Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday, 24 November 2014

QARES ASEMA, CCM HAKUNA ANAYEFAA KUWA RAIS

Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Pili na ya Tatu, Mateo Qaresi. PICHA|MAKTABA 
Na Joseph Lyimo, Mwananchi
Babati. Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Pili na ya Tatu, Mateo Qaresi amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa hakina mgombea mwenye sifa ya kuwa rais wa awamu ya tano wa Tanzania.
Qaresi ameyasema hayo hivi karibuni mjini Babati katika mahojiano maalumu na gazeti hili, ambapo alidai kwamba CCM kwa sasa imepoteza sifa zote za kutawala kwa sababu hakina tena misingi ya kuwatetea wafanyakazi na wakulima bali sasa ni chama cha matajiri.
Mwanasiasa huyo ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Babati kwa tiketi ya CCM, alisema kuwa chama hicho hakiwezi kutoa rais bora anayeweza kuwavusha Watanzania walipo sasa na kuwapeleka mahali pazuri zaidi kwa sababu ina viongozi wasiojiamini, hawawezi kutoa uamuzi mgumu katika kuendesha nchi.
“Mpaka sasa kwa watu wanaotajwa tajwa kuwa watawania urais kwa CCM, mimi naona hakuna mwenye sifa kwa sababu CCM haiwezi kumpitisha kiongozi mzuri na mwadilifu kwa kuwa watu wanatumia fedha na huwezi kupata kiongozi mzuri kwa kutumia fedha,” alisema Qaresi na kuongeza:
“Kuna ambaye ameshatangaza kwamba mwakani atagombea urais na ameshatenga fedha za kufanyia kampeni kwani ameanzisha kampuni yake na hana tatizo, fedha anazo za kutosha. Maana yake nini? Kwamba ana uwezo wa kuwahonga watu, sasa mtu wa namna hiyo anafaa kuwa rais?”
Kauli hiyo ya Qaresi imekuja wakati makada mbalimbali wa CCM wameshatangaza nia, wengine wakitajwa kutaka kuwania nafasi hiyo ya juu zaidi katika uongozi nchini.
Baadhi ya waliotangaza nia ni January Makamba ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangallah.
Pia, wanaotajwa yumo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Stephen Wasira ambaye ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Dk Asha Rose Migiro, Waziri wa Sheria na Katiba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Hata hivyo, Qaresi alisema kazi ya urais ni ngumu na siyo ya mchezo kama wanavyodhani baadhi ya watu ndio maana utaona kuwa mtu hajamaliza hata miaka mitano katika ubunge, anatangaza nia ya kutaka kugombea urais.
“Miaka mitano hajaimaliza anataka kugombea urais, wakati hana historia kubwa ya uongozi. Wengine wanajulikana kuwa wana kashfa nyingi, lakini bado wanataka nafasi hiyo,” alisema.
Alisema kwamba nchi ikipata rais legelege, haitachukua muda mrefu itachafuka, kwani ataendeleza mambo ya kilegelege yanayoendelea na kuacha watu wenye fursa waifisidi nchi hii kwa kuwa hakuna mtu anayewachukulia hatua.
“Hivi sasa tangu juu mpaka chini, hakuna kinachoendelea. Watendaji wengi wamekata tamaa, uwajibikaji umekuwa duni, kwani watu wanakwenda tu kazini, ili mradi wanapokea mshahara. Tukimpata rais legelege, hatuna miaka miwili nchi itachafuka,” alisema Qaresi na kuongeza:
“Wakati fulani, Rais Ali Hassan Mwinyi alituambia mtoto akibebwa mgongoni huangalia kisogo cha mama yake, tukamuuliza maana yake nini mzee? Akasema: “Mkiwa na kiongozi mzuri, nanyi watu wote wa chini yake mnaangalia anachokifanya pia kufuata anachokifanya. Hivyo tukiwa na viongozi wabovu, mambo yanakwenda kombo na tukiwa na uongozi mzuri, watu wote wanashika adabu na wanamfuata.”
Alisema kuwa, taifa kwa sasa limekithiri kwa ubinafsi na hakuna anayejali masilahi ya taifa na hajui nchi itafikia wapi kutokana na uongozi uliopo, kwani viongozi wanashindwa kufanya uamuzi mgumu na kurekebisha mfumo uliopo.
“Kiongozi jasiri kabisa atakayefanya uamuzi mgumu hayupo CCM atakayerekebisha mfumo uliovurugika wa nchi hii, itakuwa kazi sana kwani hivi sasa dawa za kulevya, ujangili, umaskini umekithiri na rushwa imetawala hadi kusababisha CCM imekuwa chama cha matajiri na bila kuwa na fedha, huwezi kuchaguliwa kuwa kiongozi,” alisema Qaresi na kuongeza:
“Unasema uchumi umekua, lakini huoni kukua kwa uchumi kwa kuangalia hali za wananchi, maisha yanazidi kuwa magumu, hilo tatizo ni kubwa sana.”
Rais ajaye aweje?
“Rais ajaye, lazima awe ni mtu makini, jasiri, mwelewa na mwenye maono ya juu, anayeweza kurekebisha mifumo hii ya utawala iliyovurugika.
Mifumo ya uongozi imevurugika, uchumi umevurugika, shughuli za kijamii zimevurugika nafikiri nchi inaelekea kufilisika,” alisema Qaresi.
Kwa masikitiko Qaresi alisema kuwa katika CCM mtu makini, mwadilifu, mwenye historia nzuri hawezi kupitishwa na CCM ingawa inasemekana ni Chama cha Mapinduzi, lakini ukweli ni kuwa kwa sasa ni chama cha matajiri, ni chama cha watu wenye fedha siyo kama kilichokuwa chama chenye itikadi safi inayoeleweka.
“Hivi karibuni nilisoma kwenye Gazeti la Mwananchi kuwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam alisema nchi inatakiwa kuongozwa na rais dikteta watu wakadai hapana, lakini kuna udikteta wa aina nyingi,” alisema Qaresi.
Alisema kiongozi asiye msemakweli ni mbovu na hawezi kuongoza wananchi kwani atakuwa anawadanganya kila wakati, atakuwa mnafiki kutokana na kushindwa kusema ukweli bila kuficha.
“Kiongozi ambaye siyo msema ukweli ni kiongozi mbovu kweli kweli kwa sababu atawadanganya watu kuwa nitawafanyia hiki ilihali anatambua kuwa hawezi kufanya jambo hilo,” alisema Qaresi na kuongeza:
“Wewe unakwenda kugombea ubunge unasema mkinichagua nitawajengea zahanati, kwa nini kabla hujachaguliwa hukujenga hiyo zahanati? Mkinichagua mimi kila mtoto atakwenda shule kwa nini hukuwapeleka shule kabla ya kuchaguliwa? Viongozi wa sasa wanatumia unafiki na fedha, ni wabovu kwelikweli.”
Qaresi alisema kuwa asilimia kubwa ya viongozi wa sasa nchini ni wabovu na siyo jambo la kuficha kwani wanaonekana kwa macho, kutokana na vitendo wanavyovifanya kwa wananchi wao wanaowaongoza.
Akizungumzia upande wa upinzani, Qaresi aliwataka kuungana na kumteua mtu mmoja mwenye uwezo wa kugombea nafasi hiyo ili aweze kupambana na mgombea wa CCM na kwamba wakijipanga vizuri wanaweza kuiangusha CCM.
Kilimo kiboreshwe
Kwenye suala la kilimo Qaresi alisema kuwa kukwama kunatokana na tatizo viongozi hawajui pakuanzia kati ya kutoa ruzuku kwenye mbolea na mbegu au kumwelimisha mkulima, kwani unaweza kutoa mbolea na mbegu ya ruzuku watu wasichukue au wasipande vizuri au wasihangaikie hilo kabisa.
Alisema viongozi wanatakiwa watambue mahali pa kuanzia na siyo kutoa ruzuku pekee kwani miaka ya nyuma kulikuwa na Benki za Ushirika na Maendeleo Vijijini zilizokuwa zinawawezesha na kuwanufaisha wakulima.
“Benki hiyo ilikuwa inatoa mbolea kwa wingi kwa wakulima na kurundikwa shuleni, wanagawa kupitia vyama vya ushirika na hakukuwa na mtu anachukua mbolea ya chumvichumvi, kwani ilikuwa inajulikana kwa kuharibu ardhi na kunyonya mimea,” alisema Qaresi.
Alieleza kuwa wakulima walikuwa wanaona ni vyema kutumia mbolea kama samadi, mboji na kufukia mabua shambani, kuliko kutumia mbolea hiyo ya chumvi chumvi, ambayo inaharibu ardhi na kuifanya iwe kama.
Hata hivyo, anasema hivi sasa maofisa ugani hawawatembelei wakulima vijijini na kuwapa elimu ya kilimo kinachoweza kuwanufaisha, hivi sasa wakulima wanatumia mazoea.
“Hawapiti kwenye mashamba ya wakulima na kuangalia namna wanavyolima au mifugo wanavyofuga, kwani siku hizi watu wanajali maslahi yao pekee na elimu ya zamani ya kilimo ya hata kuweka matuta shambani hakuna,” anasema Qaresi na kuongeza:
“Enzi zile, mimi nilipokuwa mdogo wakati wa ukoloni nilikuwa nachunga ng’ombe, kulikuwa na bwana shamba wa kizungu anayetembelea mashamba yetu mara kwa mara na akikukuta unachungia ng’ombe shambani, anakuweka kwenye matuta na kukuchapa viboko kisha unatozwa faini. Lakini leo hakuna wafuatiliaji wala waelimishaji.”
Alieleza kuwa kilimo cha sasa kinafanywa na wakulima kwa mazoea na hawatumii kamba wakati wa kupanda mbegu, kwani hufuata nyuma ya trekta na kuangusha mbegu kwenye mashimo bila kuwa na utaalamu.
Qaresi alitaja soko kuwa pia ni tatizo hivi sasa kwa wakulima kwani wanalima mazao na kuvuna kwa wingi lakini bei yake bado inakuwa chini, mfano ni mwaka huu wananchi wamelima mazao mengi lakini soko la kuuzia halipo.
“Hivi sasa gunia moja la mahindi lenye uzani wa kilo100 unanunua kwa kati ya Sh24,000, Sh25,000 au Sh30,000 bei ambayo haikidhi mahitaji ya wakulima. Kwa hali hiyo, mkulima hawezi kuendelea kiuchumi,” alisema Qaresi.
Mambo ambayo hatayasahau
Qaresi anasema hatasahau mwaka 2002 alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, kulitokea tetemeko la ardhi wilayani Rungwe, ambapo nyumba kadhaa zilianguka na yeye kunukuliwa vibaya kuwa ametoa kashfa na kudharau nyumba za wananchi wa eneo hilo kuwa ni mbovu hata kuku anaweza kuzipiga teke zikabomoka.
“Walinilisha maneno yasiyo kweli na watu walitafsiri vibaya kwa kuzungumza maneno mengi ila nyumba zao zilikuwa mbovu kweli kweli. Nilijaribu kuwaambia ukweli kwamba nyumba walizojenga siyo madhubuti kwani nyingine zilijengwa kwa matofali mabichi na mvua zinaponyesha matofali yanaloa,” alieleza Qaresi.
Jingine ni lile la mwaka 2003 akiwa mkoani humo, mahabusu 17 walifariki dunia na wengine wakaumia, kutokana na mrundikano katika chumba kidogo kwenye kituo cha polisi wilayani Mbarali wakati huo Kamanda wa Polisi wa Mkoa akiwa IGP mstaafu Said Mwema.
“Jambo jingine ambalo sitaweza kulisahau ni wakati nikiwa serikalini nilipoanza kazi mwaka 1975 kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, Rashid Kawawa (marehemu), tulitumwa Urambo mkoani Tabora na Naibu Waziri Patrick Qoro kufuatilia migogoro ya wananchi kuhusu suala la kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa.
“Kulikuwa na malalamiko ya wananchi kuhamishwa vibaya kwenye vijiji hivyo vya ujamaa, baada ya wabunge kulalamika kuhusu tatizo hilo akiwemo mbunge wa Urambo Said Masanywa.
“Badala ya kutumwa na mtendaji mkuu wa Serikali ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi, nilitumwa mimi, Naibu Waziri Patrick Qoro na mtu mmoja aitwaye Majaliwa, tuliambiwa tukachunguze kujua ni malalamiko yapi na wamehamishiwa sehemu gani.
“Kumbe huku nyuma kwa sababu kuhamisha watu lilikuwa ni agizo la Serikali, mkuu wa mkoa huo alikwenda Dar es Salaam na kulalamika kuwa yeye anafanya shughuli ya kuhamisha watu vijijini, lakini Ofisi ya Waziri Mkuu imetuma watu kuvuruga watu vijijini,” alisema Qaresi.
Alifafanua kuwa baada ya Waziri Mkuu Kawawa kuelezwa hivyo alimuuliza Katibu Mkuu kwa nini ametuma watu wakavuruge zoezi hilo, ndipo Katibu Mkuu akasema yeye hajatuma watu, hivyo wakatakiwa waitwe warudi haraka japokuwa wakati huo hakukuwa na simu za mikononi ila walirudi wakiwa na taarifa yao mkononi.
Alisema walipofika Dar es Salaam wakaitwa kwa WaziriMkuu Kawawa na wakaeleza kuwa walitumwa na wana barua mkononi, baadaye wakaambiwa wasubiri hatua za kinidhamu na taarifa ya kile walichokifanya Tabora hawakuitoa, walihofu wataonewa kwa kosa ambalo siyo la kwao ila baadaye wakasamehewa.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment