BASATA Arts Centre
Tel. 2863748/2860485
Fax: 0255- (022) – 286 0486
Ilala Sharif Shamba
P.O. Box. 4779, Dar es Salaam
E-mail:basata06@yahoo.com
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa nchini
linawakumbusha wasanii wote nchini kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na
taratibu zilizopo wanapokwenda nje ya nchi kufanya maonesho au kushiriki
shughuli yoyote ya Sanaa ili kuepuka matatizo na mikanganyiko mbalimbali inayoweza
kujitokeza.
Kwa
mujibu wa taratibu zilizopo, msanii yeyote anapokwenda nje ya nchi anapaswa
kujaza fomu maalumu inayotolewa na BASATA na baadaye kupewa kibali bure (bila
gharama yoyote) ambacho mbali na kueleza wapi msanii anaelekea kinaeleza kwa
kina tarehe ya kuondoka kwa msanii na ile ya kurudi nchini.
Kutokana
na kukua kwa sekta ya Sanaa nchini hususan muziki na filamu wasanii wengi
wamekuwa wakipata fursa ya kwenda nje ya nchi kufanya maonesho na shughuli
zingine za Sanaa hivyo suala la kufuata sheria, kanuni na taratizu za kupata
vibali vya kwenda nje ya nchi ni muhimu sana ili kuhakikisha kwanza; safari zao
zinakuwa na baraka ya moja kwa moja kutoka Serikalini, pili kusaidia
upatikanaji wa takwimu sahihi za wasaniii wanaokwenda nje ya nchi, tatu usalama
wa wasanii wetu na mwisho, kuwakabidhi bendera ya taifa kama ishara ya
uwakilishi na ubalozi wa nchi yetu katika mataifa wanayoyatembelea.
BASATA
limekuwa likiwaelekeza wasanii wote kuomba vibali vya kwenda nje ya nchi na kuripoti
katika balozi zetu zilizoko kwenye mataifa mbalimbali ili kuhakikisha wanakuwa
na wenyeji katika nchi husika kwa lengo la kujitambulisha pia kupata msaada
pale kunapotokea tatizo lolote linalohitaji utatuzi wa Serikali.
Dunia
imekuwa na matukio mengi ya kiusalama ni vema kuchukua tahadhari hasa ikizingatiwa
kazi za Sanaa huambatana na mikusanyiko mikubwa ya watu hali ambayo inaweza kuzaa
matatizo kwa wasanii wetu wakiwa nje ya nchi bila kuwa na nyaraka stahiki.
Baraza
la Sanaa la Taifa linatambua kwamba wasanii wanapokwenda nje ya Tanzania kwa
lengo la kufanya kazi ya Sanaa wanakwenda kuipeperusha bendera ya Taifa letu,
kwa mantiki hii ni mabalozi wa nchi. Hivyo basi, lazima wawe wazalendo,
wajivunie utanzania na kuiwakilisha vyema nchi yetu.
Ieleweke
kwamba Serikali inafarijika na kupata heshima kubwa inapoona wasanii wetu
wakivuka nje ya mipaka na kwenda kupata mafanikio kwenye majukwaa ya kimataifa suala
ambalo ni kuitangaza Tanzania kupitia Sanaa na Utamaduni baada ya kuzingatia
taratibu zote. Ndiyo maana kupitia mitandao yake ya kijamii na hata katika
programu ya Jukwaa la Sanaa BASATA
limekuwa likihamasisha wadau wa Sanaa kuwaunga mkono wasanii na kuwapigia kura
kunapokuwa na shindano lolote linalohitaji ushindi wa kura (popular vote).
Aidha, BASATA limekuwa likiandika taarifa kwenye vyombo vya habari kumpongeza
msanii yeyote anapofanya vizuri nje ya mipaka ya nchi yetu.
Ni
sababu hii ndiyo imelifanya BASATA muda wote kuwasisitiza wasanii na menejimenti
zao kutambua wajibu wao kwa serikali hasa katika kuhakikisha wanafuata taratibu
zote zilizopo na kutoa taarifa hitajika serikalini ili kuepuka mikanganyiko na
sintofahamu inayoweza kujitokeza.
Lengo
ni kuhakikisha kupitia taarifa sahihi zinazokuwa zimetolewa na menejimenti za
wasanii au wasanii wenyewe pia kupitia taarifa zilizopo kwenye vibali vya
kwenda nje kwa wasanii husika, Serikali nayo inajipanga ipasavyo katika
kuhakikisha wasanii wetu wanaagwa na baadaye kupokelewa kwa heshima wanaporejea
nchini.
BASATA
linaamini kwamba haileti picha nzuri na kwa kweli inashusha morali wasanii wetu
wanaporudi nyumbani na mafanikio makubwa pasi na mapokezi ya Kiserikali kwa
sababu tu menejimenti za wasanii zinashindwa kujipanga kwa maana ya kuzingatia
taratibu zilizopo na kutoa taarifa stahiki za lini msanii atarejea na wakati
gani ili mamlaka husika ifanye utaratibu wa mapokezi.
Serikali
kupitia BASATA imefanya mapokezi stahiki kwa wasanii Peter Msechu aliposhinda
shindano la Tusker Project Fame, Mtunzi wa filamu Timoth Konrad wakati filamu
yake ya ‘Dogo Maasai’ iliposhinda tuzo nchini Marekani na hivi karibuni
imefanyika kwa Msanii Mayunga aliyeshinda shindano la Airtel Tracing Star.
Aidha, washiriki wote wa mashindano ya urembo wamekuwa wakifanyiwa hivyo kama
ilivyo kwenye sekta ya michezo.
BASATA
linatoa wito kwa wasanii kudumisha upendo baina yao na kuhakikisha wanakuwa na
ushirikiano pia mawasiliano ya karibu na Serikali muda wote kwani zipo mamlaka
ambazo zipo kwa ajili ya kusimamia sheria, kanuni na taratibu katika tasnia ya
Sanaa.
Ni
wazi kwamba kama wadau wote wa sanaa wakielewa utaratibu huu basi sekta ya
Sanaa ambayo kiasili ni ya upendo, mshikamano na amani itaendelea kukua katika
mwenendo mwema na kuwa yenye tija zaidi kwa wasanii wenyewe pamoja na jamii kwa
ujumla. Wasanii tudumishe upendo, amani na mshikamano.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU
MTENDAJI
No comments:
Post a Comment