Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 30 July 2015

NA WAPO MALAYA WA KISIASA, TUJIHADHARI!

Ikulu ya Tanzania

Na Daniel Mbega

TAFSIRI ya Kiswahili sanifu ya ‘ukahaba’ au ‘malaya’ inaelezwa kwamba ni tendo la kufanya ngono nje ya ndoa au uhusiano unaokubalika katika jamii, tena na watu mbalimbali na kwa malipo. Sifa ya umalaya au ukahaba imekuwa ikinasibishwa zaidi na wanawake hasa kwa vile wanaume wamekuwa wakidai kuwa wao ni wa wake wengi kwa asili.
Kwa bahati mbaya katika miaka ya karibuni maana ya maneno hayo imetoka katika asili kutokana na ama kupanuka kwa lugha ya Kiswahili au jamii kuzalisha maneno mengine mapya, ndiyo maana hata mwanasiasa ambaye hatulii na chama kimoja, mwenye kubadili vyama kama ‘nguo za ndani’, amekuwa akiitwa ‘malaya’.
Neno ‘malaya’ ndilo kuntu linaloweza kuelezea tabia za wanasiasa wanaohama vyama kama nyumba za kupanga ingawaje neno hilo limeanza kupotea taratibu na limebaki kuwa ni msamiati unaotumiwa zaidi na wazee ambao, kwa sababu zilizo wazi, hawawezi kutumia lugha za msimu na hapa kwenye lugha za msimu ndiyo tunakuja kwenye maana ya neno kirukanjia.
Kirukanjia ni malaya au ukipenda kahaba. Hili limetokana na jina la ndege aitwaye ‘kirukanjia’ au ‘mbarawaji’. Neno ‘njia’ limetumika kumaanisha mtu mwenye kubadilisha njia kila mara. Ni neno la msimu au la mtaani.
Kwa maelezo hayo mafupi ni kwamba niko sahihi kabisa kuwaita wanasiasa wanaobadili vyama kila wakati ni ‘malaya wa siasa’, ambao kimsingi tabia zao hazina tofauti kabisa na malaya au makahaba wenyewe wanaozungumziwa katika tafsiri halisi.
Wahenga wanasema, umalaya wa siasa umekuwepo ulimwenguni pengine tangu kuanzishwa kwa Siasa yenyewe. Umalaya wa kisiasa unaweza kutajwa kwamba ni "hali ya kutoa huduma au dhamana ya uongozi kwa nia ya rushwa, kwa minajiri ya kupata maslahi ya kimwili au rasilimali".
Kwa hiyo basi, wanasiasa wa aina hii ambao wako tayari kuuza ushawishi wao na madaraka ya kwa nia ya kupata maslahi binafsi wanatambulika kama Malaya wa Kisiasa.
Umalaya ndiyo fani ya kwanza kabisa duniani, na siasa ndiyo fani ya pili na zote zinafanana. Siasa na umalaya ndizo kazi pekee ambazo kukosekana kwa uzoefu kunaonekana kama ndiyo kunaonekana kama ndiyo talanta, na siyo ajabu hata wanaofanya kazi ya ukahaba wanaweza kudanganya kwamba ni ‘bikira’ ili kuwavutia wateja wao wakati siyo kweli!
Sikiliza kisa hiki. Mzee mmoja tajiri alikutana na binti mbichi akamtamani, akamwambia angempatia Shilingi milioni moja kama angekubali kulala naye kwa usiku mmoja tu. Binti yule akatafakari kwa muda, halafu akasema “Hakuna taabu”. Sasa mzee akamwambia, “Unaonaje ikiwa nitakupa Shilingi elfu tano?” Yule binti akamaka, “Hivi wee babu umenionaje mimi?” Badala yake yule mzee akasema, “Tayari tumeshajua wewe ni nani. Sasa tunapatana bei.”
Tabia za wanasiasa malaya hazina tofauti na malaya anayefanya ngono, ambaye daima lazima amsifie mwanamume aliyenaye sasa kwamba ni bora kuliko yule aliyekuwa naye. Wanaume nao kwa ulimbukeni wao wa asili, hujiona ufahari wakati tayari wamekwishaibiwa!
Naam. Tanzania tunao malaya wa kisiasa, wengi sana, kama ilivyo katika nchi nyingine ulimwenguni. Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, tumeshuhudia wanasiasa wengi wakiondoka kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwenda upinzani. Hawa walikuwa na kila sababu ya kufanya hivyo, kwani ilikuwa ni lazima watoke kwenye chama kimoja waende wakaanzishe vyama vingine.
Lakini kuibuka kwa wanasiasa malaya kumekuwa kukijitokeza kila unapofika mwaka wa uchaguzi. Tumeshuhudia hayo kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 na tunaendelea kushuhudia hata sasa. Wanatoka CCM wanakwenda upinzani, wanakitukana chama tawala, halafu baadaye wanarejea na kuutukana upinzani!
Wakati vyama vya siasa vikiendelea kupanga safu za wagombea wao mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, tayari wameibuka wanasiasa malaya ambao wamehama vyama vyao, siyo kwa sababu ya kukerwa na sera za vyama hivyo, la hasa. Bali kwa sababu wanaamini wakienda kwenye vyama vingine watapatiwa nafasi ya kugombea uongozi. Yale yale ya makahaba wa kweli!
Ukiwachunguza wanasiasa wengi, kama siyo wote, ambao wamebadili itikadi zao katika kipindi hiki, utakubaliana nami kwamba ama walikuwa hawana uhakika kama watapitishwa na vyama vyao au wamepoteza mvuto wa kisiasa kwa wananchi waliokuwa wakiwaongoza na sasa wanataka kutumia mwavuli wa nguvu za vyama ‘vipya’ kurejea tena madarakani.
Wanapokimbilia upande wa pili, wanasiasa hawa makahaba wamekuwa na tabia zile zile za kukashfu kule walikotoka, wakijinasibu kwamba walikuwa wanapambana na hiki na kile lakini hawakusikilizwa, sasa wanaona bora wajiondoe na kwenda upande mwingine ambako ‘sera zao zinakubalika’.
Madhara ya wanasiasa wa aina hii yameonekana mara nyingi sana hapa nchini. Wapo ambao huko walikotoka walionekana kuwa na nguvu, wakapokelewa upande wa pili na kupewa dhamana, lakini matokeo yake wengi walianguka vibaya na hata wale walioshinda chaguzi mbalimbali, baadaye wakageuka shubiri kwa madai ya uasi. Tumewaona, sina haja ya kuwataja hapa.
Ni kwa mukhtadha huo – sina uwezo wa kuzuia, lakini nina uwezo wa kushauri – naona kwamba vyama viwe makini na wanasiasa hawa, ambao nalazimika kuwaita ‘ni makapi’, kwa sababu wanaweza wasiaminike kama wamefuata sera ama wanatafuta ngazi ya kuendelea kupata neema ya uongozi.
Kuwakumbatia wanasiasa wa aina hii, japokuwa ni haki yao ya kidemokrasia, ni kuhatarisha upinzani wa kweli kwa sababu naamini siyo wote wenye mtazamo chanya wa mageuzi bali wanatafuta maslahi binafsi. Kutoa siri za kule watokako kunamaanisha kwamba hata wakija kuondoka huko walikokimbilia pia watazitoa siri hizo!
Upinzani unaimarika nchini, tunapenda uwe na nguvu na ikibidi uongozi halmashauri na kuwa na sauti kubwa Bungeni, lakini kama mtaji wa vyama vya upinzani utakuwa kuchukua ‘makapi’, ambayo mengi ni ya CCM, uwezekano wa kutimiza ndoto hizo utakuwa mdogo.
Hivi tu niwaulize hao wanasiasa wanaoona muda mzuri wa kuondoka ni kipindi cha uchaguzi, kwa nini, kama kweli wanataka mabadiliko, hawakuondoka kabla? Kwa nini, kwa mfano wabunge wanaomaliza muda wao, hawakuondoka katikati kama tulivyomshuhudia Zitto Kabwe?
Wangu ni ushauri tu, utekelezaji ni kwa wahusika wenyewe.
Msemea sikioni, siyo majinuni!
Wasaalam.
0656-331974


 IMECHAPWA MARA YA KWANZA NA GAZETI LA WAJIBIKA JULAI 27, 2015

No comments:

Post a Comment