Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday, 12 July 2015

KOMBE LA KAGAME: YANGA WALIKWENDA UGANDA KWA MELI WAKARUDI KWA NDEGE, SIMBA WALIKWENDA KWA NDEGE WAKARUDI KWA MELI 1993


Kikosi mahiri cha Yanga. Kuanzia wa pili kutoka kushoto ni Daktari wa timu Sheki Mngazija, kipa Riffat Said, Said Mwamba 'Kizota', Willy Martin, Willy Mtendawema, Selemani Mkati, Issa Athumani 'Amiri Jeshi', Mtwa Kihwelu 'Dally Kimoko', Method Mogella 'Fundi', Steven Mussa, Mohammed Hussein 'Mmachinga', Abubakar Salum 'Sure Boy', Edibily Lunyamila, Zamoyoni Mogella 'DHL', David Mwakalebela 'MP', Steven Casmir Nemes na Kenneth Pius Mkapa.
Yanga ikipambana nchini Uganda mwaka 1993. Pichani ni Zamoyoni akihangaika uwanjani.


Na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com

MWAKA 1993 mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati yalifanyika jijini Kampala, Uganda ambapo Tanzania Bara iliwakilishwa na mabingwa watetezi, Simba SC pamojana mabingwa wa Bara, Yanga.
Mtandao wa www.brotherdanny.com unaendelea kuwaletea uchambuzi wa kihistoria katika mashindano haya wakati tukielekea kwenye michuano ya mwaka huu ambayo itaanza Jumamosi hii jijini Dar es Salaam.

Mwaka huo 1993 Yanga iliweka historia katika mashindano hayo kwa kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutwaa ubingwa huo katika ardhi ya kigeni, lakini pia iliweza kuwanyanyasa wenyeji itakavyo kiasi kwamba mpaka leo wachezaji kama Edibily Lunyamila na Said Mwamba Kizota bado wanakumbukwa huko.
Ni mwaka huo pia ambapo mchezaji ghali aliyetokea Simba, Zamoyoni Mogella ‘Morgan’, alipachikwa jina la ‘DHL’ akifananishwa na kampuni ya usafirishaji wa vifurushi. Hii ilitokana na umahiri wake wa kutoa pasi za uhakika kwa wenzake pamoja na kuiunganisha vyema timu.
Timu hii kwanza iliondoka kwa mizengwe baada ya kukosa fedha za kuisafirisha hadi Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, alipojitolea kuisafirisha.
Yanga ilisafiri kwa treni mpaka Mwanza, ambako ilipanda meli mpaka Jinja kabla ya kujipakia kwenye basi lililowapeleka Kampala. Wafadhili wa Yanga, Abbas Gulamali, Murtazar Dewji, Muhsin Hassanali, Mohammed Virani 'Babu' na Ramesh Patwa walikuwa wameweka 'ka-mgomo baridi'.
Tofauti na Yanga, Simba wenzao, wakiwa na mfadhili wao mkuu, Azim Dewji, walikwenda Kampala kwa kutumia ndege ya kukodi, ambayo iliwachukua kutoka Mwanza hadi Kampala.
Kichekesho kilikuwa wakati wa kurudi. Simba, ambayo ilitolewa mapema baada ya kufungwa na Express ya Uganda na kuvuliwa ubingwa, iliondoka kwa njia iliyokujia Yanga; yaani ilipanda basi mpaka Jinja kisha ikatumia usafiri wa boti hadi Mwanza kabla ya kukwea gari moshi lililowafikisha Dar es Salaam. Yanga wao walirejea kwa ndege moja kwa moja kutoka Kampala.
Kwa ujumla mashindano ya mwaka huo yalikuwa hayatabiriki kutokana na kushirikisha timu zenye uzoefu mkubwa na mashindano ya kimataifa.
Wasifu wa timu hizo zilizoshiriki, ambazo zilikuwa nane ingawa moja ilijitoa, ni kama ifuatavyo:
BATA BULLETS (Malawi): Ilikuwa klabu bingwa ya Malawi kwa mwaka 1992 na ndiyo ilikuwa moja ya timu mbili kubwa nchini humo. Nyingine ni Limbe Leaf Wanderers. Timu hii mashuhuri mjini Blantyre ilikuwa inashiriki mashindano haya kwa mara ya sita, ingawa haikuwahi kutwaa ubingwa mpaka sasa. Ilipata kushiriki mwaka 1976, 1979, 1982, 1987 na 1992. Mwaka huu ilikuwa na wachezaji sita mashuhuri wa timu ya taifa ya Malawi, kama golikipa George Waya, mlinzi Gilbert Chirwa, kiungo Mabvuto Lungu (nahodha), winga Chancy Gondwe na washambuliaji Brian Maulidi na Lawrence Waya.
EL-HILAL (Sudan): Hii ilikuwa El-Hilal ya 'bushi' kutoka Port Sudan na siyo ile maarufu ya Omdurman. Hata hivyo, ndiyo iliyokuwa klabu bingwa ya Sudan mwaka 1992. Nayo pia ilikuwa timu maarufu nchini humo na ilikuwa na wachezaji kadhaa katika timu ya taifa.
MALINDI (Zanzibar): Ndiyo iliyokuwa klabu bingwa ya Zanzibar na ilikuwa ikishikilia ubingwa wa Jamhuri ya Muungano baada ya kuinyang'anya Yanga mwaka 1992. Malindi ilikuwa inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano haya baada ya kutofanyika mwaka 1990, ambapo pia ilikuwa bingwa wa Zanzibar. Mwaka 1993 ilikuwa na wachezaji kadhaa mashuhuri wa timu ya taifa ya Zanzibar, kama vile, Seifu Bausi, Rashid Tall, Ally Bushiri (kipa), Hamad Hilika, Juma Bakari Kidishi na Amour Aziz.
EXPRESS (Uganda): Ilikuwa mshindi wa pili wa ligi na bingwa wa Kombe la Uganda. Timu hii ndiyo yenye wapenzi wengi kuliko zote nchini humo. Iliimarika zaidi wakati wa amani baada ya kuvunjwa na utawala wa Idd Amin Dada, ambaye aliamini kuwa klabu hiyo ilikuwa ikitumiwa na kabila la Baganda kumhujumu. Ilipata kushiriki mashindano haya mwaka 1975, 1976 na 1988. Express ilikuwa na wachezaji sita katika timu ya taifa ya Uganda iliyoifunga timu ya pili ya Tanzania Bara, Kakakuona, mjini Mwanza katika mchezo wa fainali ya Kombe la Chalenji mwishoni mwa mwaka 1992. Wachezaji hao ni George Ssemogerere, Robert Aloro, Umar Senoga, Issa Sekatawa, Richerd Kirumila na Issa Sewanyana.
SIMBA (Tanzania): Ndiye aliyekuwa bingwa mtetezi. Ilikuwa inatetea taji lake kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanikiwa kulitetea huko Zanzibar mwaka 1992. Simba ndiyo ilikuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa huo mjini Dar es Salaam, mwaka 1974. Safari hii ilikuwa inashiriki kwa mara ya kumi baada ya mwaka 1974, 1975, 1977, 1978, 1980, 1981, 1985, 1991 na 1992. Ilikuwa na wachezaji watatu kwenye timu ya taifa, golikipa Often Martin, Abuu Omar na Mbuyi Yondani.
VILLA SC (Uganda): Ndio waliokuwa mabingwa wa Uganda. Ni timu ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikitamba sana na kutawala ligi nchini humo kwa miaka kadhaa. Timu hii ilianzishwa wakati wa utawala wa Idd Amin baada ya kuvunjika kwa Express ambayo Amin hakuipenda. Imewahi kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na kati mwaka 1987 wakati mashindano hayo yalipofanyika Uganda kwa mara ya mwisho kabla ya mwaka 1993. Safari hii ilikuwa inashiriki kwa mara ya saba baada ya kushiriki katika miaka ya 1983, 1985, 1987, 1988, 1989 na 1991. Villa, ambayo mwaka 1991 ilifikia fainali za Klabu Bingwa Afrika na mwaka 1992 ilifikia fainali za Kombe la CAF, ilikuwa na wachezaji wazuri nchini humo, ambao ni Paul Hasule, William Nkemba, Suleiman 'Sula' Katto, Godfrey Higenyi na Idd Batambuze.
YANGA (Tanzania): Ilikuwa klabu bingwa ya Tanzania Bara na mojawapo ya timu mbili mashuhuri nchini Tanzania, lakini ikiwa na wapenzi wengi kuliko zote. Kabla ya wakatihuo, iliwahi kuwa bingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1975. Mwaka 1993 ilikuwa inashiriki kwa mara ya nane baada ya kushiriki katika miaka ya 1975, 1976, 1982, 1984, 1986, 1988 na 1992. Ilikuwa na wachezaji sita kwenye timu ya taifa, ambao ni nahodha wa timu ya taifa, Salum Kabunda, Willy Martin, Edibily Lunyamila, Willy Mtendawema, Said Mwamba 'Kizota' na golikipa Riffat Said.
NKANA RED DEVILS (Zambia): Siyo tu ilikuwa klabu bingwa nchini Zambia, bali pia ilikuwa klabu 'numero uno', yaani nambari wano, nchini humo, ambapo hata Rais wa nchi hiyo, Frederick Chiluba, alikuwa mmoja wa wapenzi wake wakubwa. Nkana, ambayo wakati huu ilikuwa klabu ya kulipwa, ilikuwa inaumiliki ubingwa wa Zambia kama mali yake na mwaka 1990 ilifikia fainali za Klabu Bingwa Afrika. Mwaka 1993 ilikuwa inashiriki kwa mara ya tatu mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati. Ilipata kushiriki mwaka 1984 na 1985 na ilikuwa na wachezaji mashuhuri wa timu ya taifa ya nchi hiyo, kama Eston Mulenga, Kelvin Mutale na Numba Mwila, ambaye baadaye alifariki kutokana na ajali ya ndege. Hata hivyo, timu hii ilijitoa katika dakika za mwisho.
Hizo ndizo timu zilizokuwa zinashiriki mashindano hayo, ambayo 'yalimwinua mnyonge (Yanga) kutoka mavumbini' na kutwaa ubingwa kwa mara ya pili baada ya kipindi cha miaka 18, huku watani wao wa jadi, Simba, wakiwa hoi.
Timu hizo zilikuwa katika makundi mawili; kundi A lilikuwa na Yanga, Villa na Malindi baada ya Nkana kujitoa, na kundi B lilikuwa na Simba, Express, El-Hilal na Bata Bullets.
Sasa tuangalie namna mashindano hayo yalivyoendeshwa Januari 16 hadi Januari 30, Yanga walipotawazwa kuwa mabingwa. Michezo ya Nkana sitaiandika humu kwa kuwa timu hiyo ilijitoa.

Wafungaji:
Mbali ya Yanga kutwaa ubingwa, pia mshambuliaji wake hatari, Said Mwamba Kizota alichaguliwa kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo baada ya kuzifumania nyavu mara sita. Pia alichaguliwa kuwa nambari 9 bora wa mashindano.
Katika ufungaji, Kizota alifuatiwa na Mathias Kaweesa wa Villa aliyefunga mabao matano. Issa Sekatawa wa Express alifunga mabao manne wakati Mabvuto Lungu wa Bata Bullets alifunga mabao matatu. Waliofunga mabao mawili kila mmoja ni George Akena (Villa) na Robert Aloro (Express), wakati waliofunga bao moja kila mmoja ni Edward Chumila (Simba), Amour Nassoro (Malindi), Chancy Gondwe (Bata Bullets), David Odowa (Express) na Mohammed Hussein na Edibily Lunyamila (Yanga).

Kundi A
16/01/1993: Nakivubo Villa 1-0 Malindi
Mfungaji: Mathias Kaweesa 65’

20/01/1993: Nakivubo Villa 3-1 Yanga
Wafungaji: George Akena sekunde ya 30, Mathias Kaweesa 23’ na 57’/ Said Mwamba Kizota 45’

22/01/1993: Yanga 2-1 Malindi
Wafungaji: Said Mwamba 78’, 82’/ Amour Nassoro pen. 31’

 1.Nakivubo Villa  2  2  0  0  4- 1  4  [Uganda]
 2.Yanga                 2  1  0  1  3- 4  2  [Tanzania]
 3.Malindi              2  0  0  2  1- 3  0  [Zanzibar]

Kundi B
17/01/1993: Express FC 2-2 Bata Bullets
Wafungaji: Robert Aloro 4’na Issa Sekatawa 40’/Mabvuto Lungu 8’ na Nelson George 66’

19/01/1993: Simba SC 1-0 Hilal
Mfungaji: Edward Chumila 53’

21/01/1993: Express FC 2-0 Hilal
Mfungaji: Issa Sekatawa 3’, 13’

21/01/1993: Bata Bullets 0-0 Simba SC

23/01/1993: Bata Bullets 2-0 Hilal
Wafungaji: Mabvuto Lungu 10’ na Chancy Gondwe 17’

25/01/1993: Express FC 2-0 Simba SC
Wafungaji: David Odowa 63’ na Issa Sekatawa 72’

 1.Express FC      3  2  1  0  6- 2  5  [Uganda]
 2.Bata Bullets    3  1  2  0  4- 2  4  [Malawi]
 3.Simba SC        3  1  1  1  1- 2  3  [Tanzania]
 4.El Hilal            3  0  0  3  0- 5  0  [Sudan]

Nusu fainali
27/01/1993: Nakivubo Villa 3-0 Bata Bullets
Wafungaji: Mathias Kaweesa 12’, 63’, Mzee Josam og. 26’

28/01/1993: Express FC     1-3 Yanga
Wafungaji: Robert Aloro 88’/Said Mwamba 10’, 31’ na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ 18’

Mshindi wa tatu:
30/01/1993: Express 0 vs Bata Bullets 1
Mfungaji: Mabvuto Lungu 110’

Fainali
30/01/1993: Yanga 2-1 Nakivubo Villa
Wafungaji: Said Mwamba 6’ na Lunyamila 44’/ George Akena 2’.


KUMBUKUMBU HIZI ZIMEANDALIWA NA MTANDAO WA www.brotherdanny.com. Tafadhali ukirejea weka chanzo cha habari.

No comments:

Post a Comment