Mangara Tabu Mangara (kulia) na kocha Tambwe Leya (kushoto) mwaka 1974.
WENGI wamekuwa na maelezo tofauti kuhusu chanzo cha mgogoro wa Yanga kilichozaa timu ya Pan African mwaka 1977. Wapo wanaosema kupoteza ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1976 ndiko kulikosababisha kutokea mgawanyiko. Lakini maelezo hayo si sahihi, kwani wakati ubingwa huo unatoweka Januari 1976 mjini Mombasa, Kenya, tayari kulikuwa na mgawanyiko wa Yanga Raizoni na Yanga Kandambili, na zaidi tayari uchaguzi mkuu ulikuwa umefanyika (Desemba 1975) na Mangara Tabu Mangara kudondoshwa.
Kwanza kabla ya kuingia kwa undani kuhusu mgogoro huo ni vyema mtu akaielewa kwa undani historia ya Yanga kuanzia mwaka 1968. Wengi wanasema kwamba Mangara Tabu ndiye aliyefanikisha ujenzi wa jengo la Yanga la Jangwani. Si kweli! Suala la ujenzi wa jengo lile lilianza tangu mwaka 1968, kweli, lakini kwanza lilitanguliwa na uandaaji wa Katiba ya kwanza ya Yanga.
Katiba hiyo iliandaliwa na kisha kuchapishwa mwaka huo, lakini ndani yake kulikuwa na vipengele ambavyo baadaye vikaja kuonekana vinawabana baadhi ya watu. Mojawapo ya vipengele hivyo ni kile kilichoelezea kuhusu udhamini wa jengo la klabu lililokuwa linatarajiwa kujengwa, ambacho kilisema kwamba, mdhamini ni lazima awe na nyumba iliyojengwa kwa usimamizi au utaratibu wa serikali na pia awe na pato la shilingi 1,500 kwa mwezi.
Rais wa Yanga wa wakati huo, Kondo Kipwata ndiye aliyestahili sifa zote za maendeleo ya klabu hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa tatu, pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Kaunda. Vyote hivi vilijengwa kutokana na michango mbalimbali ya wananchi, serikali (ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar) na taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Wazo la ujenzi lilipotolewa Mzee Kondo Kipwata alikuwa na nyumba zake, lakini kutokana na kutokuwa na hati za kiserikali na kutokuwa na kazi, kipato chake hakikuwa kile kilichoainishwa kwenye Katiba, hivyo kumuwia vigumu kuwa mmoja wa wadhamini wa jengo hilo. Wakati huo Makamu wa Rais, Mangara Tabu, alikuwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na kipato chake kwa mwezi kilikuwa shilingi 1,500. Yeye ndiye aliyeandaa Katiba hiyo na kuichapa, hivyo ilikuwa rahisi kwake kuweka kipengele hicho.
Lakini tayari Mangara alikuwa akipingwa na wanachama wengine kama Mathew Kashindye na David Mwambungu. Hali hiyo ikamfanya Mangara kutafuta njia ya kumwezesha kuwa mmoja wa wadhamini wa jengo hilo, na kwa vile alikuwa na nyumba Mtaa wa Swahili na pia alikuwa na kazi ya mashahara, wana-Yanga wakaamua kumweka kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi.
Hata Rais Julius Kambarage Nyerere alipotembelea ujenzi huo mwaka 1970 alikuta Mangara ndiye msimamizi mkuu. Wakati huo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia klabu ya Wananchi (zamani ikijulikana kama African Sports), chini ya Sheikh Abeid Amani Karume, ilikuwa imetoa shilingi milioni 2.0 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo. Jiwe la Msingi liliwekwa na Sheikh Karume mwaka 1971.
Pamoja na hayo, bado kuliendelea kuwepo na migogoro. Mwanzoni mwa mwaka 1973 Mzee Kondo Kipwata alifariki dunia, na kwa mujibu wa Katiba, Makamu wake, Mangara Tabu, ndiye aliyekaimu nafasi yake. Lakini katika mechi ya kwanza chini yake dhidi ya Simba mwaka huo 1973, Yanga ilichapwa bao 1-0 na kisha kuvuliwa ubingwa wa Taifa ilioushikilia kwa miaka mitano mfululizo (1968-1972). Kipigo kile kikachochea kabisa mgogoro uliokuwa unazidi kukomaa, hivyo wanachama wakaamua kumshinikiza Mangara kuhakikisha kwamba timu inaandaliwa vya kutosha kwa ajili ya michuano ya Ubingwa wa Taifa wa mwaka 1974.
Ndipo mwaka 1974 Yanga ikaendea kuzuru Brazil kwa ajili ya kujiandaa na ligi hiyo iliyofanyika Mwanza. Baada ya kurejea Yanga ilikuwa inatisha na ilipoingia fainali ikakumbana na Simba Jumanne ya Agosti 10, ambapo ilishinda kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza. Mapema mwaka 1975 ikaivua tena Simba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mjini Zanzibar kwa kuifunga mabao 2-0.
Pamoja na mafanikio hayo, bado wanachama waliendelea na mgogoro huo na walionyesha dhahiri kutokuwa na imani na Mangara hasa kutokana na kushindwa kujengwa kwa viti (jukwaa) kwenye Uwanja wa Kaunda ingawa wanachama walikuwa wamechangishwa fedha kwa ajili hiyo. Mpaka leo haijulikani fedha zile ziliingia wapi.
Mangara alikuwa ametengeneza sefu ya fedha kwenye klabu ya Yanga pale Jangwani na nyingine, kwa mujibu wa waliokuwepo, aliiweka nyumbani kwake. Wachezaji au wanachama walipokuwa na shida ya fedha walikwenda kupanga foleni pale nyumbani kwake. Kitendo hicho kilikuwa kinapingwa sana na kocha Tambwe Leya, ambaye alikuwa akiidhinisha fedha kwa wachezaji wenye matatizo. Wale wanachama waliokuwa wakimuunga mkono Mangara walikuwa wakijiita ‘Raizoni’, yaani watoto wa mjini wanaojua kuvaa, na wale wengine waliokuwa wakimpinga walionekana makabwera tu. Ni katika mgawanyiko huo, ambapo siku moja baada ya timu kumaliza mazoezi pale Kaunda, wanachama fulani wakamzonga mchezaji Juma Shaaban ‘Uncle J’ na kuanza kumshambulia kwa maneno, lakini kipa huyo akasema, ‘Yaani hata nyie mnaovaa kandambili mnaweza kusema mbele ya wenye fedha?!’ Hapo ndipo lilipoanzia neno ‘Yanga Kandambili!’
Wakati huo Yanga ilikuwa inamiliki magari matano. Kulikuwa na Isuzu iliyokuwa na uwezo wa kubeba abiria 65, Isuzu nyingine ya kubeba watu 30, Ford ya kubeba watu 35, Pundamilia Isuzu ya kubeba watu 18, ambayo mara nyingi ilikuwa ikibeba wachezaji wanapoingia uwanjani, na gari aina ya Honda iliyokuwa ikitumiwa na kocha Tabwe Leya.
Wakati Mangara alikuwa kaimu Rais wa klabu, mdogo wake Mtaruke Mangara alikuwa Makamu wa Rais, Katibu Mkuu alikuwa David Mwambungu, Katibu Msaidizi alikuwa Mohammed Misanga, Mweka Hazina alikuwa Ngakonda, Mweka Hazina Msaidizi alikuwa Punzi, Abdul Masoud (mtangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam –RTD sasa marehemu) alikuwa Katibu Mwenezi na Mathew Kashindye alikuwa Katibu Mipango.
Lakini baada ya kutwaa ubingwa kule Nyamagana mwaka 1974 mgogoro ukazidi na wanachama wakashinikiza uchaguzi ufanyike. Serikali ikaona kwamba hali hiyo ingeweza kuvuruga amani nchini hasa katika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge wa mwaka 1975, hivyo ikaamua kuwafungia Mwambungu na Kashindye kutojishughulisha na michezo maisha.
Tamko hilo la serikali halikuwakatisha tamaa wanachama, ambapo mwaka 1975 wakaamua kufanya mapinduzi baridi kwa kuchagua uongizi wa muda uliokuwa chini ya uenyekiti wa Omar Mussa Chitenje pamoja na Mohammed Misanga (Katibu Mkuu), Punzi (Mweka Hazina), Edson Mwandemane (Katibu Mipango), na Abdul Masoud (Katibu Mwenezi). Hatua hiyo ya kufanya mapinduzi baridi ilifuatia kutolewa kwa Yanga na Enugu Rangers ya Nigeria katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika mnamo Juni 1975. Katika mchezo wa kwanza huko Lagos timu hizo zilitoka suluhu, lakini ziliporudiana mjini Dar es Salaam zikafungana 1-1, hivyo Wanigeria wakapata ushindi wa sheria ya bao la ugenini.
Wanachama wa Yanga walimtuma Hamad Abdallah Kiluvia kwenda kuipokea timu ya Enugu. Alipofika Uwanja wa Ndege alianza kusalimiana na golikipa wa Enugu, Emmanuel Okala, kipa mrefu sana ambaye pia alikuwa akiidakia timu ya taifa, Green Eagles, wakati huo (sasa inaitwa Super Eagles).
Lakini upande wa Mangara inasemekana haukuwa radhi kuona Yanga inashinda, hivyo baadhi ya waliokuwa wakimuunga mkono wakawashawishi wachezaji wa Yanga wacheze chini ya kiwango. Wachezaji hao wakasikika wakisema kwamba, siku hiyo ya mchezo hakuna mtu kufunga goli. Maneno hayo yalitamkwa wakati wako ndani ya gari wakienda uwanjani siku hiyo ya mchezo, lakini viongozi hawakujua. Hata kocha Tambwe Leya hakuwa na habari.
Baada ya kuingia uwanjani, Enugu ndio walianza kupata bao, lakini baadaye Kitwana Manara akasawazisha, hali iliyosababisha kutokee ugomvi mkubwa hapo uwanjani baina ya kambi ya Mangara, ambao walikuwa wakilaumu kwa nini Kitwana alifunga bao hilo. Hata hivyo, matokeo yakabaki 1-1 na Yanga ikawa imetolewa.
Nilipata kuzungumza na mmoja wa viongozi wa Yanga wa wakati huo, Kennedy Kanyanka, ambaye alikuwa na haya ya kusema: “Baada ya wanachama kugundua njama hizo, ndipo walipofanya uchaguzi Julai 1975 na Mwenyekiti akawa Omar Mussa Chitenje. Hata hivyo, serikali ikaingilia kati na kusema kwamba uchaguzi huo ulikuwa batili kwa sababu walichofanya wanachama ni kama kuteua Kamati ya Muda tu kinyume na Katiba.
“Lakini mgogoro huo ulipoendelea ikabidi serikali iridhie kufanyika kwa uchaguzi mwingine wa Yanga mnamo Desemba 28, 1975, Jumapili, chini ya usimamizi wa Umoja wa Vijana wa TANU (TLY). Ndipo kwa mara nyingine akachaguliwa Omar Mussa kuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti alikuwa Juma Shamte, Katibu Mkuu alikuwa Mohammed Misanga, Katibu Msaidizi Hassan Lupindo, Katibu Mwenezi Abdul Masoud, Katibu Mipango Kennedy Kanyanka, Mweka Hazina Kanduru Msusa, Mweka Hazina Msaidizi Edson Mwandemane,” anakumbuka.
Unaweza kuona kwamba mpaka wakati huo tayari kulikuwa na makundi mawili; Kundi la Mangara na kundi la wanachama wengine, wakiwemo na wale waliochaguliwa kushika uongozi. Lakini kundi la Mangara lilikuwa linaungwa mkono na serikali, ndiyo maana hata baada ya Yanga kuvuliwa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mjini Mombasa, Kenya mwaka 1976, baada ya uongozi kupeleka basi la kukodi (UDA-Ikarus Kumbakumba) kule Uwanja wa Ndege ili kuwapokea wachezaji, wachezaji hao wote hawakuingia kwenye basi hilo na badala yake wakaingia kwenye magari ya mawaziri, mkuu wa mkoa, RPC na magari mengineyo ya serikali. Kitendo hicho kilizidisha hasira za wanachama, ambapo wakaazimia kuwafukuza wote na kuanza kuunda kikosi kipya.
Serikali ikatoa amri ya kutoruhusu uandikishwaji wa klabu ya michezo kutokana na migogoro. Wachezaji wale walioondoka awali walitaka kujiunga na klabu moja pale Manzese, lakini kutokana na amri hiyo ya serikali, ikabidi watimkie Morogoro walikojiunga na timu ya Nyota Afrika iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Taifa.
Katika mahojiano mwaka 2002, Kanyanka alipata kuniambia: “Viongozi wa serikali waliokuwa nyuma ya Mangara, Mshindo Mkeyenge na Shiraz Shariff, walikuwa Waziri wa Michezo, Utamaduni wa Taifa na Vijana Mirisho Sam Hagai Sarakikya, Mkuu wa Mkoa wa Pwani (wakati huo) Clement Rwegasira, Katibu Mkuu wa Rais Sammy Mdee, Mkurugenzi wa Radio Tanzania Dar es Salaam Paul Andrea Sozigwa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani (Dar) Ismail Lazaro, ambao waliona Mangara alikuwa ameonewa tu na wanachama hao,” anasema.
Baada ya kutimuliwa kwa wachezaji hao, Yanga haikuwa na kikosi kibaya sana, ingawa mwaka huo 1976 walifungwa na Simba 2-1. Hali hiyo ikawashangaza hata wapinzani wao, na hata serikali nayo ikachanganyikiwa kuona timu iliyokuwa na migogoro mingi kama Yanga iliweza kuunda kikosi imara katika muda mfupi. Hii ilitokana na kuwa na kocha mzuri, Tambwe Leya, ambaye aliamini vijana ndio walikuwa nguzo imara.
Ndipo likatolewa agizo la kuwataka Tambwe Leya na kocha wa Simba wa wakati huo, Nabby Camara kutoka Guinea, kuondoka nchini haraka sana kwa madai kwamba walikuwa makachero wa Shirika la Kijasusi la Marekani (Central Intelligence Agency – CIA). Mwaka 1977 ndipo ikazaliwa Pan African baada ya wachezaji wale kurejea kutoka Morogoro na pia ndio mwaka ambao Yanga ilichabangwa na Simba mabao 6-0.
Awamu ya pili baada ya kuondoka Mangara na kipindi cha Mzee Omar Mussa Chitenje kumalizika ilikuwa ya Dakta Daudi Aziz aliyekuwa Mwenyekiti na Christopher Mahimbo (wakati huo alikuwa Meneja Mkuu wa UDA) kuanzia mwaka 1978-81. Awamu iliyofuata ilikuwa ya Hassanar Salum (1981-84), ambaye alikuwa Hakimu katika Mahakama ya Magomeni kabla ya kuwapisha akina William ‘Bill’ Bandawe (1984-87).
Uongozi wa Bill Bandawe ulikuwa na matatizo makubwa sana na almanusura mgogoro huo uzae matunda kama yale ya mwaka 1976.
Huu ndio ukweli kuhusu mgogoro uliozaa Yanga Kandambili na Yanga Raizoni.
NB: Daniel Mbega ni mwandishi mkongwe na mtafiti wa michezo nchini ambaye anaandaa vitabu vya ‘UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ na ‘SIMBA VS YANGA: VUTA-NIKUVUTE’.
No comments:
Post a Comment