ZITTO: 
Mwaka 1997 ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme ulikamilika. Hata hivyo, TANESCO ilibaini kwamba gharama za ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme ambazo IPTL iliwasilisha kwake zilikuwa kubwa tofauti na makubaliano ya kwenye Mkataba. IPTL ilikuwa imefunga injini zenye msukumo wa kati ( medium speed) zenye gharama ndogo na uwezo mdogo badala ya injini za msukumo mdogo ( low speed) zenye nguvu kubwa na bei kubwa. Wakati huo huo IPTL waliendelea kutoza kiasi kikubwa cha fedha kinacholingana na gharama ya ufungaji wa mtambo wenye msukumo mdogo ( low speed) .

Kutokana na IPTL kukiuka makubaliano ya Mkataba kama ilivyoelezwa hapo juu, mwaka 1998 TANESCO ilifungua Shauri Na. ARB/98/8 katika Baraza la Kimataifa la Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (The International Centre for Settlement of Investiment Disputes - ICSID) kupinga ukiukwaji huo. Katika Hukumu iliyotolewa na ICSID, IPTL iliagizwa kupunguza gharama za uwekezaji kutoka USD 163.531 milioni hadi USD 127. 201 milioni kwa mwezi.

Ujenzi wa Mtambo ulikamilika mwaka 1997 lakini uzalishaji na uuzaji wa umeme ulianza mwaka 2002. Kwa mujibu wa makubaliano ya kuzalisha umeme, TANESCO ina wajibu wa kulipia gharama za uwekezaji ( capacity charges ) kwa wastani wa USD 2.6 milioni kila mwezi.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imebainika kuwa chanzo cha mgogoro kati ya TANESCO na IPTL ambacho ndio kilisababisha kufunguliwa kwa Akaunti ya Tegeta ESCROW, ni taarifa ziliyoifikia Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO mnamo tarehe 01 Aprili, 2004. Kaika Taarifa hiyo, pamoja na mambo mengine walifahamishwa na mmoja wa wanahisa wa IPTL, Kampuni ya VIP Engineering, kuwa kuna viashiria kuwa TANESCO wanailipa IPTL capacity charges kubwa.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO iliiteua Kampuni ya Uwakili ya Mkono ili kufuatilia madai hayo na kutoa ushauri kwa Bodi

Kwa kuzingatia ushauri wa Kampuni ya Uwakili ya Mkono, Menejimenti ya TANESCO kupitia barua namba DMDF&CS/02/05, tarehe 17 Juni, 2004 walitoa Notisi kwa IPTL ya kutoendelea walichokuwa kulipa capacity charges kwa sababu kiwango wanatozwa ni kikubwa kuliko inavyostahili.

Pamoja na kutoa Notisi hii Kamati imebaini kuwa Bodi na Menejimenti ya TANESCO kwa nyakati tofauti walizitaarifu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Nishati na Madini, na Msajili wa Hazina kuomba zichukue hatua stahiki kutatua mgogoro uliokuwa unaendelea. Kamati ilifanikiwa kuona barua Na. NEM/740/05 ya tarehe 6 Desemba, 2005 kutoka kwa Kampuni ya Uwakili ya Mkono kwenda kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. Patrick Rutabanzibwa akirejea mazungumzo yao ya tarehe 5 Desemba, 2005 ambapo iliamuliwa kuwa Kampuni ya Uwakili ya Mkono iandae Rasimu ya Makubaliano kwa ajili ya ufunguzi wa Akaunti ya Tegeta ESCROW.

Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali 
“... Kwa jinsi tulivyopitia fedha hii, tungesema ipo katika makundi matatu. Kundi la kwanza hiyo fedha ilikuwa na kodi ndani yake kwa hiyo tungesema kulikuwemo na fedha ya Serikali kwa maana ya kodi. Kwa upande mwingine, kwa sababu mpaka ESCROW inafunguliwa kulikuwa na dispute, kulikuwa na kutokubaliana juu ya charges, kwa hiyo kuna fedha ambayo inaweza ikawa ni ya TANESCO na kuna fedha ambayo inaweza kuwa ni ya IPTL ...”

Kamishna Mkuu wa TRA
“... TANESCO walitudhihirishia na kwa evidence kwamba katika kufanya yale malipo kwenye ESCROW Account walilipa pamoja na pesa ambayo ilitakiwa kulipwa kwetu ya VAT. Kwa hiyo, kulikuwa na VAT Component ambayo haikutakiwa kwenda kule ... 


Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Prof. Sospeter Muhongo (Mb)
“... fedha za ESCROW hizi ni fedha zilizowekwa baada ya hawa wafanyabiashara wawili kutokukubaliana na zingeweza kuwekwa popote ... kwa hiyo hizo pesa ni za IPTL, yaani ni kitu ambacho ni rahisi kabisa, lakini mtu anataka kupotosha hapa anasema fedha za walipa kodi, fedha sijui za wakulima, hakuna kitu kama hicho

MAUZO YA HISA ZA IPTL
Umiliki wa hisa unakamilika pale ambapo muuzaji anamkabidhi mnunuzi Hati ya hisa husika, vinginevyo mnunuzi anakuwa amenunua “hisa hewa”. Pamoja na ukweli huu bado Piper Links tarehe 21 Oktoba, 2011 ilimuuzia PAP hisa zile saba kwa gharama ya USD 20 milioni. Swali linalojitokeza hapa ni kuwa unawezaje kuuza kitu usichonacho?

Kutokana na mahojiano kati ya Kamati na Kamishina Mkuu wa TRA ilibainika kwamba Kampuni ya Piper Links haijulikani sio tu British Virgin Islands bali hata nchi nyingine. 20 Kamati haielewi ni jinsi gani taasisi kubwa kama Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na nyingine zilizohusika katika suala hili, na ambazo tunaamini zimesheheni Watendaji wenye weledi, zimewezaje kushindwa kufanya uchunguzi wa kina ( due diligence ) ambao ungewezesha utata huu kugundulika na kuepuka kudanganywa na PAP.

Hisa kutoka Piper Links kwenda PAP ziliuzwa kwa gharama ya USD milioni 20, lakini taarifa zilizopelekwa TRA zilionyesha kuwa hisa hizo zimeuzwa kwa USD 300,000. Kwa mantiki hiyo Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Piper Links ilitozwa na kulipa kodi ya ongezeko la mtaji kiasi cha Sh. 47,940,000 na Sh. 4,800,000 kama ushuru wa stempu ( stamp duty) ’. Katika mahojiano, Kamishna Mkuu wa TRA aliifahamisha Kamati kuwa kwa gharama ya USD milioni 20 kiasi cha kodi ya ongezeko la mtaji kilichotakiwa kulipwa ni Sh. 6,399,977,600 na sio Sh. 47,988,800, na kwa upande wa ushuru wa stempu ‘stamp duty’ kiasi kilichotakiwa kulipwa ni Sh. 320,000,000 na siyo Sh. 4,800,000. Kwa maana hiyo jumla ya kodi iliyopotea kwa maana ya kodi ya ongezeko la mtaji na ushuru wa stempu ( stamp duty) ’ ni Sh. 6,667,188,800.

Jumla ya kodi iliyopotea kutokana na uuzaji wa hisa za Mechmar kwenda Piper Links na za Piper Links kwenda PAP ni jumla ya shilingi 8,683,177,600.

Kamati ilipokea taarifa ya uchunguzi wa ndani iliyofanywa na TRA ambao ulithibitisha ukwepaji mkubwa wa kodi na udanganyifu wa mikataba. Kamati imekubaliana na uamuzi wa TRA kuondoa hati za kodi kwa IPTL na hivyo kuna uwezekano kuwa kuanzia tarehe 24 Novemba, 2014 PAP haitokuwa tena mmiliki wa IPTL mpaka hapo watakapofuata upya tararibu za kisheria na TRA kukusanya kodi stahiki.

Malipo yote ya Sh. 167,251,892,330 na USD 22,198,544 zililipwa kwa Kampuni ya PAP kupitia Akaunti Na. 912000012534 ya USD na Akaunti Na. 9120000125294 ya Shilingi za kitanzania katika Benki ya Stanbic zilizofunguliwa tarehe 27 Novemba, 2013 maalum kwa ajili ya kupokea fedha hizo. Hivyo jumla ya fedha iliyotolewa kwenye Akaunti ya Tegeta ESCROW na kulipwa kwa PAP ni shilingi 203,102,540,890.

Kuhusu suala la fedha zilizowekwa katika Akaunti ya Tegeta ESCROW, uhakiki wa wakaguzi ulibainisha kuwa kulikuwa na jumla ya Sh. 182,771,388,687, kati ya hizo TANESCO iliweka Kiasi cha Sh. 142,008,357,587 na Wizara iliweka Kiasi cha Sh. 40,763,031,100.

Pamoja na riba ya Sh. 11,160,288,948 iliyopatikana katika uendeshaji wa Akaunti ya Tegeta ESCROW, fedha hizo zote zililipwa kwa Kampuni ya PAP, huku wakala wa uendeshaji wa Akaunti husika (BOT) hakupewa kiasi chochote japokuwa walitumia gharama kubwa katika kesi zilizofunguliwa dhidi ya Akaunti hiyo na gharama za kawaida za uendeshaji
.


USHIRIKI WA TAASISI ZA SERIKALI NA WATU BINAFSI KATIKA UTOAJI FEDHA KATIKA AKAUNTI YA TEGETA ESCROWKamati imethibitisha kuwa uthibitisho na vielelezo alivyopata Gavana wa Benki Kuu katika kufikia maamuzi ni Taarifa ya Kamati ya Wataalam

Kuhusu Wizara ya fedha kupeleka ushauri kuhusiana na uwepo wa Kodi ya Ongezeko la thamani katika fedha zilizopo katika Akaunti ya Tegeta ESCROW, Kamati haikupata ushahidi kwamba Wizara ya Fedha ilishauri kuhusu masuala ya kodi ya ongezeko la thamani katika fedha zilizokuwepo kwenye Akaunti ya Tegeta ESCROW pamoja na kushauriwa na TRA kwa barua Na. 100-221-969/214 ya tarehe 29 Oktoba, 2013 iliyonakiliwa pia kwa Gavana wa Benki Kuu. Katika barua hiyo TRA waliainisha uwepo wa kodi ya ongezeko la thamani ya Sh. 26,946,487,420.80 kwenye Akaunti ya Tegeta ESCROW (Kiambatisho Na. 11). Hata hivyo, barua ya TRA Kumb. Na. TRA/CG/L.3 ya tarehe 4 Februari, 2014 kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ilionesha kuwa kiasi cha kodi barua yenye Kumb. Na. SEC.427/IPTL/10/2013 kinachodaiwa ni Sh. 21,713,935,720.75.

Mheshimiwa Spika, Kamati imepitia Mkataba wa mauzo ya Hisa kati ya Kampuni ya PAP na VIP na kuthibitisha kuwa Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo (Mb) ndiye alikuwa kiungo kati ya Bw. Harbinder Singh Sethi wa IPTL na Ndg. Rugemalira wa VIP (Kiambatisho Na. 16). Katika mkataba huo wa tarehe 19 Agosti, 2013. Ndg. James

Rugemalila alithibitisha kuwa Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Prof. Sospeter Muhongo alimwomba kuwasilisha kiasi cha fedha ambacho angependa kulipwa na IPTL ili kumaliza Shauri lililokuwepo mahakamani. Aidha, Bw. Sethi aliwasilisha kwa Bw. Rugemalira ushahidi kwamba PAP imenunua Hisa 7 za Mechmar katika IPTL.

Mchakato wote wa kutoa fedha katika Akaunti ya Tegeta ESCROW ndipo ulipoanza na mauzo ya hisa za VIP kwenda PAP na baadaye kuhitimishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu ya tarehe 5 Septemba, 2013 ambayo ndiyo yaliyotumika kuhalalisha utoaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta ESCROW tarehe 28 Novemba hadi 5 Desemba, 2013.


Baada ya kupokea taarifa za benki (bank statements) kutoka Benki ya Stanbic na Benki ya Mkombozi, Kamati ilibaini yafuatayo: -
a) Kuwepo kwa fedha zilizohamishwa kutoka Akaunti ya PAP iliyoko Benki ya Stanbic kwenda Akaunti ya VIP iliyoko katika Benki ya Mkombozi.
b) Kuwepo kwa fedha taslimu zilizolipwa kwa watu binafsi ambao majina yao hayaonekani lakini walifanya miamala mikubwa kinyume cha Sheria ya Benki Kuu na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
c) Kuwepo kwa fedha walizohamishiwa watu mbalimbali katika Akaunti zao binafsi.
d) Katika fedha ambazo zimelipwa kwa watu binafsi katika Benki hizi yapo majina ya viongozi wa kisiasa, viongozi wa madhehebu ya dini, Majaji na watumishi wengine wa Serikali.

Kamati inajiuliza ni nini mahusiano ya moja kwa moja kati ya Viongozi hawa na malipo yaliyotokana na Akaunti ya Tegeta ESCROW. Mfano kwa upande wa viongozi wa kisiasa ambao waliingiziwa fedha katika akaunti zao binafsi ni; Mhe. Andrew Chenge (Mb), ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, shilingi bilioni 1.6; Mhe. Anna Tibaijuka (Mb) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi shilingi bilioni 1.6; Mhe. William Ngeleja (Mb) na ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini shilingi milioni 40.4 na Ndg. Daniel N. Yona ambaye alikuwa pia Waziri wa Nishati na Madini shilingi milioni 40.4; Ndg. Paul Kimiti ambaye ni Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Sumbawanga shilingi milioni 40.4 na Dr. Enos S. Bukuku ambaye alikuwa Mjumbe wa Bodi ya TANESCO aliingiziwa shilingi milioni 161.7.

Upande wa Viongozi wa Madhehebu ya Dini walioingiziwa fedha na Benki ya Mkombozi ni Askofu Methodius Kilaini shilingi 80.9, Askofu Eusebius Nzigirwa shilingi milioni 40.4 na Mchungaji Alphonce Twimann Ye Simon shilingi milioni 40.4

Kamati ilithibitishiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kuwa baadhi ya watu walienda kugawana fedha kwenye Benki tajwa wakiwa na mifuko ya rambo, sandarusi, mabox, magunia na lumbesa. Kutokana na muamala uliofanyika tarehe 6 Februari, 2014 katika Benki ya Mkombozi kiasi cha shilingi bilioni 3.3 na muamala wa Benki ya Stanbic wa tarehe 23 Januari 2014 ambapo fedha taslimu (cash) kiasi cha shilingi bilioni 73.5 zilitolewa na kugawanywa kwa watu mbalimbali kinyume cha Sheria ya Benki Kuu na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006

Kwa mujibu wa Ibara ya 59(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiye mshauri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo ya sheria na anawajibika kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu mambo yote ya kisheria na ushauri wake ni wa mwisho.

Kamati imebaini kwamba maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Gavana wa Benki Kuu, kuwa hapakuwa na kodi ya Serikali iliyopaswa kukusanywa kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta ESCROW, yalimsababisha Gavana wa Benki Kuu na hivyo kubariki utoaji wa fedha hizo kabla ya kukata kodi ya Serikali. Aidha maelekezo hayo yalikiuka masharti ya kifungu cha 5(4) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Mwaka 2006. Mheshimiwa Spika, kitendo cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutofanya mawasiliano na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na kwamba ana mamlaka ya kutafsiri sheria alipaswa kujiridhisha kwamba hapakuwa na kodi iliyopaswa kukatwa kutoka kwenye fedha zilizokuwa kwenye Akaunti hiyo. Aidha, angeweza kujiridhisha kutoka TANESCO iwapo fedha zilizokuwa zinapelekwa
 kwenye Akaunti ya Tegeta ESCROW hazikuwa na kodi ya ongezeko la thamani. Kwa kutotimiza wajibu huo Ofisi yake ilifanya uzembe wa kutokufanya uchunguzi wa kina wa suala hili ( due diligence ) kabla ya kutoa maelekezo kwa Benki Kuu ya Tanzania. Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Gavana yaliikosesha Serikali kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kiasi cha shilingi 23,154,003,077.

Miongoni mwa wahusika wakuu wa suala zima la IPTL hususan Akaunti ya Tegeta ESCROW ni Bw. Harbinder Singh Sethi, ambaye anafahamika kama Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa IPTL na wakati huohuo kama Mkurugenzi Mtendaji na Mmiliki wa PAP. Uhusika wake unaanzia katika ununuzi wa hisa saba (7) za Mechmar kwenda Piper Links Investments na kisha kutoka Piper Links Investiments kwenda PAP na hatimaye hisa 3 za VIP kwenda PAP na hivyo kumpa umiliki wa IPTL na PAP kwa asilimia mia moja.

Kwa mujibu wa Mkataba wa ufunguaji wa Akaunti ya Tegeta ESCROW, washirika wawili katika akaunti hiyo walikuwa ni Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba ya TANESCO na IPTL na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ilikuwa ni Wakala wa Akaunti husika kwa ajili ya utunzaji wa fedha na uwekezaji.

Kamati imebani kuwa uongozi wa Wizara kwa namna moja au nyingine umefanikisha utoaji wa fedha kwenye akaunti ya ESCROW Kinyume na kipengele 2.1 cha Mkataba wa ESCROW ambacho kinabainisha kuwa washirika wa Akaunti ya Tegeta ESCROW ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya IPTL na sio vinginevyo, kama kinavyonukuliwa hapo chini:

Pamoja na msimamo huo wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kuwa umiliki wa fedha za ESCROW au sehemu ya fedha hizo ni ya Umma, tarehe 20 Septemba, 2013 siku nne baada ya kuwa na mtizamo kuwa fedha za ESCROW ni za Umma au kiasi chake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini alimjulisha Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa IPTL Bw. Harbinder Singh Sethi ambaye pia ni Mmiliki wa PAP kupitia barua yenye Kumb. Na. SBD.88/147/01/4 (Kiambatisho Na. 19) kuwa Wizara haikuwa na pingamizi dhidi ya kutolewa kwa fedha za ESCROW kama bwana Sethi angewasilisha ushahidi wa kuuzwa kwa hisa asilimia 70 za Mechmar katika IPTL na kutoa kinga kwa Serikali na TANESCO baada ya utoaji wa fedha hizo. 


Kamati imepata mashaka makubwa juu ya sababu iliyomshawishi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kubadili msimamo na kuondoa masharti yake ya awali kwa Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa IPTL ndani ya siku nne na kuamua kuwa Wizara haioni tena kikwazo cha kuruhusu utoaji wa fedha ikiwa ni Kinyume kabisa na mkataba wa ESCROW uliohitaji kukamilika kwa mgogoro baina ya TANESCO iliyokuwa ikisimamiwa na Wizara na IPTL.

Kamati iliendelea kubaini kuwa makubaliano ya uuzwaji wa hisa za Mechmar kwenda kwa Piper Links Investment yamejaa utata mkubwa kutokana na uchunguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kubaini kuwa watia saini katika makubaliano husika hawakuainisha majina yao dhidi ya sahihi walizoweka, hivyo kutoa tafsiri kuwa kuna jambo lilikuwa linafichwa kwa makusudi.

Kamati imethibitisha bila chembe ya mashaka kwamba mchakato mzima wa kutoa fedha katika akaunti ya Tegeta ESCROW uligubikwa na mchezo mchafu na haramu wenye harufu ya kifisadi ulioambatana na udanganyifu wa hali ya juu ambao kwa kufuata sheria tu ungeweza kugundulika na kuzuiwa. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mfumo mzima wa Serikali ni kama ulipata ganzi au uliganzishwa ili kuwezesha zaidi ya shilingi bilioni 306 kuporwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania na kutakatishwa kupitia Benki mbili hapa Nchini na baadhi ya mabenki ughaibuni.

Kamati imethibitisha kuwa hukumu ya Jaji Utamwa ya kukabidhi masuala yote ya IPTL kwa Kampuni ya PAP, ilitafsiriwa vibaya kwanza na Bwana Harbinder Singh Sethi mwenyewe na baadaye ikatafsiriwa vibaya pia na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hata baadhi ya viongozi wakuu wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tafsiri hii potofu ilirudiwa rudiwa na kuimbwa na viongozi wa Wizara kiasi cha kuliaminisha Bunge na Umma kwamba ndio ilikuwa tafsiri sahihi. Baada ya kupata ushahidi usio na mashaka kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za 91 Serikali na Mamlaka ya Mapato Tanzania, ni dhahiri Kampuni ya PAP haikuwa na uhalali wowote wa umiliki wa IPTL wakati inalipwa fedha za kutoka Akaunti ya Tegeta ESCROW.


Kamati inapendekeza kama ifuatavyoTaasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) mara moja wachukue hatua ya kumkamata Bwana Harbinder Singh Sethi na kumfikisha mahakamani kwa makosa ya Anti money laundering , ukwepaji kodi na wizi. Kamati pia inaelekeza Serikali kutumia sheria za Nchi, ikiwemo sheria ya ‘ Proceeds of Crime Act ’ kuhakikisha kuwa Bwana Harbinder Singh Sethi anarejesha fedha zote alizochota kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Kwa kuwa suala hili ni suala la utakatishaji wa fedha haramu, Mamlaka ziwasiliane na mamlaka za Nchi nyingine kuhakikisha mali za Bwana huyu zinakamatwa na kufidia fedha hizo.

Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU fedha hizo pia ziligawiwa kwa watu mbalimbali binafsi. Kamati haina tatizo na watu wawili kuuziana makampuni yao kwa thamani wajuazo wenyewe, au jinsi ya kuzitumia fedha zao, ama kuwachagulia watu wa kuwagawia, lakini Kamati imejidhihirishia kuwa fedha iliyotumika kulipia manunuzi hayo ni fedha ambayo sehemu yake ni ya umma iliyochotwa bila huruma wala aibu, kutoka Benki Kuu. Hivyo, Kamati inazitaka mamlaka za uchunguzi kuhakikisha kuwa fedha hizo zinarudi Benki Kuu hata ikibidi kwa kufilisi mali za watu wote 97 waliofaidika na fedha hizo kwa thamani ya fedha walizopewa na Bwana Rugemalira

Baadhi ya waliofaidika na fedha hizo ni Viongozi wa Umma ambao wanapaswa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Sheria namba 13 ya Mwaka 1995) ambayo inawataka kutoa taarifa ya zawadi wanazopokea au malipo wanayolipwa. Vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi kutambua kama walifuata matakwa ya sheria na hatua mahsusi zichukuliwe, ikiwemo kuvuliwa nyadhifa zao zote za kuchaguliwa na/au kuteuliwa, kufilisiwa mali zao na kushtakiwa mahakamani kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 132 (1) – (6). 


Kamati imejiridhisha kwamba, suala la akaunti ya Escrow ni jambo la utakatishaji wa fedha (Money Laundering), kama alivyosema Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU katika mahojiano yake na Kamati. Kamati inazitaka mamlaka zinazohusika, ikiwemo Benki Kuu kuzitangaza benki za Stanbic na Mkombozi Commercial Bank kama asasi za utakatishaji fedha (Institutions of Money Laundering Concern).


Aidha, Kamati inalikumbusha Bunge lako tukufu pendekezo muhimu lililotolewa na Kamati Teule ya Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe kuhusu sakata la maarufu la Richmond

Kamati inapendekeza kwamba, azimio hili litekelezwe kwa kupitia upya mikataba yote ya umeme ambayo inalitafuna Taifa letu.

Aidha, Kamati imebaini kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye alikuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Bwana Harbinder Singh Sethi na Bwana James Rugemalira, tena katika ofisi ya Umma; na pengine hii ndiyo iliyokuwa sababu ya upotoshaji huu. Waziri wa Nishati na Madini alifanya udalali huo akijua dhahiri kuwa Bwana Sethi hana uhalali wa kisheria kufanya biashara kwa jina la IPTL. Iwapo Waziri wa Nishati na Madini angetimiza wajibu wake ipasavyo, Fedha za Tegeta ESCROW zisingelipwa kwa watu wasiohusika, na Nchi ingeweza kuokoa mabilioni yaliyopotea kama kodi za VAT, Capital Gain Tax na Ushuru wa Stempu ambazo ni sawa na takribani shilingi bilioni 30.

Mheshimiwa Spika, Kamati inapendekeza kuwa Mamlaka yake ya uteuzi itengue uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini kutokana sababu hizo zilizoelezwa.

Kamati pia imethibitisha uzembe wa hali ya juu uliofanywa na Katibu Mkuu huyo, kushindwa kujiridhisha kama masharti ya Sheria ya kodi ya Mapato Sura ya 333, Kifungu cha 90(2) yalitekelezwa. Kifungu hicho kimsingi kinaitaka mamlaka ya ‘ approval ’’ ya uhamishaji wa Makampuni kutotambua Kampuni mpaka kwanza kodi za uhamishaji ziwe zimelipwa na hati za malipo ya kodi zimetolewa na mamlaka ya kodi. Mheshimiwa Spika, Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Katibu Mkuu huyu utenguliwe, na TAKUKURU wamfikishe mahakamani mara moja, kwa kuikosesha Serikali Mapato, matumizi mabaya ya ofisi na kusaidia utakatishaji wa fedha haramu.

Kamati imethibitisha kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitoa ushauri ulioipotosha Benki Kuu ya Tanzania kuhusiana na hukumu ya Jaji Utamwa J. Kwa kutumia madaraka yake vibaya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliagiza kodi ya Serikali yenye thamani ya shilingi 21 bilioni isilipwe 106 na hivyo kuikosesha Serikali mapato adhimu. Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kujua na kwa makusudi alilipotosha Bunge na Taifa kwamba mgogoro uliopelekea kufunguliwa kwa Akaunti ya ESCROW ulikuwa ni mgogoro wa Wanahisa wa IPTL badala ya mgogoro kati ya TANESCO na IPTL. Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali utenguliwe mara moja na kisha afikishwe mahakamani kwa matumizi mabaya ya Ofisi yaliyopelekea Serikali kupoteza mabilioni ya fedha. 


Baada ya kupitia vielelezo vilivyomo kwenye ripoti ya CAG, Kamati imejiridhisha pasipo mashaka kuwa, Waziri Mkuu, alikuwa ana taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa kuchotwa fedha kutoka katika akaunti ya ESCROW.

Kamati, kwa kuzingatia kielelezo namba 22, inathibitisha bila shaka kwamba, Waziri Mkuu alikuwa analijua jambo hili vizuri na kwamba aliridhia muamala huu ufanyike. Ndiyo maana katika maelezo yake ya Bungeni mara kadhaa Waziri Mkuu alithibitisha kuwa fedha za Escrow hazikuwa fedha za Umma.

Ni dhahiri kwamba viongozi wenye mamlaka makubwa wanapaswa kila wakati kukumbuka kauli ya muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Muasisi wa Muungano, Sheikh Thabit Kombo, ambaye alikuwa akipenda kusema ‘ weka akiba ya maneno.

Kwa uzito na unyeti wa jambo hili, kwa vyovyote vile, Waziri Mkuu anapaswa kuwajibika kwa kauli zake na kwa kutokutekeleza wajibu wake wa kikatiba ipasavyo, ili kurejesha imani ya wananchi kwa serikali yao na viongozi wao wa kisiasa.

MAKINDA: Nasitisha shughuli zote za bunge mpaka kesho kulingana na kikao cha uongozi wa bunge tulichokaa leo asubuhi.