada ya azimio la Bunge kutaka awajibishwe na mamlaka yake ya uteuzi akidaiwa kuishauri vibaya Serikali katika suala hilo.
Pia, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi amesimamishwa kazi kwa uchunguzi.
Katika uamuzi wake, Bunge liliagiza watuhumiwa wote wa kashfa hiyo, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye bado ameachwa kiporo na Rais Jakaya Kikwete na wenyeviti wa kamati za Bunge za kisekta wawajibishwe.
Hao ni pamoja na Andrew Chenge anayeongoza Kamati ya Bunge ya Bajeti aliyedaiwa kupokea Sh1.6 bilioni kutoka akaunti hiyo.
Pia, William Ngeleja (Kamati ya Sheria na Katiba) aliyepokea fedha, Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), ambaye pia alikuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco.

Hali kadhalika, tayari watumishi kadhaa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamesimamishwa kutokana na kashfa hiyo.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment