Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar/Dodoma. Moto wa kashfa ya ufisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow unaoendelea kuwaka bungeni, sasa unaonekana kugeuka gharika inayoweza kuwakumba vigogo wengi zaidi na kuiweka Serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika hali ngumu.
Kashfa hiyo ya uchotaji wa Sh306 bilioni za akaunti ya Escrow, inahofiwa kuwakumba vigogo zaidi ya 50 ndani ya Serikali wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu, wabunge, majaji na wakuu wa taasisi za Serikali waliohusika.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya mawaziri na watendaji wa Serikali na mahakama, inatishia anguko la Serikali.
“Kuna waziri (anamtaja) ameniambia ameangalia ile orodha ya watu wanaodaiwa kuchukua fedha hizo ni zaidi ya 52. Hofu yangu hili jambo likiingia bungeni na kujadiliwa huenda likasababisha kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri kwa mara nyingine,” alisema mbunge mmoja kutoka Kanda ya Mashariki.
Wabunge wajipanga
Mbunge mwingine kutoka Zanzibar (CCM), alisema kuwa anasubiri kwa hamu kuchangia katika mjadala huo ili waondoke wale wote ambao wamekwapua fedha hizo.
Juzi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliitisha kikao cha mawaziri ambacho kilihudhuriwa na baadhi ya mawaziri na walifikia uamuzi kuwa suala hilo litajadiliwa ndani ya chama kabla ya kuingia ndani ya Bunge.
“Kinachosubiriwa ni ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) halafu tutakutana wabunge wa CCM kabla ya kwenda bungeni,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Pamoja na hali hiyo, wabunge katika makundi makundi kwa wiki nzima wamesikika wakijadili jambo hilo huku wakilihusisha na mbio za urais mwakani.
Mbunge mmoja (jina tunalo) alisema kuhusishwa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika sakata hilo kunatokana na mtuhumiwa mmoja ambaye ni kiongozi katika Wizara ya Nishati na Madini, kuwa mmoja wa meneja wake wa kampeni.
“Hakuna mahali ambapo Pinda ameguswa moja kwa moja katika ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) wala Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), bali wanasema ni kwa sababu ya kampeni za urais na mhusika mmoja katika sakata hilo anatajwa kuwa kama Pinda akipata urais, yeye ndiye atakayekuwa Katibu Mkuu Kiongozi,” alisema mbunge huyo kutoka upinzani.
Jana Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu akizungumza na gazeti hili, alisema sakata hilo linatakiwa liishe kwa kuwa linaumiza uchumi wa nchi kwa kuwa mtambo wa IPTL ni matatizo.
“Hili jambo kwa namna yoyote lazima liishe na kwamba mwisho wake ni bora tutaifishe ule mtambo na ufie mbali,” alisema Mangungu.
Alisema linatakiwa liishe kwa kuwa limekuwa ni jambo la kushutumiana kila upande kitu ambacho si kizuri, na kwamba Bunge linapaswa kusimama kuonyesha makali yake.
“Ni mzigo kwa wananchi hivyo lifike mwisho. Ni heri shari yenye heri kuliko heri yenye shari,” alisema Mangungu.
Mbunge wa Ole (CUF), Rajabu Mohammed Mbarouk alisema sakata hilo limetokea juu na sasa limefika chini na kukwamisha mambo mengine yasifanyike.
“Bunge haliwezi kuisha kwa kuwa linagusa masilahi ya watu wengi, pia linagusa masilahi ya chama. Hili hata lijadiliwe bungeni haliwezi kuisha hivyo,” alisema Mbarouk.
Alisema ni jambo la ajabu kama alivyosema Zitto kwamba halikufaa kufanyika kwenye nchi ambayo ina dola, bali lingefanyika kwenye nchi ambazo hazina mhimili wa dola kama Somalia.
“Haya mambo yanaweza kumwangusha Waziri Mkuu na wengine, hivyo ni jambo zito,” alisema Mbarouk.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani kuridhia Itifaki ya Uzuiaji wa Vitendo Haramu dhidi ya Miundombinu jana, alisema viongozi kama wabunge na mawaziri wametajwa kupiga dili katika akaunti ya Tegeta Escrow kwa kuwa viongozi wa Serikali hawaonyeshi dhamira njema katika kuheshimu misingi ya utawala bora na ndiyo maana wezi na mafisadi wanaotakatisha fedha kiharamu wameendelea kuachwa.
Alisema katika uchotwaji wa fedha hizo, Serikali imedhihirisha wazi kwamba ufisadi ni sehemu ya maisha ya baadhi ya mawaziri na watendaji wa Serikali.
“Ni aibu na majanga kwa Waziri Mkuu na mawaziri wengine kusema kwamba suala la Escrow haliwezi kuzungumzwa bungeni kwa sababu eti liko mahakamani, jambo linaloashiria Waziri Mkuu anakusudia kuwalinda wale wanaotajwa kuchota fedha hizo,” Machali alisema na kuongeza:
“Mbaya zaidi ni pale inapoonekana wazi mhimili wa Bunge unaingiliwa na mhimili mwingine unaotajwa kuliandikia Bunge barua likitaka kutojadiliwa sakata la Escrow jambo ambalo ni dharau kwa Bunge.”
Kwa upande wake, Zitto ambaye kamati yake inapitia ripoti hiyo hakutaka kuzungumzia chochote kuhusu sakata hilo lakini juzi aliwataka wabunge wajiandae kupambana na taarifa atakazoziwasilisha mezani mara tu ripoti hiyo itakapokabidhiwa bungeni kwa ajili ya majadiliano.
Escrow yavuka mipaka ya nchi
Sakata la utoroshwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow ambalo linawaandama baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali limejitokeza kwa sehemu kubwa katika baadhi ya magazeti ya nchi za Magharibi yaliyohoji jinsi Serikali inavyoingiwa na kigugumizi cha kulipatia ufumbuzi sakata hilo.
Magazeti hayo likiwamo DailyMail la Uingereza ambalo lililowahi kufichua kuwapo kwa vitendo vya ufisadi katika uwindaji wa wanyamapori kulikolisababishia taifa hasara kubwa, lilisema kuwa Tanzania inaendelea kuandamwa na jinamizi la ufujaji wa mali ya umma.
DailyMail limesema wabunge wameibana Serikali wakitaka kujadiliwa kwa ripoti ya Escrow ili kuliokoa taifa ambalo tayari limeanza kuonja machungu ya kusitishiwa misaada kutoka kwa wafadhili wa kigeni.
Katika ripoti yake hiyo ambayo imelinukuu Shirika la Habari la Reuters, DailyMail ilisema rushwa ni ugonjwa unaoendelea kuiandama Tanzania na kwamba vitendo hivyo sasa vimevuka mipaka na kuwakwaza wawekezaji wa kigeni.
Limesema kuwa Tanzania ambayo hivi karibuni ilitangaza kugundua hifadhi kubwa ya gesi iko katika njiapanda na bado haieleweki hatima yake hasa baada ya Serikali kuonyesha kuwa haiko tayari kuruhusu ripoti hiyo ijadiliwe hadharani.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment