Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday, 22 July 2015

HUYU NDIYE MGOMBEA URAIS WA CHADEMA 2015

Mbunge wa Kahama, James Lembeli akizungumza na
Mbunge wa Kahama, James Lembeli akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akitangaza kujiunga rasmi na Chadema, Dar es Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman 

Na Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar/Mikoani. Baada ya vuta vikuvute ya muda mrefu, hatimaye leo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kumtangaza mgombea wake wa urais katika mkutano maalumu utakaofanyika jijini Mwanza.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na viongozi wa chama hicho Kanda ya Ziwa Magharibi na makao makuu zilisema kuwa leo mgombea huyo atatangazwa mkoani hapa huku zikibainisha kuwa anayepewa nafasi kubwa ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa.
Taarifa hizo zimekuja wakati kukiwa na tetesi kuwa chama hicho kilikuwa kinafanya mazungumzo na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyekuwa anawania urais kupitia CCM na kutemwa katika hatua za awali, huku vyanzo mbalimbali vikisema mazungumzo hayo yanachukua muda mrefu na kuna uwezekano mkubwa wa kutozaa matunda.
Jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na baadhi ya wabunge walikaririwa wakitoa matamko ya kumkaribisha Lowassa kuingia Chadema lakini kwa sharti la kufuata kanuni na taratibu za chama hicho, lakini Dk Slaa alisita kumzungumzia kiongozi huyo akiahidi kuzungumza mambo yatakapokuwa sawa.
Mratibu wa Operesheni za Chadema Kanda ya Ziwa Magharibi, Tungaraza Njugu alisema mgombea huyo (bila kumtaja jina), atatangazwa katika mkutano wa hadhara utakaofanyika kwenye Viwanja vya Magomeni, Ilemela kuanzia saa nane mchana.
Njugu alisema katika mkutano huo, viongozi wakuu wa Ukawa wanatarajia kuwapo na maandalizi yake yamekamilika.
“Kesho (leo) tutakuwa na mkutano mkubwa kwenye viwanja vya Magomeni,” alisema Njugu na kuongeza: “Mgombea urais kupitia Ukawa atajulikana hapo, kwani tunatarajia viongozi wakuu wa Ukawa watamtangaza.”
Katika mazingira tofauti, akihutubia mkutano wa hadhara mjini Geita juzi, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alidokeza jina la Dk Slaa kama mgombea urais wa chama hicho, kitendo kilichoibua hamasa na umati kumshangilia, lakini akawapoza akisema ulimi umeteleza.
Alipoulizwa kuhusu mkutano huo, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikiri kuwa leo kulikuwa na mpango wa kumtangaza mgombea wa Ukawa, lakini alidhani ingekuwa Dar es Salaam, hivyo kwa kuwa wameamua iwe Mwanza angefanya utaratibu wa ndege ili aweze kuwahi.
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia hakupatikana kuzungumzia mkutano huo, lakini Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe alisema hakuwa na taarifa hizo, hasa kwa kuwa vikao vya mwisho vilivyofanyika Jumapili na Jumatatu vilihusisha wenyeviti wa vyama pekee.
Hata hivyo, alisema ilibidi mgombea huyo atangazwe ama jana au leo. Chama cha CUF kimekwishatangaza kuwa kinasubiri uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi litakaloketi Julai 25 kuamua juu ya hatima yake ndani ya Ukawa.
Alipotakiwa kudokeza ni nani atasimama kuwakilisha Ukawa, Njugu alisema jukumu hilo ni la viongozi wa juu na kwamba yeye akiwa kiongozi wa Kanda anatambua mgombea urais wa Ukawa atatangaziwa Mwanza leo.
Lissu arusha watu roho Geita
Akihutubia mkutano wa hadhara juzi, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema mgombea wa Ukawa anafahamika ndani na nje ya nchi na kinachosubiriwa ni kutangaza jina lake baada ya taratibu kukamilika akisisitiza kwamba chama hicho hakitashindwa kwa goli la mkono.
Aliwaambia wananchi wa Mji wa Geita waliokuwa wamefurika kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Nyankumbu kuwa Ukawa wamechelewa kumtangaza mgombea huyo kutokana na kuchelewa kupatikana mgombea mweza kutoka Zanzibar.
“Ndugu wananchi mgombea wa Ukawa nimtaje, nisimtaje,” aliwauliza wananchi waliofurika kwenye mkutano huo, nao wakaitikia, “mtajeee”
“Tumeshampata mgombea urais wa Ukawa na mnampenda sana na mnamjua sana. Ni mtu anayefahamika nchi nzima na duniani kote,” alisema Lissu huku akishangiliwa na wananchi.
Huku wananchi wakiwa na shauku ya kujua jina la mgombea, Lissu alisema baada ya taratibu za kumpata mgombea mwenza kukamilika, mgombea huyo atatangazwa.
“Siku tunamtangaza mtajua tu, tutaita vyombo vyote vya habari ili kumtangaza kwa hiyo mtamjua,” alisema Lissu.
Wakati Lissu akitoa ufafanuzi huo, alijikuta akitaja jina la Dk Slaa na kusababisha umati uliokuwa umefurika uwanjani hapo kushangilia.
“Kuna mambo yametuchelewesha, lakini wakati tunashughulika kumtangaza Dk Slaa... Wananchi (wakalipuka kushangilia)..., Lissu akaendelea, “Samahani ulimi hauna mfupa, samahani sana naomba mniwie radhi jamani…jamani, jamani, tulieni.”
Alisema umoja huo bado una presha kubwa kuhusu kutaja jina la mgombea na kuwa wapo baadhi ya viongozi wa Serikali na vyama hasimu ambao wanaombea Ukawa iparaganyike.
“Wapo wanaotuombea mabaya Ukawa na wengine wanapewa fedha ili kuhakikisha Ukawa inavunjika. Kamwe Ukawa haitavunjika. Ninawahakikishia wananchi kwamba Ukawa iko imara na haitavunjika hata wakituombea mabaya,” alisema Lissu.
Amtaja Dk Magufuli
Akimzungumzia mgombea wa CCM, Dk John Magufuli, Lissu alisema Ukawa haitishiki naye kwa sababu hajawahi kuzungumzia kero zinazowakabiliwa wananchi, yakiwamo mateso yaliyowapata wafugaji baada ya ng’ombe wao kuuawa na wengine kuteswa wakati wa Operesheni Tokomeza.
Alisema tangu kuibuka kwa tuhuma mbalimbali dhidi ya Serikali iliyopo madarakani likiwamo sakata la Richmond na Tegeta Escrow, Dk Magufuli hajawahi kusimama na kuutangazia umma nini msimamo wake kuhusiana na kashfa hizo.
Bulaya atajwa Chadema
Mkutano huo utakaorushwa moja kwa moja katika televisheni, pia unatarajia kumpokea Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya aliyetangaza kukihama chama hicho juzi bila kuweka wazi anakohamia.
Hata hivyo, mbunge huyo ambaye tayari ameweka wazi kupitia ukurasa wake wa Facebook kuwa atawania ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini, amekaririwa na gazeti hili akisema hatima yake itakuwa hadharani leo.
Lembeli rasmi Chadema
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli jana alihitimisha uvumi kuwa angehamia Chadema baada ya kutangaza rasmi kujiunga na chama hicho na papo hapo akatangaza kulitetea jimbo hilo kupitia chama hicho cha upinzani.
Lembeli (58), ambaye pia anatarajiwa kutambulishwa rasmi katika mkutano wa Mwanza, aliwaambia wanahabari Dar es Salaam jana kuwa amekihama chama tawala baada ya kushindwa kuvumilia fitna na rushwa.
“Nimekaa, nimetafakari, nimezungumza na mama yangu kwa muda wa zaidi ya saa 10, mke wangu na watoto na kwa kusikia kilio cha wananchi wa jimbo la zamani la Kahama nimeamua yafuatayo; kwanza ni kujiondoa uanachama wangu ndani CCM.
“Sikupenda ila nimelazimika kuchukua uamuzi huu, najua umewauma wengi na kuwakera wengi lakini nawaomba nao waangalie hali ya viongozi wa wilaya wa Kahama waliosababisha hayo… ni uamuzi mgumu sikupenda iwe hivyo na pili, kuanzia leo najiunga na Chadema,” alisema Lembeli aliyeambatana na binti yake ambaye pia alijiunga nacho.
Mbunge huyo aliyeitumikia CCM katika nafasi hiyo kwa miaka 10, aliwataka wananchi wa Jimbo jipya la Ushetu alikozaliwa kutovunjika moyo na kuunga mkono safari yake mpya akiahidi kuwa atakuwa nao bega kwa bega kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Alipoulizwa kwa nini aliamua kuhamia Chadema na siyo vyama vingine vya upinzani, Lembeli alisema ni chama cha pili kwa nguvu na kina mtandao nchini, hivyo asingependa kuhamia chama ambacho angeanza upya safari yake ya kisiasa.
“Mimi nimeonyesha nia kutoka rohoni ya kuhamia Chadema, nitapitia mchakato wote wa kumtafuta mgombea ili nipate ridhaa ya kupererusha bendera ya chama hicho na nina uhakika kwa Kahama kwa asilimia 100 nitapita… iwapo nitafeli mimi sina mpango mbadala na nimeshajiunga Chadema mpaka mwisho,” alisema.
Si mtandao wa Lowassa
Huku akizungumza kwa umakini, Lembeli alisema Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa yeye si miongoni mwa makada wanaoihama CCM kutokana na kukatwa kwa Lowassa, bali kutokana na rushwa iliyokithiri, hivyo hatua hiyo (ya kukimbia rushwa), itamsaidia kukwepa fedheha.
Imeandikwa na Nuzulack Dausen, Aidan Mhando na Salum Maige
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment