Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 29 November 2013

NYAYO ZA CHIFU MKWAWA (7)

Kamanda wa Jeshi la Wajerumani, Emil von Zelewiski

Na Daniel Mbega
Ndugu zangu,
Wengi wanaikumbuka Vita ya Maji Maji iliyodumu kwa miaka miwili baina ya Watanganyika na Wajerumani kati ya mwaka 1905 hadi 1907. Kinachofanya waendelee kuikumbuka ni mbinu zilizotumiwa na Mtawala wa Wangindo kule Kilwa, Kinjekitile Ngwale huko kwenye Bonde la Ngalambe alipowapaka na kuwanywesha dawa wapiganaji wake na kuwasadikisha kwamba risasi za Wajerumani zingegeuka kuwa maji.
Utaalamu huo ulisambaa karibu sehemu kubwa ya Kusini mwa Tanzania pamoja na Nyanda za Juu ambapo uliwaongezea ujasiri mkubwa wapiganaji hao waliokuwa wakiitetea ardhi yao isitawaliwe na Wazungu.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba, Chifu Mkwawa na watemi wengine wengi wa wakati huo, pamoja na kuwa na mbinu za kupigana vita, walitumia jadi, kwa maana ya dawa za kienyeji, katika kupanga na kupambana na maadui zao.
Kama ambavyo tunaelezwa katika Vitabu Vitakatifu kwamba, Wafalme wa Israel – tangu enzi za Nabii Musa – walikuwa wanawauliza kwanza Makuhani kabla ya kupanga vita, ndivyo watawala wetu wa Kiafrika walivyofanya nao kwa kuomba miungu yao iwasaidie, hasa wakati huo kwa vile dini ya Kikristo ilikuwa haijaenea.
Kwa kutambua mafanikio ambayo alikuwa ameyapata katika vita dhidi ya Mwamubambe Mwalunyungu na wafuasi wake, Chifu Mkwawa alimtumia pia mganga wa jadi Ngondo Kimamula Mbugi katika timu yake ya kumtabiria nini ambacho kingetokea, kama anavyoeleza kitukuu wa mganga huyo, Robert Gabriel Meza Mwaigoga.
Mwaigoga anaeleza kwamba, wapiganaji wa Chifu Mkwawa walikunywa dawa Lundamatwe, mahali pale pale waliponywea kabla ya kupambana na Mwambambe, katika eneo linaloelekea Mto Ruaha, takriban kilometa tisa hivi kutoka Lugalo ambako ndiko walikotakiwa kupambana na Wajerumani.
Chifu Mkwawa alikuwa na bunduki moja aliyopewa na Waarabu wakati ule wa Biashara ya Watumwa, lakini wapiganaji wake wote walikuwa na silaha za jadi kama mikuki, kombeo, pinde na mishale na mapanga.
Inaelezwa kwamba, akiwa tayari amepewa siri zote za lilivyokuwa jeshi la Wajerumani chini ya Emil von Zelewiski na silaha walizokuwa nazo, Chifu Mkwawa aliwaeleza wapiganaji wake kwamba, watajipanga vyema katika kingo za bonde ambalo Wajerumani wangepita, lakini hakuna ambaye alitakiwa kushambulia mpaka yeye atakapofyatua risasi ya kuashiria mapambano.
Ngondo Kimamula Mbugi alikuwa amewapaka dawa ambazo aliwasadikisha kwamba, hakuna Mjerumani ambaye angeweza kuwaona kabla ya mapambano, na wakati huo Wahehe wangekuwa tayari wamewavamia na kuwashambulia, hivyo hata kama wangefyatua risasi zao zingetoka maji.
Sehemu waliyopita Wajerumani pale Lugalo ilikuwa nyembamba kama mkia, kukiwa na kingo kila upande, hivyo kuwawia vigumu kuweza kufanya mashambulizi ya aina yoyote. Zaidi ya hayo, msitu uliokuwepo ulitoa hifadhi nzuri kwa wapiganaji wa Chifu Mkwawa.
Kosa alilokuwa amelifanya Von Zelewiski, pamoja na uzoefu mkubwa wa vita aliokuwa nao, ni kujiamini kupita kiasi na kutotuma wapelelezi wakachunguze njia na uimara wa jeshi la Mkwawa. Aliamini kwamba, jeshi hilo lilikuwa kama yale mengine aliyoyapiga sehemu nyingine na kwamba huenda Chifu Mkwawa hakuwa na nguvu kama za Abushiri wa kule Pangani aliyepigwa mwaka mmoja nyuma.
Inasimuliwa kwamba, malengo ya Von Zelewiski yalikuwa kwenda kuivamia ngome ya Chifu Mkwawa kule Kalenga, lakini hakujua kama tayari Wahehe walikuwa wamejipanga njiani kukifanya kile ambacho hakuna aliyekitarajia.
Ili kuwazuia Wajerumani wasithubutu kufanya shambulio lolote, Wahehe ambao tayari walikuwa wanafahamu uwezo wa jeshi hilo la maadui pamoja na kulifahamu eneo lote na kupanga ni mahali gani waanze kushambulia, walipanga kuwazuia wasitumie mtindo wao wa nusu duara kushambulia. Kwa kuwa walikuwa wamepata taarifa za Wajerumani walivyopigana huko Pwani, Wahehe walikuwa wamejiandaa kuhakikisha wanakabiliana vilivyo na askari hao.

Tutaendelea…

No comments:

Post a Comment