Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura. Picha na Maktaba
Na Pamela Chilongola, Mwananchi
Dar es Salaam. Matukio ya ujambazi yanaendelea kutikisa Jiji la Dar es Salaam baada ya watu wanaoaminika kuwa majambazi kumjeruhi kwa kumpiga risasi mkazi wa Kibaha, Nyalinga Steven na kumpora kiasi cha Sh15 milioni jana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema jana kuwa Steven alipigwa risasi sehemu ya ubavuni katika eneo la Magomeni Mikumi.
Akisimulia tukio hilo, Camillius alisema Steven alikuwa akitoka Manzese na alipofika Magomeni Mikumi, alipigwa risasi na majambazi hao na kutokomea na kiasi hicho cha fedha.
Alisema tukio hilo lilitokea saa saba mchana, wakati Steven akiwa kwenye gari na kutakiwa kutoa fedha kabla ya kupigwa risasi iliyomjeruhi vibaya sehemu ya ubavu.
Kamanda Camillius alisema majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Wambura alisema maelezo ya awali ya Steven ni kwamba alikuwa na kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kununua samani eneo la Keko.
“Kila siku tunatoa maelezo kwa wananchi kuchukua tahadhari wanapokuwa wamebeba fedha nyingi, lakini inaonekana imekuwa ngumu,” alisema Wambura.
Aliwataka wananchi kutumia mitandao ya simu kufanya malipo au kuomba ulinzi wa polisi wanaposafirisha fedha nyingi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Hatari zingine ni kama za kujitakia, huwezi kuwa na kiasi kikubwa cha pesa kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila kuwa na ulinzi,” alisema Wambura.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment