Taarifa ya Haraka kwa Vyombo vya Habari Kuhusu Mgogoro wa Ardhi
Loliondo
Sisi Viongozi wa Mila, Kisiasa, Wawakilishi wa Wanawake
tumesikitishwa sana na Taarifa ya uongo aliyoitoa Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Lazaro Nyalandu juu ya ukweli wa Mgogoro wa Loliondo. Ifuatayo ni ufafanuzi wa hali halisi kinyume na Waziri
alivyodanganya Dunia kupitia BBC tarehe 19/11/2014 na Gazeti la leo la
Mwananchi
- Kwamba eneo la Loliondo halina Wamaasai 40,000 watakaoadhirika endapo Serikali itatoa tamko Wakati wowote sasa:
Jibu: Idadi ya wakazi katika eneo
la km za mraba 1,500 ambavyo ni vijiji vya Ololosokwan, Soitsambu, Oloipiri,
Arash, Maaloni, Olorien/Magaiduru, Piyaya na Malambo ambavyo vina jumla ya
wakaazi 57,532. Kwa mujibu wa sensa
ya Taifa ya watu na Makazi ya 2012 kama ilivyo kwenye jedwali hapa chini.
SN
|
Kata
|
Idadi ya watu
|
1
|
Arash
|
7,841
|
2
|
Olosoito/Maaloni
|
4,353
|
3
|
Oloipiri
|
4,114
|
4
|
Soitsambu
|
10,956
|
5
|
Ololosokwan
|
6,557
|
6
|
Piyaya
|
5,303
|
7
|
Malambo
|
8,923
|
8
|
Olorien- Magaiduru
|
9,485
|
9
|
Orgosorok
|
1,521
|
10
|
Engusero Sambu
|
12, 268
|
|
Jumla
|
71, 321
|
Vijiji viwili (Engusero sambu na
Orgosorok) venye idadi ya watu 13,789 hawana makazi katika eneo la mgogoro
lakini ni watumiaji wa eneo hilo la malisho.Hivyo tunathibitisha kuwa watu
watakaoathirika eneo hili likichukuliwa ni 71,321.Hivyo Waziri kusema eneo hilo
halina watu 40,000 ni uongo mtupu.
- Kwamba Serikali ya Tanzania haijawahi kuwa na mpango wa kuwaondoa Wamaasai katika eneo la Loliondo:
1992: Serikali ilitoa ardhi ya
vijiji vya Tarafa za Loliondo na Sale kwa Mfalme wa UAE bila RIDHAA ya wananchi
na kusababisha mgogoro unaoendelea mpaka sasa. Kumweka mwekezaji katika ardhi
ya jamii bila ridhaa ilikua ni mpango wa muda mrefu wa kupora ardhi.
2008: Mgogoro huu umechukua sura
tofauti baada ya kampuni kuweka mikakati ya kuchukua ardhi yetu kwa ajili ya
uwindaji na kutengeneza mikataba iliyoridhiwa na viongozi na sio wananchi.
2009: Serikali ilitumia mikataba
iliyoridhiwa na baadhi ya viongozi wa vijiji kufanya opersheni ya kijeshi
ambayo iliharibu rasilimali, ilichoma makazi na kusababisha mtoto moja katika
kijiji cha Arash kupotea mpaka leo. Kijana Ngodidio Rotiken alijeruhiwa kwa
bomu na kupoteza jicho na madhara mengine mengi.
2010: Serikali ilitengeneza RASIMU
ya mpango wa Matumizi wa Ardhi ya Wilaya
kwa ufadhili wa OBC wa shilingi 157,000,000. Mpango huo ulitengeneza rasimu ya ramani ya kutenga eneo la Kilomita za
Mraba 1,500 kutoka kwenye ardhi ya vijiji. Mpango ulipingwa vikali na kukataliwa
na baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya Ngorongoro na jamii kwa ujumla kwa
sababu ya dhana nzima ya kutenga ardhi ya vijiji bila ushiriki wa wananchi.
2011/12: Serikali kupitia kamishina wa ardhi iliagiza vijiji vya
Ololosokwan na Engaresero kurudisha vyeti vya ardhi ya vijiji kwa madai kuwa
vina migogoro. Madai hayo yalithibitishwa kuwa ya uongo na yenye hila ya kupora
ardhi ya vijiji.
2013: Serikali kupitia Mhe. Waziri wa Maliasili na Utalii (Mhe. Khamis
Kaghasheki) ilitangaza RASMI kutenga eneo la Kilomita za mraba 1,500 ya ardhi
ya vijiji kuwa Pori Tengefu la Loliondo. Jambo hili lilizua taharuki kubwa
ndani na nje ya Nchi na kutishia usalama kwenye jamii ya Wafugaji na hatimaye
kumlazimu Waziri Mkuu kuingilia kati.
2014: Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu (Mb) alizuru
Loliondo mara mbili kwa nia ya kuhamasisha na kushawishi madiwani na wenyeviti
wa vijiji kukubali pendekezo la Serikali/OBC kutoa FIDIA ya shilingi Bilioni
moja kwa vijiji endapo watakubali kuachia eneo la kilomita za mraba 1,500. Pendekezo
lake halijakubaliwa hata na viongozi wachache aliyokutana nao.
Tarehe 19/11/2014 wakati wa
mahojiano na mtangazaji wa BBC, Mhe. Lazaro Nyalandu alisema alikwenda Loliondo
Kuhamashisha Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi:
Jibu: Waziri kisheria, hana mamlaka juu ya
kupanga matumizi ya Ardhi ya vijiji na wala haijawahi kuzungumziwa katika
mikutano ya Waziri na Baadhi ya Madiwani na wenyeviti alipokuja Loliondo. Mipango
ya Matumizi bora ya ardhi za vijiji inaratibiwa na Wizara ya Ardhi na Makazi na
sio Wizara ya Maliasili na Utalii…….. Ni Wizara hiyo hiyo inayoongozwa na
Nyalandu iliyopinga upimaji wa vijiji uliokuwa unatekelezwa na Wizara ya Ardhi
na Makazi mwaka 2013 kwa kuwarudisha ndani ya masaa 24 timu ya wataalamu
wakiongozwa na mpima wa Wizara ya Ardhi Ndg. Isaa Marwa waliokuwa wameanza
zoezi la upimaji.
Katika Mahojiano na BBC
tarehe 19/11/2014, Waziri Nyalandu alisema sio Wamaasai tu wanaishi katika eneo
la kilomita za mraba 1500:
Jibu: Wakazi wa eneo hili ni wafugaji wa jamii
ya wamaasai ambao ni zaidi ya 40,000
Katika gazeti la Mwananchi la tarehe 21/11/2014 Mhe Nyalandu alisema “yaani tunapanga kutumia askari kuwaondoa
wananchi kwenye maboma yao na kuyachoma moto…..Huu ni uongo, hakuna mpango kama
huo”
Jibu: Kwa kuwa Mhe Waziri Lazaro Nyalandu
yaelekea hana kumbukumbu ya matukio ya Loliondo tunamrejesha kwenye tukio la
mwaka 2009 lililoratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kutumia jeshi la
Polisi (FFU) kuteketeza kwa moto maboma ya wafugaji ya jamii ya Kimaasai zaidi
ya 300 katika eneo la Loliondo.
- Baada ya mkanganyiko huu wa Mhe Nyalandu, sisi viongozi wa Kisiasa, Kimila na Wawakilishi wa wanawake tumedhamiria kumwona tena Mhe. Waziri Mkuu ili kupata uhakika wa mpango huu wa Nyalandu, kwani hatuna imani tena na Wizara ya Maliasili na Utalii. Tumeumizwa na kusikitishwa sana na kitendo cha kushindwa kumwona japo tulipata uhakika wa muda wake wa kutuona (appointment) tarehe 19/11/14.
- Katika sakata hili tunatoa tena kwa mara nyingine ushauri ufuatao kwa Serikali ili kufikia suluhu ya kudumu kwa mgogoro huu:
I.
Waziri
Mkuu kutoa agizo lenye masharti ya muda kwa Wazira ya Maliasili na Utalii
kufuta kwa Maandishi Tamko lake kwa vyombo vya habari la tarehe 21, Machi 2013 kama ulivyotuahidi Sept
mwaka jana.
II.
Serikali
kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kutengua/kufuta hadhi ya Pori Tengefu
katika vijiji vya Loliondo kwa mujibu wa sheria mpya ya Wanyamapori ya mwaka
2009 na kuheshimu miliki halali za kisheria kwa ardhi yetu na mfumo wa maisha
yetu usioharibu mazingira.
III.
Waziri
Mkuu kutoa TAMKO kwa umma wa Watanzania
na Dunia nzima kwa maandishi kuhusu
Ahadi yake ya tarehe 23/9/13 kwetu kwamba
Serikali imeachana na mpango wa
kupora ardhi ya Vijiji vyetu. Aidha tunamwomba Waziri Mkuu kukemea kwa uzito
usumbufu huu tuanoupata watu wa Loliondo toka kwa Wizara ya Maliasili na Utalii
unaojirudia kila Wakati.
IV.
Tunaishauri
Serikali kufuta uwindaji katika Ardhi yetu, kwani hauhifadhi Wanyamapori wala sio
rafiki na mazingira, ufugaji na utalii wa picha. Uwindaji katika eneo la
Loliondo ni mpango wa kuwamaliza wanyama katika ikolojia ya Serenegeti,
Ngorongoro na Maasai Mara. Kuendelea kuruhusu uwindaji katika eneo hili, mgogoro
utaendelea na kusababisha madhara endelevu kwa uhifadhi wa wanayamapori, maisha
yetu na ustawi wetu.
V.
Tunamwomba
Mhe. Waziri Mkuu kutoa maelekezo ya haraka
kwa Wizara ya Ardhi na Makazi iendelea na zoezi la upimaji wa vijiji lililohairishwa
na Wizara ya Maliasili na Utalii mwezi
August, 2013 ili kuharakisha zoezi la kuandaa mipango ya Matumizi ya bora
za Ardhi.
VI.
Tunamwomba
Mhe. Waziri Mkuu kutekeleza haya kwa muda mfupi uwezekanavyo kwani tumekuheshimu
kwa kuvuta subira kwa mwaka mzima kama ulivyotuelekeza kwenye Barua yako ya Mwezi Mei mwaka jana “tuwe watulivu na
wavumilivu wakati ukishughulikia kilio chetu”. Kama utashindwa kutoa maelekezo
hayo ya kutimiza ahadi yako kwetu,
basi hatuna budi kuhamasisha dunia kupitia vyombo vya habari na kufika Dodoma ofisini
kwako kwa maelfu ili utueleze hatma ya Ardhi yetu na maisha yetu. Japo
tunaamini katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani, hata hivyo uvumilivu umetuishia na kamwe ardhi
yetu haitaporwa kwa maslahi ya kampuni ya OBC.
Imeandaliwa na:
1.Elias Ngorisa –
Mwenyekiti Wa Halmashauri
2. Ibraham Sakai-
Mwenyekiti wa CCM Wilaya.
3. Daniel
Ngoitiko- Diwani
4. Mathew Siloma-
Diwani
5. Tina Timan-
Diwani
6. John Kulinja-
Kiongozi wa Mila.
7. Mathew Timan-
Kiongozi wa Mila
8. Loserian
Minis- Mwakilishi wa Wenyeviti wa Vijiji.
9. Kooya Timan –
Mwakilishi wa Wanawake
10. Manyara
Karia- Mwakilishi wa Wanawake
Imetolewa leo
tarehe 21/11/2014, Arusha na Wawakilishi wa Jamii toka Tarafa za Loliondo na
Sale.
No comments:
Post a Comment