Na Beatrice Moses, Mwananchi
Dar es Salaam. Vigogo wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika akiwamo Katibu Mkuu Sophia Kaduma, wametimuliwa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) baada ya kutoa majibu yasiyoridhisha.
Vigogo hao walikuwa wameitwa mbele ya kamati hiyo kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusiana na hati isiyoridhisha, waliyopewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
CAG alitoa hati hiyo baada ya kugundua kuwa taarifa za fedha za wizara hiyo, hazikuandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Uhasibu.
Pia wakiwa ndani ya kikao cha PAC, vigogo hao walishindwa kutoa majibu ya kuridhisha kuhusu deni la Sh4 bilioni linalotokana na mauzo ya mbolea ya Minjingu na namna walivyojipanga kuwasaidia wakulima kuuza mahindi yao.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe awali alimuhoji Kaduma akitaka kujua jinsi gani wanavyotoa vibali vya kuingiza mchele kutoka nje ya nchi, wakati wakulima wamezalisha zao hilo kwa kiwango kikubwa.
“ Kwanza kabla ya yote nataka kujua wizara inatumia utaratibu gani katika kutoa vibali vya kuingiza mchele kutoka nje, wakulima wetu wanaumia kwa sababu inasemekana wapo wafanyabiashara wanaochanganya mchele huo na kuharibu soko la mchele wa ndani,”alihoji Kabwe.
Pia jambo lingine ni kwamba hayo mahindi ya ziada yaliyozalishwa kwa wingi nchini mnawasaidiaje wakulima katika kutafuta soko.
“Maana nyie mnaonekana mnakaa ofisini mnaendelea kupokea mishahara huku wakulima wakiwa wanateseka, nani wa kuwasaidia kama siyo nyie,” alisema Kabwe.
Kaduma alitoa maelezo kuwa kwa sasa wizara inatoa vibali vya kusafirisha mahindi na mchele nje ya nchi na siyo kuingiza, na kwamba hana taarifa kama kuna mchele kutoka nje ya nchi unaouzwa nchini.
Jibu hilo liliwakera wajumbe hao na Mbunge Zainab Kawawa alimjia juu na kumuhoji kazi yake ni nini kama hawezi kujua kuwa kuna mchele kutoka nje unaouzwa nchini, anataka nani amfanyie kazi hiyo.
Hali hiyo ilisababisha Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Karimu Mtambo kutakiwa atoe majibu, ambapo katika maelezo yake kwa kamati hiyo, alikiri kwamba kuna mchele kutoka nje ya nchi lakini unaingizwa bila kibali.
“ Wizara haitoi vibali vya kuingiza mchele huo, lakini kuna wafanyabiashara ambao wanauingiza kwa njia za panya wakipitia Zanzibar, jambo hili hata waziri aliomba msaada wa vyombo vya dola ili kudhibiti,” alisema.
Awali Kaduma pia alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la vyakula vya nafaka hasa mpunga na mahindi, kwani matarajio yalikuwa tani milioni 12 lakini zimezalishwa tani milioni 16.
“Hali hiyo imesababisha tuwe na chakula cha ziada cha tani zaidi ya tani milioni tatu, lakini soko la ndani halijitoshelezi kwa hivyo katika mkakati wa kutafuta soko, tunatoa vibali kwa wafanyabiashara kwenda kuuza nchi jirani ikiwemo Kenya,” alisema Kaduma.
Kaduma alikiri kwamba wizara yake ina hati isiyoridhisha ya CAG, kwa sababu ya kukosekana kwa nyaraka za deni la Sh2.1 bilioni.
“Tunakubali kweli kuna udhaifu uliotokana na utunzaji wa nyaraka kutokuwa mzuri, lakini tayari nyingine zimepatikana, ni madeni ya muda mrefu, kwa sasa tumetakiwa kuthibitisha nyaraka za fedha za Sh1.2 bilioni na siyo Sh2 bilioni.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment