Na Hadija Jumanne na Tausi Ally, Mwananchi
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana iliahirisha kutoa hukumu ya rufaa iliyofunguliwa na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda hadi Novemba 27.
Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Augustine Shangwa aliiahirisha kesi hiyo kwa kuwa hukumu bado haijaandikwa.
Katika rufaa hiyo, Ponda anayetetewa na wakili Juma Nassoro anapinga hatia ya adhabu aliyopewa katika hukumu ya Mahakama ya Kisutu, akidai kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
Katika kesi ya msingi, Ponda na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6 milioni na kuingia kijinai kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali eneo la ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd.
Ponda na mwenzake, Mukadamu Swaleh walikuwa wakikabiliwa na shtaka lingine la uchochezi.
Katika Mahakama ya Kisutu, hukumu ya Ponda ilitolewa na Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, Mei 9, 2013 na kumtia hatiani kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo hilo la ardhi, lakini ikawaachia huru washtakiwa wengine.
Hata hivyo, licha ya kumtia hatiani Ponda, Mahakama hiyo ilimwachia huru kwa masharti ya kutokutenda kosa lolote katika kipindi cha mwaka mmoja, chini ya kifungu cha 25 (g) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu. Katika rufaa yake kupinga hukumu hiyo, Ponda anadai kuwa Mahakama hiyo ilikosea kumtia hatiani kwa shtaka hilo kwa kuwa hakukuwa na ushahidi wa kuingia kijinai katika eneo hilo.
Awali, kabla ya kuahirishwa, idadi kubwa ya wafuasi wa Sheikh Ponda walifurika katika viwanja vya Mahakama ili kujua hukumu itakayotolewa.
Nje ya mahakama hiyo, ulinzi mkali uliimarishwa likiwamo gari moja la maji ya kuwasha, mbwa na askari waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment