Rais Jakaya Kikwete
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa endapo mipango yote itakwenda kama inavyoandaliwa,
Watanzania watapata nafasi ya kuipigia kura ya maoni Katiba
Inayopendekezwa, ili kukamilisha mchakato wa Tanzania kusaka Katiba
Mpya.
Rais Kikwete amesema hayo asubuhi ya
leo, Jumatano, Oktoba 22, 2014, wakati alipokutana na kuzungumza na
mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Jamhuri ya Watu wa China.
Mkutano
huo na mabalozi wa Afrika uliofanyika kwenye Nyumba ya Kufika Wageni ya
Serikali ya Diaoyutai mjini Beijing ambako Rais amefikia, ilikuwa
shughuli ya kwanza ya Rais Kikwete katika ziara yake rasmi ya Kiserikali
ya siku sita katika Jamhuri ya Watu wa China kwa mwaliko wa Rais Xi
Jinping. Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete aliwasili China
usiku wa jana, Jumanne, Oktoba 21, 2014.
Rais
Kikwete ametumia nafasi hiyo ya kukutana na mabalozi kuwaelezea hali ya
kisiasa, kiusalama na kiuchumi katika Afrika ikiwamo maendeleo ya
mchakato wa Tanzania kusaka Katiba Mpya.
Kuhusu
mchakato huo wa Katiba, Rais Kikwete amesema kuwa mchakato huo
unakwenda kama ilivyofikiriwa tokea mwanzo kuwa wakati ulikuwa umefika
wa Tanzania kuipitia upya Katiba ya sasa kwa nia ya kutunga Katiba Mpya
“ambayo itaiongoza nchi yetu kwa miaka mingine 50 kama ilivyofanya
Katiba ya sasa.”
Rais Kikwete amesema kuwa
mpaka sasa mchakato huo unakwenda vizuri baada ya kupitia hatua zote
ikiwamo ile ya Kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Kuundwa kwa
Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi, Kuundwa na Bunge Maalum ya Katiba
na hatimaye Bunge hilo kuipigia kura ya kuipitisha Katiba
Inayopendekezwa.
“Lilikobakia sasa ni Kura
ya Maoni ya Wananchi. Tunadhani kuwa kama itakwenda kama tulivyopanga,
Kura hiyo itapigwa wakati wowote mwezi Aprili mwakani. Bado tunaangalia
tarehe mwafaka kwa ajili ya shughuli hiyo muhimu,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katiba
hiyo ikipita, sote tutashangilia na kushereheka lakini matokeo ya Kura
ya Wananchi ikiwa tofauti basi tutaendelea kuongozwa na Katiba ya sasa
mpaka huko mbele wakati nchi yetu na wananchi watakapoamua tena kujaribu
kupata Katiba Mpya.”
Baadaye leo, Rais
Kikwete amekutana kwa mazungumzo na wakuu wa taasisi kubwa za fedha
katika China za Benki ya Maendeleo ya China ya China Development Bank
(CDB) na Mfuko wa Maendeleo wa China na Afrika wa China-Afrika
Development Fund (CADF) kuzungumzia miradi mbali mbali ya Tanzania .
Mazungumzo
hayo yalilenga kuona jinsi gani taasisi hizo zinavyoweza kuzisaidia
benki za Tanzania za Tanzania Investment Bank (TIB) na Tanzania
Agricultural Bank kuongeza mitaji yake ili kuweza kutoa mikopo zaidi ya
shughuli za maendeleo.
Aidha, Rais Kikwete
amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi ya China Poly
Group na China Poly Technologies ambayo imekuwa inatoa mikopo kwa
shughuli za maendeleo nchini katika sekta za umeme kupitia Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO na ujenzi wa nyumba kupitia Shirika la Taifa la
Nyumba (NHC).
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
22 Oktoba,2014
Ikulu – Dar es Salaam.
22 Oktoba,2014
No comments:
Post a Comment