Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday 26 January 2015

WABUNGE WABEBA KASHFA YA NBC

 
Na Mwandishi Wetu
KASHFA ya kuuzwa kwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa bei ya kutupwa inayotarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa 18 wa Bunge unaoanza kesho Mjini Dodoma, inatajwa kuwa moja ya ajenda ambazo zitatawala mwenendo wa mjadala wa vikao vya Bunge.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Bunge waliokuwa wakihudhuria vikao vya kamati hizo jijini Dar es Salaam, vilivyoketi kwa muda wa wiki mbili wamesikika wakieleza kuwa wamejipanga kwenda kuibana serikali ili itoe maelezo ya kina ya jinsi NBC ilivyobinafsishwa kwa bei ya chee na pia iwataje maofisa wa serikali waliohusika na ubinafsishaji huo.
NBC iliuzwa kwa Shs. 15 bilioni, fedha ambazo ni ndogo kuliko thamani halisi, kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya fedha.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, zimeeleza kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo hawajaridhishwa na maelezo ya serikali iliyoyatoa kuhusu ubinafsishaji wa NBC, jambo ambalo limeibua hali ya mashaka kuwa huenda wapo viongozi wa serikali waliohusika na sakata hilo ambao wameamua kuficha ukweli.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la jina lake kutotajwa gazetini kwa sababu yeye siyo msemaji, alidokeza kuwa kuna hali ya sintofahamu kuhusu chanzo cha kufisilika kwa NBC kabla ya kubinafsishwa kwa bei ya kutupwa kwa Benki ya ABSA ya Afrika Kusini.
Alisema, wabunge wamehoji na kuomba maelezo ya kina kutoka serikalini kwa muda mrefu pasipo mafanikio huku kwa upande mwingine hali ya uchumi wa taifa ikizidi kuwa mbaya.
“Suala la kuuzwa NBC kwa bei ya kutupwa bado halijafa, serikali imeshindwa kutupa maelezo ya kina ingawa tumekuwa tukiyaomba kwa muda mrefu, sasa tumeamua kwenda na ajenda hii kwenye Mkutano wa 18 wa Bunge kwa sababu mjadala wake haustahili kufa mpaka ukweli halisi ufahamike kwa umma,” alisema Mbunge huyo.
Taarifa nyingine kutoka ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) zimeeleza kuwa wajumbe wa kamati hiyo wameshtushwa na habari walizozipata serikalini zinazoonyesha kuwepo kwa uwezekano wa serikali kupoteza asilimia 30 ya hisa zake inazozimiliki kwenye NBC.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa agizo la kuongezwa kwa mtaji wa NBC ili kufidia hasara iliyoipata na hivyo kuchota akiba yake.
Zilieleza kuwa wakati NBC ikibinafsishwa baada wafanyabiashara wa ndani kuchota mabilioni ya fedha ambayo hawakulipa baada ya kutumia njia za udanganyifu, serikali haikuwa na fedha na ikailazimu kukopa kwa mbia mwenzake ambaye ni Benki ya ABSA ya Afrika Kusini, Shs. 22.5 bilioni kwa riba ya asilimia 8 kwa mwaka ili kuchangia mtaji wake ndani ya benki hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa serikali ilishindwa kulipa deni hilo na ilipewa muda unaoishia mwezi Machi 2015 kuwa imekwishalipa deni lake, vinginevyo itapokwa hisa hizo na hivyo kuifanya NBC kumilikiwa na wageni kwa asilimia 100.
Kabla ya kuibuka kwa taarifa hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, (PAC) Zitto Kabwe alitoa taarifa katika mitandao ya kijamii akieleza kuwa kashfa ya uuzwaji NBC kwa bei ya kutupwa haitaachwa bila kuchunguzwa na ukweli wake kuwekwa wazi.
Akiandika katika mitandao hiyo, Zitto alisema wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) alipendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye uchunguzi maalumu kuhusu benki hiyo jambo ambalo halikuchukuliwa kwa uzito.
Katika andishi lake hilo, Zitto alieleza kuwa mwishoni mwa mwaka jana, Kamati ya PAC anayoiongza ilikutana na watendaji wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ambaye ndiye mmiliki wa mali zote za Serikali kwenye Mashirika ya Umma na  kampuni binafsi ambazo Serikali ina hisa na kujadili uwezekano wa Serikali kupoteza hisa zake katika NBC lakini ufumbuzi wa uhakika haukupatikana.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa wabunge, bado haijafahamika iwapo mjadala kuhusu kashfa ya ubinafsishaji NBC utakuwa katika ratiba ya shughuli za mkutano wa 18 wa Bunge.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamati ya Uongozi ya Bunge chini ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, ilikutana Ofisi Ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam kupanga ratiba ya mkutano wa 18 wa Bunge ambayo inatarajiwa kufahamika kesho.
CREDIT: DIRA YA MTANZANIA

No comments:

Post a Comment