Na Hussein Issa,Mwananchi
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema inakusanya Sh10 trilioni ikiwa ni makusanyo ya kodi kila mwaka tangu mwaka 2001.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa Mamlaka wa TRA, Rished Bade alisema kwamba mapato hayo yameongezeka tangu mwaka 2001 na kabla ya hapo mamlaka hiyo ilikuwa ikikusanya Sh800 bilioni.
Akizungumza katika ziara ya Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kukagua ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam jana, Kamishna Bade alisema kwa sasa kuna mwitikio mkubwa kwa Watanzania kulipa kodi.
Alisema miaka ya nyuma wananchi hawakuwa na mwamko wa kulipa kodi licha ya semina mbalimbali zilizokuwa zikitolewa.
“Kuna mabadiliko makubwa tunaendelea kuyashuhudia kuhusiana na mwitikio wa watu kulipa kodi bila kushurutishwa kama zamani,” alisema.
Alisema kodi za wananchi ndizo zilizotumika kutengenezea barabara kwa asilimia kubwa nchini pamoja na kuboresha miundombinu mingine.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Mapato, kutoka DRC, Deo Ruwegiza alisema wamekuja Tanzania kwa ajili ya kuzungumzia mfumo wa pamoja wa forodha.
“Tumefurahi kuja Tanzania, na tuna imani tutajifunza mengi wakati wa kubadilishana mawazo na viongozi wa TRA hapa nchini. Fursa hii ni nzuri na tutaitumia kwa manufaa makubwa,’’ alisema na kuongeza:
“Tumekuwa na ukaribu na nchi ya Tanzania katika mambo mengi hasa suala la biashara, hivyo kuwa kwetu hapa tunajifunza mengine kwa ajili ya manufaa ya nchi zote mbili.”
Alisema Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukusanya kodi na ndiyo maana wamekuja kujifunza mambo mbalimbali na kujua mbinu ambazo zimetumika kufanikisha makusanyo hayo.
“Urafiki uliopo kati ya Tanzania na DRC ni muda mrefu na lengo lake ni kusaidiana mbinu mbalimbali za kuleta maendeleo kwenye nchi hizo,” alisema.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment