JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MWENENDO WA KAMPENI KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA JIMBO LA CHALINZE
1.0 UTANGULIZI
Ndugu
zangu wanahabari, awali ya yote nawashukuru sana kwa kuitikia wito wa
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Natambua mna majukumu mengi ya
kuhabarisha umma, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu ipo katika
mchakato wa mabadiliko ya katiba na uchaguzi huu mdogo wa Chalinze.
Kwanza
nianze kwa kuvipongeza vyama vyote vya siasa ambavyo vimeweka wagombea
katika uchaguzi huu. Hivi sasa hapa nchini kuna vyama vya siasa ishirini
na moja (21) vyenye usajili wa kudumu na ambavyo kisheria
vinastahili
kushiriki chaguzi zote, lakini vyama vya siasa vilivyofanikiwa kuweka
wagombea ni vitano (5) tu, AFP, CCM, CHADEMA, CUF na NRA. Pongezi hizi
nazitoa kwa kutambua kuwa, kushiriki uchaguzi ni gharama.
2.0 MAJUKUMU YA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KATIKA UCHAGUZI
Kabla
ya kuwaeleza madhumuni ya kuwaita, naomba kwanza nitumie nafasi hii
kuwaeleza majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika
uchaguzi, kwani kuna wadau ambao bado hawaelewi kwa nini Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa ipo katika jimbo la Chalinze na Ofisi hii
inafanya nini katika uchaguzi huu.
Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa
Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za
Uchaguzi namba 7 ya mwaka 2010 katika chaguzi zote ikiwamo chaguzi ndogo
za wabunge na madiwani.
Katika kusimamia
utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa inafuatilia na kutoa adhabu kwa vyama vya siasa vinavyojihusisha
na vitendo vifuatavyo:-
a)Chama ambacho
wanachama na/au mashabiki wake wanajihusisha na vitendo vya fujo, vurugu
na uvunjifu wa amani wa aina yoyote ile;
b)Chama ambacho viongozi na/au wanachama wake wanatumia maneno ya matusi, kashfa na uchochezi; na
c)Chama ambacho kinatumia na/au mgombea wake anatumia mali za Serikali katika kampeni na uchaguzi.
Katika
kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa ina jukumu la kuweka sawa uwanja wa ushindani
katika siasa, kwa kufuatilia na kupendekeza/kutoa adhabu kwa chama cha
siasa na/au mgombea anayejihusisha na masuala yafuatayo.
a)Kutumia
fedha nyingi zaidi ya kiwango kilichowekwa na Sheria katika jimbo
husika. Katika jimbo la Chalinze sheria inasema mgombea asitumie zaidi
ya shilingi milioni hamsini;
b)Uwazi katika
matumizi ya pesa katika kampeni ambapo kila chama, mgombea na taasisi za
kiraia zinazoshiriki katika kampeni, zinatakiwa kutoa taarifa ya fedha
zitakazotumia katika kampeni na uchaguzi na baada ya uchaguzi kuisha,
kutoa taarifa ya fedha zilizotumia katika uchaguzi.
c)Chama
cha siasa au mgombea kushawishi kupigiwa kura au kushawishi wananchi
kuacha kumpigia kura mgombea mwingine kwa kutoa vitu vya thamani kama
pesa, chakula, pombe au ahadi za kupewa cheo au kazi.
d)Matumizi ya mali za Serikali katika kampeni;
e)Vyombo vya habari vya Serikali vinavyopendelea upande mmoja katika kampeni.
Aidha,
jukumu lingine la muhimu sana ni kutoa elimu kwa wananchi, vyama vya
siasa na wagombea, kuhusu wajibu wao na makatazo yaliyomo katika Sheria
tajwa hapo juu.
3.0 MADHUMUNI YA KUONGEA NA WANAHABARI
Ndugu
wanahabari, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeona sasa ni wakati
muafaka wa kufanya tasmini ya kampeni zinavyofanyika katika jimbo la
Chalinze, kwani tumeshavuka nusu ya muda wa kampeni na umebaki muda wa
wiki moja tu, ambao kwa maneno ya mitaani naweza kusema ni muda wa lala
salama.
Hivyo, tumewaita katika mkutano huu kwa madhumuni yafuatayo:
a)Kuwafahamisha
wananchi kupitia kwenu kazi zilizofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya Siasa tangu kampeni za uchaguzi mdogo wa Chalinze zianze mpaka sasa;
b)Kuwafahamisha
wananchi tathimini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu
mwenendo wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Chalinze; na
c)Dhumuni jingine la kuwaita ni kuwaeleza shughuli iliyopo mbele yetu mapaka siku ya uchaguzi.
4.0 KAZI ZILIZOFANYWA MPAKA SASA
Ndugu
wanahabari; Kazi kubwa zilizofanywa na maafisa wa Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa tangu kampeni za uchaguzi wa Chalinze zianze ni
zifuatazo:-
a)Kutoa elimu kwa umma kwa
wananchi, vyama vya siasa na wagombea kuhusu wajibu wao na makatazo
yaliyomo katika Sheria ya Vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi;
b)Kuonana na wadau wa uchaguzi kupata maoni na malalamiko kuhusu kampeni; na
c)Kufuatilia
taarifa na malalamiko ya uvunjifu wa Sheria tajwa hapo juu, ili kujua
ukweli na kuwaasa wahusika wajirekebishe, wasipojirekebisha kuchukua
hatua za stahiki.
Mpaka sasa tumeonana na
wagombea vyama vinne, CUF, CCM, CHADEMA na NRA, bado mgombea mmoja wa
AFP ambaye tunaendela kuwasiliana naye.
5.0 TATHMINI YA KAMPENI KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA CHALINZE
Ndugu
wanahabari, mpaka sasa kampeni zinaendalea vizuri, ila kuna malalamiko
na vitendo vichache vya uvunjifu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria
ya Gharama za Uchaguzi, ambavyo kimsingi malalamiko mengi na vitendo
vingine vinahitaji uchunguzi wa kina.
Baadhi ya
vyama vya siasa vimealalamikia vitendo vya kuingiliwa na wafuasi au
wanachama wa chama kingine katika mikutano yao ya kampeni, mabango yao
kuchanwa, bendera kushushwa, viongozi, wanachama na wafuasi wao kupigwa
na ununuzi wa shahada za mpiga kura. Aidha, kumekuwa na matumizi ya
maneno ya kashfa na dhihaka katika majukwaa ya kampeni.
Kimsingi,
ikiondoa matumizi ya maneno za kashfa na dhihaka jukwaani, ambayo
yanasikika kwa watu waliopo na muongeaji anaonekana na vitendo vya
wanachama na mashabiki wa chama kuingilia mkutano wa kampeni wa chama
kingine, vitendo vingine vinahitaji uchunguzi wa kina wa taasisi husika,
ili kujua wahusika na mazingira ambayo kitendo husika kimetokea, kwa
lengo la kuchukua hatua stahiki.
Kwa upande
wake, Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa inaendelea kufuatilia malalamiko
iliyopata kutoka kwa vyama vya siasa na wagombea, ili kupata undani wake
na kujiweka katika mazingira mazuri ya kuchukua hatua stahiki. Ni vyema
wananchi wakaelewa kuwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ipo makini
na ufuatiliaji wa masuala ya vyama vya siasa kuvunja Sheria
inazozisimamia hasa wakati wa uchaguzi. Ila haiwezi kuchukua hatua
stahiki kwa chama husika bila kuwa na ushahidi wa kutosha kuwa, chama
hicho kimehusika na kitendo hicho cha uvunjifu wa sheria.
Ndugu
waandishi wa habari, natumia nafasi hii pia kusisitiza kuwa, ahadi
aliyoitoa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Francisi S.K.
Mutungi, kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatafuta mwarobaini
wa vurugu katika kampeni, haikuwa utani wala ahadi hewa. Kwani uzoefu
tunaoupata katika chaguzi hizi ndogo unatusaidia katika kutengeneza
mwarobaini huo.
6.0 WITO WA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KWA VYAMA VYA SIASA NA WAGOMBEA
Ndugu
zangu wanahabari, kwa kuzingatia mwenendo wa kampeni na ukweli kuwa,
kampeni huwa kubwa na pilika nyingi wiki ya mwisho kuelekea siku ya
uchaguzi, naomba nitumie nafasi hii kuviasa vyama vya siasa na wagombea
wote katika uchaguzi huu mdogo wa Chalinze ifuatavyo:-
a)Kuepuka
kutumia maneno ya matusi, kashfa na mambo yanayofanana na hayo, badala
yake wanadi sera zao, kwani licha ya kuwa maneno ya matusi na kashfa ni
kinyume na sheria na maadili, lakini wananchi wanahitaji kulikiliza sera
si matusi na kashfa;
b)Kuepuka vitendo vya
vurugu na uvunjifu wa amani, kwani licha ya kuwa vinaleta madhara kwa
watu na mali zao, lakini pia vinawaogopesha wananchi kushiriki kampeni
na hata kwenda kupiga kura;
c)Kutochukua hatua za kisheria mkononi, badala yake wakiona au kusikia mtu kavunja sheria watoe taarifa katika vyombo husika;
d)Kutojihusisha na vitendo vya uchokozi mfano kuingilia mikutano ya kampeni ya chama kingine;
e)Kutojihusisha na vitendo vyovyote vya rushwa, mfano kununua au kuuza shahada ya mpiga kura;
f)Kutoa taarifa kwa vyombo husika ili zifanyiwe kazi, badala ya kutoa tu kwa wanahabari na kulalamika;
g)Kuepuka propaganda ambazo zinawatia hofu wananchi na wapiga kura.
Aidha,
Waandishi wa habari waepuke kutoa taarifa bila kuzifanyia uchunguzi
ikiwamo kupata maoni ya upande wa pili, kwani kufanya hivyo kunaweza
kuwapa hofu wananchi wa nchi nzima na wapiga kura ikiwa taarifa
iliyotolewa ni ya kuogofya wakati si ya kweli.
7.0 KAZI ZILIZO MBELE YETU
Siku
za kampeni zilizobaki, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imejipanga
kuendelea kutekeleza majukumu yake niliyoyataja hapo juu, isipokuwa siku
ya uchaguzi tarehe 06 Aprili, 2014, Ofisi imejipanga kushirikiana na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufuatilia chama cha siasa na
wagombea wanaofanya mambo yalikatazwa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi,
ikiwamo kubeba wapiga kura katika vyombo vya usafiri kuwapeleka au
kuwatoa katika vituo vya kupiga kura.
8.0 FAIDA YA UWEPO WA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KATIKA CHAGUZI MBALIMBALI
Ndugu
waandishi wa habari; naomba nitumie nafasi hii pia kuwaeleza faida za
uwepo wa Ofisi ya Msajili ya Vyama vya Siasa katika chaguzi mbalimbali
hasa chaguzi ndogo.
Uwepo wa Ofisi ya Msajili
wa Vyama vya Siasa katika chaguzi mbalimbali unasaidia uchaguzi
kufanyika vizuri, kwa amani na utulivu na wananchi kuchagua viongozi
wanaowataka kwa namna zifuatazo:-
a)Kwa
kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Ofisi vya
Msajili wa Vyama vya Siasa inasaidia kuweka uwanja sawa wa ushindani
katika uchaguzi kwa kuepusha matumizi makubwa ya fedha katika kampeni,
kuweka uwazi katika matumizi ya fedha na rasilimali nyingine katika
kampeni na kuepusha matumizi ya mali za Serikali katika kampeni.
b)Kwa
kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Ofisi vya Msajili
wa Vyama vya Siasa inasaidia kuepusha vitendo vya vurugu, matusi na
uchochezi kwa kuchukua hatua stahiki kwa chama kinachohusika kwa mujibu
wa Sheria.
Aidha, kitendo cha maafisa wa Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwepo tu katika kampeni, kinawatia hofu
wanasiasa na vyama vya siasa vyenye lengo la kuvunja sheria, kwani
wanaelewa fika kuwa, Ofisi ya Msajili ipo na inafuatilia. Hivyo, uwepo
wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kampeni za uchaguzi
hupunguza sana vitendo vya uvunjifu wa sheria nilizozitaja hapo juu.
9.0 MWISHO
Namalizia
kwa kutoa wito kwa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huu kuelewa
kuwa, vinawajibu wa kisheria wa kuwaasa na kuwadhibiti wanachama na
wagombea wao kuheshimu na kufuata Sheria zote zinazohusika. Hivyo, kila
chama kitekeleze wajibu wake, ili uchaguzi huu unafanyike kwa amani na
utulivu. Nawaomba pia wanachi wa Chalinze waendelee kuhudhuria mikutano
ya kampeni ya vyama vya siasa bila hofu na woga. Aidha, washawishike kwa
hoja na sio rushwa. Watoe taarifa kwa vyombo husika pale wanapoona mtu
yeyote anajihusisha na vitendo vya uvunjifu wa Sheria na wajitokeze kwa
wingi siku ya kupiga kura.
Asanteni kwa
kunisikiliza na ninawatakia kazi njema katika kazi yenu ya kuwahabarisha
wananchi kuhusu kampeni za uchaguzi wa Chalinze.
Sisty L. Nyahoza
Kny: MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
30 Machi, 2014