Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 28 November 2013

SIYO MZEE MTEI, HATA MWALIMU NYERERE ‘ALIICHAGULIA’ CCM VIONGOZI



Na Daniel Mbega

NIMEKUWA nikifuatilia mijadala inayoendelea ya siasa ndani ya Chadema, lakini kubwa zaidi lililonifanya niandike waraka huu mfupi ni madai kwamba muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei, anawachagulia viongozi.
Madai mengi dhidi ya Mtei yametolewa hivi karibuni baada ya Kamati Kuu kuwavua uongozi Zitto Kabwe, Samson Mwigamba na Dk. Kitila Mkumbo, huku Makamu Mwenyekiti Bara, Said Arfi, akijiuzulu mwenyewe nafasi hiyo kwa maelezo kwamba muasisi huyo anawachagulia viongozi.
Hii yote ilitokana na kauli ya Mzee Mtei kwamba kuna baadhi ya watu wanakesha usiku na mchana kuhakikisha wanafanya njama za kukidhoofisha na hata kukipoteza kabisa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Mtei alisema kuna baadhi ya watu kutoka Chama Tawala cha CCM wanahakikisha wanatengeneza mifarakano kila kukicha ili kukivuruga Chadema hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa kauli kuwa huenda CCM ikang’oka mwaka 2015.
Kuhusu kuvuliwa uongozi kwa Zitto, Dk. Kitila na Mwigamba, Mtei alisema anaunga mkono uamuzi huo wa Kamati Kuu. Akamtaka makamu mwenyekiti aliyejiuzulu naye ajitazame upya na kujisahihisha badala ya kulalamika kila siku.
 “Aache kulalamika kwa sababu, wakati alipochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti mimi nilisimamia uchaguzi. Kama alikuwa na ndoto kwamba siku moja atakuwa mwenyekiti wa Chadema taifa alipaswa kujichunguza kwanza,” alisema. "Naunga mkono uamuzi wote wa Kamati Kuu, kuwasimamisha na kuwavua uongozi Naibu Katibu Mkuu wetu Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo."
Lakini wanaomtuhumu Mtei kuingilia uongozi wamekwenda mbali sana na kusema huenda mzee huyo anaona asipofanya hivyo hatakuwa na mamlaka tena kwenye chama, hivyo anastahili kukitazama kwa karibu na kuangalia nani anaweza ‘kumsikiliza’.
Wanamtuhumu kwamba anawakumbatia mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Wilbrod Slaa na Mbunge wa Arusha Mjini, kijana wake Godbless Lema, kiasi kwamba alishindwa hata kumkanya wakati zilipotokea fujo hivi karibuni mjini humo.
Wengine wameandika katika mitandao ya kijamii wakisema: “Mtei alikataa kushiriki kupigania uhuru, akakataa kujitolea kuitumikia nchi katika kipindi kigumu na sasa anataka kuivuruga nchi kwa kupitia Chadema!”
Hili linaweza kuwa na ukweli ndani yake, lakini mbona hata Mwalimu Nyerere naye alipoona mambo yanakwenda kombo ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) aliingilia kati?
Nakumbuka mwaka 1994 alipoingilia kati na kuizima hoja ya Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, akawatuhumu Waziri Mkuu wa wakati huo John Samuel Malecela kwamba ni mhuni na Katibu Mkuu wa CCM Horace Kolimba kwamba ni mlevi.
Hata mwaka 1995 wakati wa kura za maoni kutafuta mgombea urais kupitia CCM, Mwalimu alisimama kidete kuhakikisha ‘Boyz II Men’ hawapiti na akamuuliza mmojawao kwamba fedha amezitoa wapi.
Mwalimu ndiye aliyesema mgombea wa CCM, Ben Mkapa anauzika, na akafanya juhudi za kumnadi kwa Watanzania kiasi kwamba ghafla akawa maarufu.
Na je, wanaCCM si wanakumbuka jinsi Mwalimu alivyokwenda ghafla Dodoma mwaka 1997 na kuzima mapinduzi yaliyokuwa yamuondoe Malecela kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara?
Sasa binafsi sioni ajabu ikiwa Mtei, kwa kutumia hekima na busara, anaona wapo wanaoweza kukisimamisha chama. Najua Ukubwa wa umri ni ujana wa umahiri, hivyo yawezekana Mtei anajua anachokifanya.
Kama kuna hoja nyingine kama za ukabila, ukanda na udini, hizi zinapaswa kujadiliwa na ingawa ‘Mkubwa hakanyiki’ basi anaweza kushauriwa ili kukijenga chama chao.


No comments:

Post a Comment