Na Florence Majani, Mwananchi
Dar es Salaam. Hali ni mbaya katika Hospitali ya saratani ya Ocean Road (ORCI), Dar es Salaam kutokana na uhaba mkubwa wa dawa.
Wagonjwa wengi waliolazwa katika hospitali hiyo kwa nyakati tofauti wamesema wameshuhudia wenzao kadhaa wakipoteza maisha kwa kuwa taasisi hiyo haina dawa.
Mmoja wa wagonjwa aliyekuwa amelazwa kutokana na saratani ya utumbo, Miriam Obadia kutoka Geita, alikata roho mbele ya mwandishi wa habari wa gazeti hili aliyeingia katika Wodi namba 322 huku kukiwa na taarifa kwamba alikosa dawa.
Muuguzi ambaye hakutaka kutaja jina lake kutajwa gazetin, alisema mgonjwa huyo alifariki dunia kwa kukosa dawa ambazo hazipo hospitalini hapo. “Ndugu zake waliambiwa wakanunue nje lakini hadi leo hawajamletea na hapa sisi hatuna dawa anazohitaji.”
Mwandishi alijaribu bila mafanikio kuwatafuta ndugu zake ambao walikuwa wameondoka kwenda kutafuta fedha za kununua dawa hizo.
Mkurugenzi wa Tiba wa ORCI, Dk Diwani Msemo alithibitisha kuwapo kwa uhaba mkubwa wa dawa katika taasisi hiyo. “Hilo halina ubishi, ni kweli kuwa tuna uhaba wa dawa, ni tatizo kubwa na lipo nje ya uwezo wetu.”
Akizungumza kwa tabu, mmoja wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Miyana Mushi, aliyelazwa katika wodi namba 321 alisema ameshindwa kupata dawa za saratani ya koo alizoandikiwa mwezi mmoja uliopita baada ya kuambiwa kuwa zimekwisha hospitalini hapo.
“Sasa hivi natapika damu na usaha, siwezi kula wala kunywa chochote kwa sababu koo linauma sana. Mwanangu amejaribu kuulizia dawa nilizoandikiwa katika maduka ya dawa lakini tumeshindwa kununua kutokana na kukosa fedha.”
Ili Mushi aweze kupona, anahitaji dozi nzima ambayo katika maduka ya dawa inauzwa Sh3.5 milioni, fedha ambazo alisema hawezi kuzimudu.
Gharama za dawa
Imebainika kuwa dawa zinazotakiwa kwa ajili ya wagonjwa wengi zinapatikana kwenye maduka ya dawa lakini kikwazo ni bei.
Katika baadhi ya maduka, bei ya baadhi ya dawa walizoandikiwa wagonjwa katika hospitali hiyo hazishikiki. Mathalan, tiba ya saratani ya damu kwa watoto kwa dawa iitwayo 1/M asparafinase 20,000IV ni kati ya Sh900,000 na milioni moja kwa dozi moja. Kwa mtoto hata kama ni wa mwaka mmoja huhitaji dozi 12 ili apone.
Dawa za bei ya chini kabisa za saratani kwa mfano, Finesteride na Menthotrexate ambazo ni za kutuliza tu maumivu zinagharimu kiasi cha Sh20,000 kwa dozi.
Kadhalika, imebainika kuwa mbali na uhaba wa dawa, mashine ya mionzi ya ORCI pia imeharibika kutokana na kutumika zaidi ya uwezo wake.
Akizungumzia suala hilo Dk Msemo alisema: “Ni kweli mashine ni mbovu. Tunasubiri mafundi kutoka Canada watakuja kuitengeneza, tunawatarajia wakati wowote.”
Kauli za wagonjwa
Baadhi ya wagonjwa waliorudishwa nyumbani kwa kukosa huduma ya mionzi walisema wameambiwa watapigiwa simu pindi mashine itakapopona.
“Nina saratani ya kizazi, ninatokwa damu kila siku, nimeambiwa mashine mbovu na sijui hatima yangu ni nini kwa sababu naumwa sana, tena sana... Serikali itusaidie jamani tutakufa,” alisema Zuhura Kigobe, mkazi wa Nyamagana, Mwanza.
Kigobe pamoja na wenzake wenye saratani za aina mbalimbali walirudishwa nyumbani tangu Agosti mwaka huu na hawajui hatima yao hadi sasa.
Takwimu kutoka ORCI zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa wa aina hiyo inaongezeka kwa kasi kutoka wagonjwa 2,807 mwaka 2006 hadi 5,384 mwaka jana.
Mkurugenzi wa takwimu wa ORCI, Dk Julius Mwaiselage alisema ongezeko kubwa la maradhi ya saratani linatokana na mfumo wa maisha.
Wizara ya Afya
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja alisema kuwa kuna uhaba mkubwa wa dawa katika hospitali nyingi nchini lakini na kwamba Serikali inatafuta fedha... “Lakini inawabidi wasubiri kwa sababu hata Serikali nayo imepungukiwa fedha ndiyo maana hatujapeleka fedha (Bohari Kuu ya Dawa) MSD.” Alisema suala la ORCI ni zito na linaitatiza Serikali kwani taasisi hiyo haina chanzo chochote cha fedha na inajiendesha kwa kuitegemea Serikali kwa asilimia 100.
“Pale wagonjwa wanatibiwa bure na tiba yao gharama ni kubwa kwa mfano mgonjwa mmoja wa saratani huweza kutibiwa kwa Sh2 milioni, ndiyo maana kuna changamoto kubwa katika suala hilo kwa kweli,” alisema Mwamwaja.
Hata hivyo, alisema kwa sasa wametoa kipaumbele kwa taasisi hiyo ili ipate mgawo mkubwa zaidi wa dawa kutokana na unyeti wa ugonjwa huo, sambamba na kufungua kanda katika baadhi ya mikoa nchini.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment