Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday, 30 October 2014

MSIBA MZITO: ZAMBIA YAPOTEZA RAIS WA PILI AKIWA MADARAKANI!

Marehemu Michael Sata

Na Isaya Kisimbilu
Zambia imeendelea kukumbwa na mkasa wa kufiwa na marais wake wakiwa bado madarakani, baada ya Rais Michael Sata (77) kufariki dunia  jijini London, Uingereza alikokuwa amelazwa kwa  matibabu.


Sata anakuwa ni Rais wa pili wa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu barani Afrika  kufariki jana akiwa madarakani.Ni  baada ya Rais wa awamu ya tatu, Levy Mwanawasa, kufariki dunia Julai 3 mwaka 2008 kwa mshtuko wa moyo.

Baadhi ya marais wengine barani Afrika ambao walifariki wakiwa bado madarakani ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Ghana, John Atta Mills Julai 2012 akiwa na miaka 68.
Pia  Rais wa Malawi, Profesa Bingu wa Mutharika  naye alifariki Aprili 2012 akiwa na umri wa miaka 78.

Akizungumza kuhusu msiba huo, Katibu wa Bunge la Zambia, Rowland Msiska, alisema, Sata alifariki jana asubuhi kwenye Hospitali ya King Edward VII London nchini  Uingereza alikokuwa amelazwa kwa matibabu takribani wiki moja iliyopita.

Awali  vyombo vya habari viliripoti kuwa, kabla ya kufikwa na mauti hayo,  Rais Sata aliruhusiwa kutoka hospitalini alikokuwa amelazwa  nchini Uingereza.

BALOZI WA ZAMBIA AZUNGUMZAAkizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Balozi wa Zambia nchini, Judith Kangoma Kapijimpanga,  alisema alipata  taarifa ya msiba huo  jana asubuhi baada ya saa tatu kupita na kwamba taratibu za kuurejesha mwili nchini Zambia kwa ajili ya mazishi zinaandaliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Uingereza na Ubalozi wa Zambia uliopo jijini London.

Hata hivyo, hadi taarifa za msiba huo zinasambazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, bado haikuwekwa bayana  kuhusu ugonjwa aliokuwa anaugua wala jina la hospitali alikokuwa amelazwa.

Sata ni Rais wa tano nchini humo akitanguliwa na Keneth Kaunda, Fredrick Chiluba, Levy Mwanawasa na Rupiah Banda.

Kabla ya kiongozi huyo, kufariki dunia, kulikuwapo na wasiwasi kuhusiana na hali yake ya afya  kuanzia aliposhindwa kuonekana hadharani kuanzia Juni mwaka huu kabla ya kuondoka nchini humo ghafla wiki moja iliyopita akiwa ameambatana na mkewe na watu wengine wa karibu na familia yake baada ya hali yake kuwa mbaya.

Hali ya wasiwasi iliongezeka baada ya Sata kutoonekana hadharani katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Zambia wiki iliyopita. Waziri wa Sheria wa nchi hiyo, Edgar Lungu, aliongoza sherehe hizo.

Kufuatia taarifa hiyo, Katibu huyo wa Bunge la Zambia, Msiska, alitoa wito wa kuwapo kwa utulivu nchini humo na kwamba taarifa ya mipango ya mazishi itatolewa hivi karibuni.

Jana Shirika la Habari la Kimataifa la CNN, lilisema kuwa anayekaimu nafasi hiyo kwa sasa ni Makamu wake, Guy Scotty.

MTANZANIA RAFIKIYE AZUNGUMZAAkizungumza na NIPASHE jana, rafiki wa karibu wa kiongozi huyo, Mchungaji Florence Temba, alisema, Sata alikuwa na msimamo wa kutetea maslahi ya wengi kwani baada ya kushika kiti hicho, alirudisha taasisi za fedha zilizouzwa kinyemela ikiwamo benki ya nchi hiyo iliyokuwa imebinafsishwa kwa wawekezaji wa Afrika Kusini.

Mchungaji Temba, ambaye ni kiongozi wa Kanisa la Penueli Healing Ministry, lililopo jijini Dar es Salaam, alisema, Sata akiwa Rais, alisaidia kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na kuokoa thamani ya fedha ya nchi hiyo kwa kuondoa Kwacha ya noti ya 100, 000  na kuweka ya noti ya 1,000.

Kadhalika, alisema Rais Sata katika uongozi wake, mbali na kuwashusha vyeo baadhi ya maafisa polisi nchini umo ambao walikuwa wamepandishwa vyeo kinyume na utaratibu, alianzisha mradi wa kuwajengea nyumba askari wa jeshi la nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Temba, alisema Sata aliwajali sana wanawake  nchini humo kwa kuwapa nafasi za juu zikiwamo za ubalozi na Spika wa Bunge.“Sata ni Rais wa wengi. Sata alikuwa ni kama baba yangu. Alikuwa ni mzee wa misimamo akitetea wananchi. Amekura rais mara baada ya mara nne kushindwa,” alisema Mchungaji Temba ambaye pia alifanikiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake kuwa Rais wa nchi hiyo.

HISTORIA YAKERais Michael Sata alizaliwa mwaka 1937 katika eneo la Mpika lililopo Kaskazini mwa nchi hiyo.Alianza kazi kwa mara ya kwanza akiwa afisa wa polisi na baadaye kuwa  mfanyakazi wa reli kabla ya kuwa mwanachama wa chama cha wafanyakazi nchini humo.

Baada ya Uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa Waingereza mwaka 1964, Sata alijiunga na chama tawala cha muungano wa kitaifa wa Uhuru ‘ United National Independence Party’ na kuwa gavana wa mji mkuu wa nchi hiyo, Lusaka, katika miaka ya 80.

Enzi hizo alijulikana kwa uchapakazi wake  kwani alikuwa akichangia katika kusafisha barabara yeye mwenyewe.Hata hivyo, baadaye akajitenga na Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Kenneth Kaunda, baada ya kupatikana uhuru na kujiunga na vuguvugu la demokrasia ya vyama vingi ‘ Movement for Multi-Party Democracy (MMD).

Vuguvugu hilo linadaiwa kuchangia kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1991.

Chini ya Serikali ya MMD, Sata alishika nafasi za uwaziri katika  wizara za Serikali za Mitaa, Kazi, Afya na Waziri asiyekuwa na wizara maalumu.
Mwaka 2001 aliunda chama chake cha Patriotic Front, ambacho kilimpa kushinda kwa takribani asilimia 42 ya kura  katika  Uchaguzi Mkuu mwaka 2011 nchini humo.

Sata alijulikana kwa jina la Utani kama ‘king cobra’ kutokana na kuwakemea mawaziri wake hadharani na kumuita Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush, kuwa kijana mdogo aliye mkoloni wakati alipochelewa kuwasili katika mkutano wao.

Hata hivyo, anadaiwa kushutumiwa na wakosoaji wake kwa madai ya kuongoza kimabavu na kuukandamiza upinzani na vyombo vya habari.

JK AMLILIARAIS Jakaya Kikwete ameelezea kushtushwa na kusononeshwa na taarifa za kifo cha Rais Sata.Hayo yamo katika  salamu za rambirambi alizomtumia Makamu wa Rais wa Zambia,  Dk. Guy Scott kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rais Kikwete baada ya kupokea taarifa za kifo hicho.

Kikwete, alisema amepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi.

“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hakika, kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kukutumia wewe Mheshimiwa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu, na kupitia kwako familia ya wafiwa na ndugu wa Sata  na Serikali na ndugu zetu wananchi wote wa Zambia kufuatia msiba huu wa ghafla,” alisema katika taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais.

Rais Kikwete alisema  Sata atakumbukwa daima kama mmoja wa viongozi wa mfano wa kuigwa barani  Afrika na kwamba katika kipindi kifupi cha uongozi wa juu wa Zambia, alifanikiwa kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya raia wa nchi hiyo.

Alisema pia atakumbwa kwa imani yake isiyoyumba ya kupigania Uhuru, haki na usawa, sifa zilizomfanya kupendwa ndani na nje ya mipaka ya Jamhuri ya Zambia.

“Huyu ni kiongozi ambaye siyo tu atakumbukwa na wananchi wa Zambia lakini atakumbukwa na sisi sote wenzake na watoto wote wa Afrika.”

Alisema anaungana na familia ya kiongozi huyo na wananchi wa Zambia katika kipindi  kigumu cha majonzi na huzuni, maombolezo na kumwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu ili waweze kuhimili machungu.

Alisema: "Tuko pamoja nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema roho ya Marehemu   Sata."
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment