Na Daniel Mbega
ILIKUWA jioni yenye majonzi na simanzi kupindukia kwa wachezaji, viongozi na wapenzi wa Sunderland Jumamosi ya Juni Mosi, 1968, kwani siyo tu siku hiyo walipata kipigo kisichovumilika cha magoli matano kwa gurudumu toka kwa Yanga, bali pia kipigo hicho kilitia saini Yanga kuchukua ubingwa wa soka nchini.
Kipigo hicho kilikuwa kikiuma zaidi ikikumbukwa kuwa, katika mechi ya kwanza ya ligi hiyo mwaka huo baina yao, mchezo ulivunjika baada ya fujo kuibuka kufuatia Yanga kujipatia goli la kwanza kwenye dakika ya 28 kupitia kwa Kitwana ‘Popat’ Manara. Hii sasa ilikuwa ni mechi ya marudiano ili kumpata bingwa.
Vinara wa Yanga katika mechi ya marudiano walikuwa washambuliaji hatari wa timu hiyo, Maulid Dilunga na Salehe Zimbwe waliofunga magoli mawili kila mmoja, na Kitwana Manara alifunga goli moja lililokamilisha kifo cha Sunderland siku hiyo.
Katika mchezo huo wa Ligi ya Taifa uliofanyika kwenye Uwanja wa Ilala (sasa Kumbukumbu ya Karume), Yanga iliinyanyasa zaidi Sunderland ikielekea kuumudu mchezo katika kila idara kuliko wapinzani wao na kuwadhibiti ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kucheza watakavyo.
Awali Sunderland walikuwa wamelalamika kutaka mchezaji wao Emmanuel Mbele, aliyefungiwa kutocheza mpira kwa kipindi cha miezi 6 kwa kusababisha mchezo wa kwanza kuvunjika, afunguliwe. FAT ikakataa kwa kufuata sheria, lakini Yanga, wakiwa wanajiamini, wakaiomba FAT imwachilie huru mchezaji huyo aliyekuwa tegemeo kubwa la ushambuliaji kwa timu yake. Hivyo, akaachiliwa, lakini bado maji yakawa mazito kwa Sunderland.
Ukiondoa rafu za hapa na pale zilizojitokeza mara kwa mara, mchezo ulikuwa wa kuvutia ambapo timu zote zilipigana kiume ingawa hatma ya yote Yanga walitoka kifua mbele wakiwa na ushindi mkubwa uliowachukua Sunderland (baadaye Simba) karibu miaka 10 hadi mwaka 1977 walipokuja kulipa kisasi kwa kushinda kwa magoli 6-0, kipigo ambacho kinaelezewa kuwa kilitokana na Yanga kuwa ndio kwanza imetoka kwenye mgogoro mkubwa uliopelekea kufukuzwa kwa wachezaji wake wazoefu wote, hivyo kuingia uwanjani ikiwa haijatengemaa sawa sawa kwa mikiki mikiki ya ligi.
Katika dakika ya 10 ya mchezo huo, Omari Kimimbi wa Sunderland aliumia baada ya kugongana na golikipa wa Yanga, Elias Michael, katika harakati za kuwania mpira. Kama utakumbuka vyema, mwaka 1974 kwenye mchezo mwingine wa ligi kati ya timu hizo mbili, golikipa Elias Michael wa Yanga na marehemu Willy Mwaijibe wa Sunderland waligongana kiasi cha kulazimika kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando mjini Mwanza kwa matibabu ya haraka. Pambano hilo lilifanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana.
Karamu ya magoli ya Yanga katika mchezo wa Juni Mosi, 1968 ilianza kwenye dakika ya 18 pale Durban wa Sunderland alipounawa mpira kwenye mstari wa goli alipokuwa akijaribu kuokoa huku golikipa wao, Mbaraka Salum akiwa ‘amekwenda marikiti’. Kufuatia kitendo hicho cha kuunawa mpira, Yanga ilipewa penati ambayo Maulid Dilunga hakufanya makosa kuzitikisa nyavu za Sunderland kuandika goli la kwanza.
Jitihada zote za Sunderland kusawazisha goli hilo hazikuzaa matunda, kwani ukuta wa Yanga ulisimama imara. Alikuwa ni Dilunga tena, ambaye siku hiyo ‘control’ yake ya mpira haikuwa na mpinzani, aliyeandika goli la pili kufanya timu ziende mapumziko huku Yanga ikiongoza kwa magoli 2-0.
Kwenye kipindi cha pili, Salehe Zimbwe alifungua kitabu cha magoli kwa kupachika goli la tatu kwa Yanga kwa mpira wa kichwa baada ya kumvisha kanzu golikipa wa Sunderland, Mbaraka Salum. Sunderland walicharuka baada ya goli hilo, lakini Emmanuel Mbele ‘Dubwi’, Saidi Abdallah ‘Walala’, Adamu Athumani na Hamisi Kilomoni walikosa nafasi za wazi kabisa katika kile kilichoonekana kama ‘Sikio la kufa halisikii dawa’.
Vibao vya magoli viliendelea kusomeka 3-0 hadi zikiwa zimesaliwa dakika nne tu Sunderland waliporuhusu magoli mawili ya haraka haraka. Kwenye dakika ya 87 Dilunga alimmegea krosi nzuri Kitwana Ramadhani Manara aliyeachia kombora safi na kufunga goli la nne kwa Yanga kabla Salehe Zimbwe naye hajaipangua ngome ya Sunderland na kuweka mpira kimiani kufanya kitabu kifungwe huku Yanga ikijidai na ushindi wa magoli 5-0, ambao hawajaukaribia tena hadi hii leo katika mechi dhidi ya watani wao wa jadi.
Kwa kuwa dakika zilikuwa chache, Yanga walianza mchezo wa mzaha na maonyesho (show-game) ili kuvuta muda. Wachezaji wa Sunderland walikatishwa tamaa na kuudhika sana. Katika mzaha wao, Yanga walikuwa wanakokota mpira kutoka golini kwa wapinzani wao hadi golini kwao na kumpasia mlinda mlango wao Elias Michael. Naye aliurudisha mpira kwa wachezaji wa ndani, ambao walifanya dhihaka kwa wachezaji wa Sunderland huku wakicheka na kufunga soksi au kufanya kama wanavua jezi au kaptura zao.
Wakati ambapo Emmanuel Mbele na Adamu Athumani wa Simba walionywa kwa mchezo mbaya, Juma Bomba wa Yanga aliumia kwenye kipindi cha pili na kupelekwa hospitali kwa matibabu huku Twaha Masimenti akiingia kuchukua nafasi yake. Mechi ilisimamishwa kwa dakika tano wakati mashabiki walipovamia uwanja lakini FFU walizima vurugu hizo na mchezo kuendelea.
YANGA: Elias Michael, Kitenge Said, Hamisi Mnubi, Athumani Kilambo, Omari Kapera, Gilbert Mahinya, Awadh Gessan/Leonard Chitete, Juma Bomba/Twaha Masimenti ‘Bryson’, Kitwana Manara, Maulid Dilunga, Salehe Zimbwe.
SIMBA: Mbaraka Salum, Yusuf Salum, Ally Durban, Hamisi Kilomoni, Adam Athumani, Mussa Libabu, Omari Kimimbi, Emmanuel Mbele, Arthur Mambetta, Saidi Abdallah ‘Walala’, Ally Wage ‘Kajo’.
Mwamuzi alikuwa Bwana Banda kutoka Zambia, na alisaidiwa na washika vibendera Marijani Shaaban Marijani na Ramadhan Kahabuka wa Dar es Salaam.
NB: Makala haya ni kutoka kwenye muswada wa kitabu cha 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' cha mwandishi Daniel Mbega, ambacho kiko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com
No comments:
Post a Comment