Na Kalunde Jamal, Mwananchi
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inaelekeza nguvu katika kutangaza utalii wa ndani ili kuvutia watalii wengi kutoka nje ya nchi.
Akifungua maonyesho ya kwanza ya utalii (SITE) jana, Rais Kikwete alisema ili kuvutia watalii ni lazima kuwekeza fedha katika masuala mbalimbali ya sekta hiyo, hasa huduma bora, usafiri wa uhakika na malazi.
Alisema bila kufanya hivyo ni vigumu kwa watalii kuja nchini kwa kuwa watakaoondoka hawatakuwa mabalozi bora wazuri wa nchi.
Alisema njia nyingine ya kuvutia watalii ni kujitangaza na kila mmoja kujivunia Uafrika na Utanzania wake kwa kuwa wageni wengi wanafahamu Afrika ni moja na hawaelewi uwapo wa Afrika Mashariki.
Alisema vyombo vya habari vinatakiwa kupaza sauti kutangaza utalii badala ya kutangaza majanga ya njaa, maradhi, migogoro na machafuko, jambo linalowaaminisha watalii kuwa nchi zote za Afrika zina matatizo hayo.
Alisema endapo vyombo vya habari vitatangaza utalii wa Tanzania na kuutofautisha nchi za Kiafrika, ni lazima watalii watafahamu kuwa kuna nchi za Afrika hazina njaa, machafuko na baa la njaa.
Alisema licha ya kuwapo kwa changamoto kadhaa, lakini nyanja ya utalii inaendelea kufanya vizuri ikiwamo kuongezeka kwa watalii kulingana na takwimu za mwaka 2013.
Rais alisema mwaka 2012 watalii wa kimataifa walioingia nchini walikuwa 1,077,058 na mwaka 2013 waliongezeka na kufikia 1,095,885.
Alisema kutokana na watalii kutembelea nchini, mwaka 2012 Serikali iliingiza Dola za Marekani milioni 1,712.7 na mwaka 2013 pato hilo liliongezeka na kufikia Dola milioni 1,853.28.
Alisema kungekuwa na ongezeko kubwa zaidi kama kusingekuwa na mtazamo tofauti kuhusu Afrika miongoni mwa watalii kutoka nje ya bara hilo, hasa wanaposikia kuna maradhi kama ugonjwa wa ebola.
Alisema ni vyema kufafanua kuhusu bara la Afrika ili kuondoa dhana kwa watalii kuwa Afrika ni moja na kufanya hivyo watalii watakuwa wengi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, (TTB), Charles Sanga alisema maonyesho hayo yamepata mafanikio kwani licha ya kwamba ni mara ya kwanza wamepata washiriki zaidi ya 60 jambo linaloashiria kwamba watafika mbali.
Sanga aliitaja gharama waliyotumia kuandaa maonyesho hayo kuwa ni Sh 800 bilioni ambazo alisema zitazaa matunda kulingana na maendeleo ya maonyesho hayo.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment