Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 17 November 2013

KWANI PROFESA KAPUYA NI MNYAMWEZI AU NI WALE WALIOTOKEA BURUNDI, CONGO NA RWANDA? NAITAFAKARI MAKALA HII HAPA...

Usanii wa Profesa Kapuya ni matusi kwa Wanyanyembe

Toleo la 316
18 Sep 2013

MANAMBA ni binadamu, nguvu kazi ya vijana waliokuwa wakitumikishwa kwenye kilimo cha mashamba makubwa ya mkonge na hasa katika mikoa ya Morogoro na Tanga, enzi za wakoloni wa Kijerumani na Mwingereza.
Manamba hao walitoka katika maeneo mbalimbali nchini, lakini wengi kulingana na historia ya manamba, walitoka mikoa ya magharibi mwa Tanzania - Tabora na Kigoma; mikoa ya kusini -  Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini - Iringa, Mbeya na Rukwa.
Ukiacha manamba wa mkonge, mradi mwingine mkubwa uliovuta manamba wengi kutoka maeneo hayo, ni ujenzi wa Reli ya Kati, inayoanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na matawi yake ya Kigoma na Mpanda.
Kwa wanaofahamu historia ya manamba waliotumiwa na wakoloni hao wa Kijerumani na Kiingereza kama nguvu kazi yao ya kulima mashamba ya mkonge na kuvuna, pamoja na kupasua miamba na kujenga reli kutoka Dar es Salaam hadi maeneo hayo, wanatambua kwamba manamba waliotokea njia ya Kigoma na Tabora, baadhi yao walitokea katika nchi za DR Congo, Burundi na Rwanda.
Kama ambavyo wakoloni hao wakati mwingine walilazimika kutumia nguvu kuwapata vijana wenye nguvu wa kwenda kulima mashamba yao ya mkonge, ndivyo pia wakoloni hao walivyotumia nguvu kuwasaka vijana wenye nguvu wa kwenda kushiriki ujenzi wa reli hiyo ya kati kwa ujira mdogo mno ikilinganishwa ukubwa wa kazi walizozifanya.
Baada ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, umanamba unaonekana kama udhalili. Siasa za wakati wa Uhuru zimeugeuza umanamba kama utumwa. Lakini, kusema ukweli, umanamba katika mkonge na ujenzi wa reli ya kati, enzi hizo, ilikuwa ni ufahari na ajira iliyowainua wengi kiuchumi.
Mwanzoni mwa ukoloni huo, vijana hao walilazimishwa kwenda kufanya kazi hizo. Lakini baadaye, baada ya jamii ya vijana kuona tofauti ya kiuchumi kati ya vijana waliotoka kwenye umanamba na waliobakia nyumbani na wazazi wao wakichunga ng’ombe na mifugo mingine, baadhi ya vijana walitoroka majumbani, bila kuwaaga wazazi wao na kwenda kushiriki kazi hizo.
Ilifika mahali ikawa ‘fasheni’ katika baadhi ya jamii zetu kwamba ili kijana aanze kujitegemea, kwa kuoa, kuanzisha mji wake na kuwa na familia yake, ili aaminiwe na jamii anaweza kujitegemea na kuitunza familia, kipimo cha uwezo huo kilikuwa kazi ya manamba. Kijana alilazimika kwanza kufanya kazi za manamba ili apate fedha za kuanzia maisha na kununulia mifugo!
Ujenzi wa reli ya kati na kilimo cha mkonge, ndizo ajira kuu za uhakika zilizokuwapo enzi hizo kwa kijana wa Tanganyika ambaye elimu kwake ilikuwa kitu cha anasa kutokana na sera za wakoloni wote wawili hao. Enzi hizo, kazi za manamba hazikuwa kazi za kitumwa kama ilivyokuja kuelezwa baadaye na wanasiasa wetu baada ya Uhuru, bali ndizo kazi za mishahara zilizokuwepo!
Lakini kikubwa zaidi ya ajira, kazi za manamba ndizo zilikuwa msingi wa kwanza uliowaunganisha na kuwaweka pamoja vijana wa Kitanganyika katika kambi. Vijana wa Kitanganyika kutoka makabila tofauti nchini, walikusanywa, kuchanganyika na kuishi pamoja kama ndugu kwenye kambi za mkonge na ujenzi wa reli, wakichukua likizo kwenda makwao na kurejea tena kwenye makambi hayo.
Ndiyo maana leo, ni rahisi kukuta watu wa makabila mbalimbali ya Tanzania, na hasa ya Wangoni wa Songea, Waha wa Kigoma, Wanyamwezi wa Tabora, Wahehe wa Iringa, Warundi na Wanyarwanda walioingia manamba kupitia mikoa ya Kigoma na Kagera, wakiwa na kizazi chao katika maeneo kadhaa ya mikoa ya Morogoro na Tanga kulikokuwa kukilimwa mkonge kwa wingi.
Lakini pia kizazi cha manamba hao kinaonekana leo katika miji mikubwa na midogo ambako njia ya reli ya kati inapita. Kuna vijana na watu wazima walioamua kutorudi makwao na kuhamia maeneo hayo moja kwa moja. Hao kwetu nyumbani tukiwaita ‘Abhalobhezi’ (Walowezi).
Kijiji cha Kaliua, kilichoko wilayani Urambo, Tabora, kilikuwa ni kijiji kidogo tu, wakati Profesa Juma Athuman Kapuya anazaliwa mwaka 1945. Kwa asili, Kaliua ni kijiji cha Wanyamwezi, kabila kubwa linalopatikana katika Mkoa wa Tabora.
Kwa sasa, Kaliua ni mji mdogo katika wilaya hiyo ya Urambo, na una mwingiliano wa watu kutoka makabila mbalimbali ya Tanzania, waliohamia hapo kutokana na shughuli za kiuchumi, wakiwemo manamba walowezi waliokuwa wakifanyakazi katika mashamba ya mpunga na tumbaku pamoja na masalia ya manamba waliokuwa wakijenga reli ya kati inayopita katikati ya mji huo mdogo.
Kiutawala, eneo la mji wa Kaliua kwa sasa liko Mkoa wa Katavi. Kwa hiyo, Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya, si Mnyamwezi wa Tabora tena, bali ni Mnyamwezi wa Katavi. Ameungana na kabila la ndugu zao Wapimbwe, kabila la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kaliua kuna idadi kubwa ya Waha kutoka Kigoma. Kwa wasiofahamu tu, Muha wa Kigoma ni ama atakuwa Muha Mhutu au Muha Mtutsi. Ni kama ilivyo kwa Mrundi au Mnyarwanda. Kila Mnyarwanda au Mrundi ni ama atakuwa Mhutu au Mtutsi! Hao wapo hata Kagera. Wapo Wahaya wenye asili ya Ututsi, Uhutu na au Unyankole.
Ningekuwa na uwezo wa kifedha wa kutafiti kizazi cha Profesa Kapuya, Mnyamwezi wa Kaliua, bila shaka yoyote, utafiti wangu ungenifikisha kwenye ukweli halisi kwamba kizazi cha Profesa Kapuya kina mizizi Mkoa wa Kigoma au ng’ambo, na kwa hiyo Profesa Kapuya mwenyewe ana damu ya ama Kihutu au Kitutsi!
Nafikia hitimisho hilo la utafiti wangu huo kutokana na imani kwamba mtu akishaathiriwa na umanamba, akaathiriwa na utumwa, inakuwa vigumu kwake kusimama peke yake. Hata ukimjazia vyakula vya aina zote ndani, atakwenda kuomba tu chakula kama hicho hicho alichonacho ndani kwake, kwa jirani.
Tukio la wiki iliyopita mjini Tabora, limenikumbusha umanamba wetu, limedhihirisha taathira ya umanamba na utumwa kwa baadhi ya jamii zetu. Kwamba kwa kuwa kiutawala sasa Profesa Kapuya hawezi kuwa sehemu ya Wanyamwezi wa Tabora, na kwa kuwa Wanyamwezi wa sasa, baada ya kizazi cha Mirambo na Isike kutoweka, hawawezi kujisimamia na kujitawala wenyewe, mwanasiasa huyo na msomi huyo aliratibu na kusimamia hafla ya kusimikwa kwa Chifu mpya na Mlezi mpya wa Wanyanyembe wote, Edward Lowassa.
Kwamba kwa hekima, busara na fikra za Profesa Kapuya, Wanyamwezi wote kwa ujumla wao, wakiwemo kina Profesa Ibrahimu Lipumba, Aden Lage, Samuel Sitta, Said Mkumba, Rostam Aziz na wengineo, hawana sifa ya kuwa Machifu na Walezi bora wa Wanyanyembe, bali wanahitaji Laigwanan wa Kimaasai kuwaongoza, Edward Lowassa.
Kumbe kwa Mnyamwezi, umanamba haujaisha. Mnyamwezi bado ni mtu wa kubebeshwa mzigo mzito, na si yeye kubebesha mtu! Kwa hakika kabisa, hili la profesa Kapuya kuwachagulia kiongozi Wanyanyembe, ni usanii wa kisiasa, ni aibu na fedheha kubwa kwa yeyote anayejiita Mnyamwezi!
Chanzo: www.raiamwema.co.tz

No comments:

Post a Comment