Matokeo hayo yalifanya wapenzi wa soka waliofurika kwenye uwanja huo siku hiyo kusema kwamba, ‘Bubu ameongea uwanjani’, wakiwa na maana kwamba, vipigo vitatu bila majibu viliifanya Yanga kuwa bubu, yaani haikutamba mbele ya Simba.
Hata hivyo, Yanga mwaka huo ilikuwa imara, kwani awali ilikuwa imezifunga Coastal Union 2-1, Pamba ya Kigoma 4-1, Biashara Kagera 5-1, CDA 2-0, KMKM 3-0 na baadaye kuifunga tena CDA 2-1 ingawa ilikuwa imetoka sare ya goli 1-1 na TCC (Sigara) ya Dar es Salaam.
Simba ilizifunga Tembo ya Ruvuma 2-0, Biashara Kagera 1-0, Pamba Mwanza 2-1, Ujamaa ya Zanzibar 4-1, CDA 2-1, lakini mbali ya kufungwa na Yanga na kuvuliwa ubingwa, pia ilifungwa na Pan African mara mbili. Kwanza ilifungwa goli 1-0 halafu ikafungwa magoli 2-0 katika mchezo wa mwisho wa ligi hiyo.
Katika ligi hiyo, mchuano ulioleta upinzani mkubwa msimu huo ulikuwa huo wa wapinzani wa jadi. Ilikuwa wazi kabisa kuwa, Yanga ya mwaka huo haikuwa ile ya miaka iliyopita, na Simba waliona hali ilivyokuwa ngumu kwao.
Goli lililokata mzizi wa fitina kwa Simba lilifungwa na nahodha wa Yanga, ‘Jenerali’ Juma Mkambi katika dakika ya 42 kufuatia mpira wa kona uliopigwa na mlinzi wa kushoto wa timu hiyo, Ahmad Amasha kutoka magharibi ya uwanja upande wa kusini. Mlinda mlango wa Simba, Omari Mahadhi bin Jabir, aliupiga kwa ngumi na ukamfikia Mkambi, ambaye bila ajizi aliutumbukiza wavuni kwa kichwa.
Ukiacha rafu za hapa na pale, mpira ulikuwa safi na Yanga wangetulia, basi wangejipatia magoli mengi. Hata hivyo, kwa ushindi huo, Yanga wakawa na matumaini ya ubingwa, kwani baada ya kuifunga CDA 2-1 sasa ikabakia na mchezo dhidi ya Pan African, ambapo ilihitaji sare ili kuwa bingwa. Na ndivyo ilivyokuwa katika mchezo wao wa Septemba 13, kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo timu hizo hazikufungana.
Jumla ya shilingi 818,845 zilipatikana, watu 31,608 walilipa kiingilio.
Timu hizo ziliwakilishwa na:
YANGA: Hamisi Kinye, Athumani Juma ‘Chama’, Ahmad Amasha, Allan Shomari, Charles Boniface, Shaaban Katwila/Charles Kilinda, Juma Mkambi (nahodha), Rashidi Hanzuruni, Omari Hussein.
SIMBA: Omari Mahadhi, Kihwelu Mussa, Mohammed Kajole, Yussuf Ismail Bana, Mohammed Bakari ‘Tall’, Nico Njohole, George Kulagwa, Mrage Kabange, Jumanne Hassan ‘Masimenti’/Adamu Sabu, Abdallah Mwinyimkuu.
NB: Makala haya ni kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘MIAKA 50 YA UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment