Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 16 January 2015

KASHFA NZITO YAIBUKA BANDARI

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akifafanua jambo mbele ya ujumbe kutoka Wizara ya Uchukuzi pamoja na Mamlaka ya Bandari jana. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe. Picha na Salim Shao 
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeitaka menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kurejesha nyongeza ya fedha zote za malipo ya safari ilizowalipa watendaji wake tangu mwaka 2011, baada ya kubainika kuwa zililipwa bila kuidhinishwa na Msajili wa Hazina.
Ukaguzi maalumu uliofanywa katika mamlaka hiyo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2011/12, unaonyesha kuwa TPA iliomba nyongeza ya malipo ya safari lakini kabla ya kupewa kibali na Msajili wa Hazina, ilianza kuwalipa watendaji wake nyongeza hiyo.
Msajili wa Hazina ametoa kibali cha nyongeza ya malipo hayo ya safari Januari 2, mwaka huu na kwa takriban miaka minne mamlaka hiyo imefanya malipo bila kupewa kibali na Serikali.
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe alisema malipo ya safari kwa wafanyakazi wa ngazi za chini wa mamlaka hiyo kwa siku, awali ilikuwa Sh94,000 na sasa ni Sh123,000 na watendaji wa juu awali ilikuwa Sh270,000 na sasa ni Sh500,000.
Alisema malipo kwa safari za nje watendaji wa ngazi za chini kwa siku, awali walikuwa wakilipwa Dola 296 za Marekani na wa ngazi za juu Dola 600 na kwa sasa wanalipwa Dola 800.
“Tunataka mrejeshe fedha hizi tangu mlipoanza kuzilipa mwaka 2011 maana mlifanya makosa kwani mmelipa bila kupewa idhini na Msajili wa Hazina,” alisema Zitto na kuongeza: “Wote ambao mmewalipa mnatakiwa kuwakata katika mishahara yao.”
Kamati hiyo ilikutana jana na TPA katika ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam kujadili hesabu za mamlaka hiyo kwa mwaka 2011/12.
Akijibu suala hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPA, Madeni Kipande alisema kati ya waliolipwa, wapo waliostaafu, kuacha kazi na kufariki dunia, huku akisisitiza kuwa ukusanyaji wa fedha hizo utakuwa mgumu kwa watu hao.
Hata hivyo, Zitto alijibu: “Hayo mtayaeleza katika taarifa yenu mtakayotuletea kuhusu urejeshaji wa fedha hizo.”
Katika hatua nyingine, kamati hiyo iliibana TPA kutokana na kutokuwa na nyaraka za uthibitisho wa matumizi ya fedha kutokana na kutokuwa na mfumo wa kisasa wa kutunza kumbukumbu na kuitaka kuwasilisha taarifa hizo haraka.
“Ripoti inaonyesha kuwa mmetumia Sh6.4 bilioni kwa ajili ya matangazo, tuliwabana na mmetuletea uthibitisho ila kuna Sh384 milioni matumizi yake hayaonekani,” alisema mjumbe wa kamati hiyo, Abdul Marombwa.
Awali, mamlaka hiyo ilieleza kuwa imetumia Sh9.6 bilioni kwa ajili ya mikutano na kushindwa kuonyesha mchanganuo wa matumizi na baada ya kubanwa ilitoa nyaraka huku zikiwa na pungufu ya Sh686 milioni.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment