Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 8 November 2013

SITA MBARONI KUCHARANGWA MAPANGA DK. MVUNGI

Dk. Sengondo Mvungi akiwa taabani hospitalini

Na Waandishi Wetu
5th November 2013
Jeshi  la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu sita wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la kumvamia na kumjeruhi kwa mapanga Mjumbe wa  Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 7:30 usiku eneo la Mpigi Magohe jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo watuhumiwa hao waliiba kompyuta mpakato (laptop) moja aina ya HP, simu mbili na fedha taslimu Sh. 1,000,000.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, alisema baada ya kupokea taarifa ya tukio hilo, polisi walianzisha msako kuanzia eneo la tukio na kwa kushirikiana na raia wema, waliwatilia shaka baadhi ya watu na kuwakamata.
Kova alisema watuhumiwa hao baada ya kukamatwa walipekuliwa na kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi puli 17 na gongo lita 15.
“Msako mkali unaendelea kwa kushirikiana na polisi wa Mkoa wa Pwani ili kuhakikisha kuwa yeyote aliyehusika na tukio hilo ni lazima akamatwe ili kukamilisha hatua za kiupelelezi na hatimaye kufikishwa mahakamani,” alisema Kova na kuongeza:
“Tulienda asubuhi  ya leo (jana) kumpa pole Dk. Mvungi na hali yake inatupa matumaini.”
Aidha, alikataa kuwataja watuhumiwa hao kwa maelezo kuwa ni sababu za kiupelelezi.
Wakati huo huo, hali ya Dk. Mvungi inaendelea vizuri ingawa bado hajapata fahamu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, hali ya Dk. Mvungi inaendelea kuimarika ukilinganisha na wakati alipofikishwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi) juzi.
Hata hivyo, Mbatia alisema hali ya Dk. Mvungi inatia matumaini baada ya kufanyiwa vipimo na kuanza kupatiwa matibabu kwenye taasisi hiyo.
Mbatia aliwashukuru watu wote wanaomwombea hasa viongozi wa dini na kuwaomba watu wote waendelee kumwombea ili afya yake izidi kuimarika haraka hasa ukizingatia kuwa Dk. Mvungi ni mtaalamu wa Katiba na ni mtu muhimu katika mchakato wa Katiba mpya.
Aidha Mbatia amewaasa wananchi wote wenye mapenzi mema ambao wanapenda kwenda kumuona Dk. Mvungi hospitalini hapo kuendelea kumwombea kwani kutokana na hali yake, watu hawajaruhusiwa kumtembelea.
Aliongeza kuwa misa ya kumuombea Dk. Mvungi inatarajiwa kufanyika leo jioni katika Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam.
Mbatia alimshukuru Rais Jakaya Kikwete; Mkuu wa Jeshi la Polisi,  Said Mwema na Wajumbe wa Tume ya Katiba wakiongozwa na Jaji Joseph Warioba ambao wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa.
Alisema anatumaini Jeshi la Polisi litatimiza wajibu wake kwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wa tukio hilo.
Dk. Mvungi jana alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Aliondolewa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili saa nne asubuhi na gari la kubebea wagonjwa  na kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa tano asubuhi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment