Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, Shaffin Sumar na Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Lucy Mayenga.
Na Hastin Liumba, Uyui
WAGOMBEA tisa wa jimbo la Tabora Kaskazini wamemwandikia barua Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Uyui mkoani Tabora wakimlalamikia mbunge aliyemaliza muda wake Shaffin Sumar kutoa rushwa ya pikipiki na baiskeli kwa makatibu kata na makatibu tawi.
Madai hayo katika barua hiyo ambayo gazeti hili ina kopi yake ya mwezi Juni 21, 2015 yana kichwa cha habari kisemacho Malalamiko ya rushwa dhidi ya Sumar kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Tabora Kaskazini.
Barua hiyo ambayo imesainiwa na wagombea tisa kati ya kumi walisema Mbunge aliyemaliza muda wake Shaffin Sumar siku chache kabla mchakato wa chama wa nafasi ya ubunge aligawa pikipiki kwa makatibu kata 17 kati ya 19 wa jimbo hilo.
Wanasema makatibu wawili hawakupewa pikipiki hizo ambao ni wa kata ya Ikongolo na Bukumbi wakidaiwa hawamuungi mkono.
Aidha madai kwenye barua hiyo wanasema licha ya makatibu hao kupewa pikipiki hizo hazina kadi licha ya kuonekana zimesajiliwa TRA lakini haijulikani kama zina majina yao au mtu binafsi.
Walisema hali hiyo inamaanisha kuna mazingira ya rushwa kwa makatibu wanaomuunga mkono na wasiomuunga mkono.
Kuhusu ugawaji wa baiskeli walisema Sumar aligawa baiskeli kwa makatibu tawi wa CCM na viongozi wote wa jumuiya za UVCCM,UWT na WAZAZI siku chache kabla ya mchakato kuanza.
Aidha kama ilivyo kwenye pikipiki aliwanyima baiskeli hizo wale wote ambao hawamuungi mkono na walionyesha msimamo.
Aidha barua hiyo inasema kutokana na hayo mchakato wa uteuzi wanaona kanuni za uchaguzi toleo la Februari 2010 Ibara namba 33 (2) inazuia mgombea au kiongozi yoyote wa chama kufanya vitendo vya rushwa katika mchakato.
Wanasema kanuni za uchaguzi CCM ibara namba 33 (13) inadhihirisha kwa kufanya vitendo vya kukiuka kanuni za uchaguzi kama zinavyoelekeza.
Hivyo wanasema malalamiko yao yajadiliwe na vikao husika na yatolewe uamuzi kabla ya kupiga kura ya uteuzi.
Wanasema pikipiki hizo endapo zimetolewa kwa mlango wa CCM basi kadi zote zikabidhiwe kwa katibu wa CCM wilaya ya Uyui.
Aidha barua hiyo inasema makatibu wote walionyimwa pikipiki hizo nao wapewe huku makatibu waliopewa pikipiki hizo kama ni zao binafsi basi wakabidhiwe kadi zao za pikipiki na suala hilo lisiwekwe la Ku-Perform kwanza wakati kura za uteuzi ndipo wapewe.
Madai mengine makatibu tawi na jumuiya zake walionyimwa nao wakabidhiwe kabla ya kura ya uteuzi.
Kutokana na madai hayo wagombea hao tisa wanatamka hawana imani makatibu kata waliokabidhiwa pikipiki, makatibu wa jumuiya na tawi ambao watasimaia kura za uteuzi.
Hivyo wanaomba mamlaka husika kuchukua hatua dhdi ya Shaffin Sumar kuvuruga kanuni ibara ya 33 (2) na Ibara namba 33(13) za kanuni za uchaguzi.
Wanasema hatua zichukuliwe dhidi ya Sumar kama ibara namba 34 ya uchaguzi ya CCM inavyosema ambapo wanaweka pingamizi dhidi ya mgombea huyo kugombea ubunge 2015.
Barua hiyo nakala imekwenda pia kwa katibu wa CCM mkoa Janeth Kayanda na kamati ya maadili na usalama CCM makao makuu Dodoma.
Gazeti hili lilimtafuta Shaffin Sumar kuelezea sakata hilo alisema hawezi kutamka chochote anasubiri maamuzi ya sehemu husika.
Katibu wa CCM wilaya ya Uyui Innocent Nanzabar alisema barua hiyo bado haijamfikia ezani kudai kwa sasa hawezi kutoa ufafanuzi.
No comments:
Post a Comment