Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday, 27 October 2014

NAPE ABEZA USHIRIKIANO WA UKAWA

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akifafanua jambo. Picha na Maktaba 
Na Boniface Meena, Mwananchi
Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema hatua ya viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuingia katika makubaliano ya kushirikiana “ni kaburi la vyama hivyo.”
Wakati Nape akisema hayo, baadhi ya wasomi wamesema ni hatua kubwa lakini yenye kuhitaji kuwa na sera na itikadi ya pamoja. Akizungumza kwa simu jana, Nape alisema Ukawa ni kaburi la vyama vya upinzani vilivyoungana kwa kuwa vitapoteza utambulisho wao.
“Huu ni mwanzo wa kumomonyoka kwa vyama vya upinzani, moja vyama hivyo vitapoteza identity (utambulisho) zao na kama mkutano wenyewe ndiyo umehudhuriwa na watu kidogo vile, basi hali yao ni ngumu sana,” alisema Nape.
Alisema kutakuwa na mgogoro mkubwa hasa kwenye nafasi za kugombea kwa kuwa hasa katika majimbo akitolea mfano wa Jimbo la Ubungo ambalo alisema Julius Mtatiro wa CUF anataka kugombea huku John Mnyika wa Chadema naye akitaka kutetea nafasi yake.
“Ukawa ni bomu ambalo litawalipukia na kwangu sijaona jambo jema kwa ushirikiano huo,” alisema Nape.
Hata hivyo, Nape alisema jambo moja ambalo vyama hivyo vimelifanya ni kuunganisha nguvu kupambana na CCM ambayo misuli yake ni mikubwa.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitila Mkumbo alisema ushirikiano huo ni hatua kubwa kwa kuwa angalau umeweza kuainisha mambo ambayo watashirikiana.
Hata hivyo, Profesa Mkumbo alisema hiyo iwe ni hatua ya kwanza kushirikiana na hatua ya pili iwe ni kwa vyama vya upinzani kuungana kabisa na kuwa chama kimoja kiitikadi na kifalsafa ili kuweza kuwa na vyama viwili vikubwa nchini.
“Nilidhani wangekuwa na sera ya kuweza kuchambua tofauti za kiitikadi ndani ya vyama na kuja na vipaumbele vya msingi katika nchi, lakini ushirikiano huo unaonekana ni wa kimadaraka zaidi,” alisema Profesa Mkumbo.
Alisema itikadi za vyama ni muhimu kuzingatiwa kwa kuwa ni jambo la msingi katika kuunda Serikali. “Ukiangalia Chadema wao itikadi yao ni ya kibepari, CUF ni kiliberali na NCCR-Mageuzi ni ujamaa, sasa wakiunda serikali itakuwa ya itikadi gani? Hili ni jambo la kujiuliza,” alisema.
Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk Benson Bana alisema si jambo baya lakini kinachohitajika ni kujulikana wamejenga ushirikiano huo kwa msingi gani.
“Hamuwezi kuungana kwa sababu ya kwenda Ikulu. Tunahitaji wawe na itikadi ya aina moja na sera za mbadala ingekuwa ni jambo jema zaidi,” alisema Dk Bana na kuongeza: “Wakubaliane sera za mambo mbalimbali ambayo yataweza kuing’oa CCM na si kujiwekea mkakati wa kugawana madaraka.”
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment