Dodoma/Dar. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema atafurahi kuona mchakato mzima wa Katiba ukikamilika kabla rais mpya hajapatikana katika Uchaguzi Mkuu ujao, pendekezo ambalo ni kinyume na makubaliano baina ya Rais Jakaya Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kuwa upigaji wa kura ya maoni ufanyike baada ya Uchaguzi Mkuu 2015.
Akizungumza Bungeni baada ya kupewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta kutoa shukrani, Pinda alipendekeza kura ya maoni ipigwe sambamba na Rais ili kiongozi ajaye afanye kazi ya kutekeleza matakwa ya Katiba hiyo.
Alisema rais ajaye anaweza kuwa na ajenda zake, hivyo ni muhimu kumaliza kazi yote na kumkabidhi Katiba ambayo imekamilika ili aitekeleze.
“Nampongeza sana mwenyekiti kwa kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha Katiba inayopendekezwa inapatikana kwa wakati na kwa kuzingatia maoni ya wananchi,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
Alichojifunza
Pinda alieleza kuwa katika mchakato huo wa Mabadiliko ya Katiba, amejifunza mambo makuu manne, kubwa likiwa ni kutii sauti ya wengi, kwani ni sauti ya Mungu. Alisema wingi wao bungeni ni kiashiria cha uwepo wa sauti ya Mungu.
Alisema umoja wao bungeni ni silaha muhimu iliyofanikisha hatua zote zilizowezesha kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa, bila kujali pingamizi kutoka kwa watu waliojaribu kukwamisha mchakato huo.
“Nawaomba sasa kwa umoja wetu huu, twende nao kwa wananchi ili kueleza kuwa kazi waliyotutuma tumeikamilisha na wao watuunge mkono katika kura ya maoni,” alisema.
Alisema amevutiwa zaidi na Sura ya Pili ya Katiba hiyo kwa sababu imechukua malengo makubwa ya kitaifa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kisera. Aliwapongeza Wazanzibari akisema wasiwasi wa wengi ulikuwa kukosekana kwa theluthi mbili kutoka kwa wajumbe wa upande huo wa pili wa Tanzania. “Nimetambua kuwa wote wanajenga Taifa moja na wao ni wamoja,” alisema.
Ulinzi na usalama
Pinda alisema suala la ulinzi na usalama ni ajenda ya Taifa hili na kwamba anashangaa kuona baadhi ya watu wakikaa na kupanga kuvuruga amani ya nchi kwa masilahi binafsi.
Alisema maridhiano ndiyo njia pekee inayoweza kuleta suluhu baina ya pande mbili zinazotofautiana kimawazo na siyo kwenda kufanya vurugu kama wafanyavyo baadhi ya wajumbe waliosusia Bunge hilo.
Bunge lahitimishwa
Akihitimisha Bunge hilo Mwenyekiti wake Samuel Sitta, alisema Rais Jakaya Kikwete na Dk Ali Mohammed Shein wamekubali kuwa shughuli ya kuzipokea Katiba ifanyike Jumatano ijayo.
“Watapokea nakala ya Katiba inayopendekezwa hapa Dodoma katika sherehe maalumu,” alisema na kuongeza kuwa Rais pia amekubali kila aliyeshiriki mchakato huo na kufikia mwisho atapewa cheti.
Sitta pia alizishukuru kamati zote 12 zilizohusika katika kuboresha Rasimu na kutengeneza Katiba inayopendekezwa ambayo alisema imebeba maoni ya wananchi.
Walichosema wengine
Baadhi ya wajumbe waliopewa nafasi ya kuzungumza wamewapongeza viongozi wa Bunge la Katiba; Mwenyekiti, Samuel Sitta na Makamu wake Samia Suluhu Hassan, pamoja na Kamati ya Uandishi iliyoongozwa na Andrew Chenge kwa kufanya kazi hiyo ngumu, bila kujali walivyoshambuliwa.
Mjumbe Hamad Rashid alisema kuna baadhi ya watu walisema wao wana kura za Wazanzibari na kuwa walipendekeza Serikali ya mkataba. Hata hivyo, alisema, matokeo yaliyotolewa ndiyo yamebainisha nani ni Wazanzibari na Serikali gani wanaitaka.
“Katiba inapatikana kisheria, ndiyo maana tumekuwa hapa kuifanya kazi hiyo. Sasa hawa wenzetu waendelee kupiga kelele wenyewe. Sasa ni wazi kuwa sauti ya watu wa Kibanda Maiti imesikika katika matokeo haya,” alisema Rashid.
Mjumbe mwingine, Stephen Wasira alisema: “Wapo waliosema wao ndiyo wanawasemea wananchi lakini waliondoka humu ndani sasa wanakwenda kusemea wapi. Wengine wakasema tutakutana mtaani sawa, tutakutana huko maana ndiko tunakoishi,” alisema Wasira.
Aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho aliwapa pole Sitta na Samia kwa kupitia changamoto nyingi kuliko ilivyokuwa wakati wake.
Alisema anakumbuka wakati wake alizushiwa kuwa anarefusha mjadala wa kuandaa kanuni ili ajikusanyie fedha nyingi za posho ya Sh7 milioni kwa siku, jambo ambalo alikanusha na kusisitiza kuwa alilipwa posho kama wajumbe wengine.
Mjumbe John Shibuda alisema hakutaka kuwa sehemu ya wasaliti ndiyo maana alishiriki kikamilifu katika kutengeneza historia ya Taifa. Alisema ni heri kuitwa msaliti kuliko kuwa mhaini wa Watanzania.
Askofu Donald Mtetemela alipinga matamko yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari kuwa hayakuwa ya maaskofu kwa sababu hayakusainiwa na maaskofu wote kama ambavyo hufanyika mara zote wakitoa tamko.
Alisema yalikuwa maoni ya mtu binafsi na si maoni ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) au Makanisa ya Kipentekoste (PCT).
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment