Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 29 November 2013

MCHUNGAJI MSIGWA, UKITAKA KURUKA SHARTI UAGANE NA NYONGA!



Na Daniel Mbega

NIMEKUWA nikifuatilia minyukano ya kauli inayoendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) tangu kuibuliwa kwa kinachoitwa ‘Ripoti ya Siri dhidi ya Zitto Kabwe’ mpaka ‘Waraka wa Uhaini’ uliomuondoa madarakani Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini.
Wengi wanazungumza – wa ndani na nje ya Chadema – kuhusu uamuzi uliochukuliwa na Kamati Kuu ya Chadema Novemba 22, 2013 wa kumvua nyadhifa zote Zitto Kabwe kwa waraka wa ‘kihaini’ adhabu iliyowapata pia Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba.
Hata hivyo, kati ya wote walioibuka kuzungumzia yanayoendelea ndani ya chama hicho, nimeguswa zaidi ya Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Nimesoma mabandiko yake aliyoyatoa kwenye kurasa za mitandao ya jamii, hasa facebook, na nimemsikia akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio.
Mchungaji Msigwa ametamka bayana kuunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho, ambayo yeye ni mjumbe, jambo ambalo siyo kosa kisheria kwa sababu anayo haki ya kutoa mawazo.
Mbunge huyo ameuvamia ugomvi wa Zitto Kabwe na viongozi wa juu wa chama hicho bila kuelewa. Amempinga Zitto kwa kauli zake mbalimbali alizozitoa baada ya kuvuliwa uongozi.
Mchungaji Msigwa amesema kinachofanywa na Zitto Kabwe na wenzake ni kutafuta huruma ya watu wengine kutokana na adhabu waliyopewa.
Nimesema Mchungaji Msigwa ameuvamia ugomvi huo kwa sababu moja – kwamba haelewi ulikoanzia, unakoelekea na nini hatma ya yote. Sijui aliingia lini Chadema, lakini najua aliingia Bungeni mwaka 2010 kwa kutumia karata ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kujivuruga wenyewe kwenye kura za maoni kwa Halmashauri Kuu kumpitisha Monica Mbega badala ya Fredrick Mwakalebela aliyeshinda kwa kura nyingi.
Haelewi kwamba, hata michezo michafu iliyofanywa na wanaCCM wa Iringa waliokasirishwa na uamuzi wa NEC ilikuwa ni katika kupiga kura ya kisasi na siyo kwamba yeye alikuwa anakubalika kiasi hicho. Ndiyo maana wale waliopigania aingie Bungeni walikuwa tayari kufanya lolote kuhakikisha hawamchagui mtu wa kuchaguliwa.
Mchungaji Msigwa anapaswa kutambua kwamba mchezo wa siasa ni kama ndondi, kila mtu anajitahidi kumwangusha mpinzani wake.
Zitto Kabwe amekuwepo muda mrefu kwenye harakati za siasa – kuanzia Chuo Kikuu ambako yeye na wenzake walikuwa katikati ya migomo ya wanafunzi kwa lengo la kutetea maslahi yao. Lakini pia amekuwepo Chadema kitambo, pengine wakati huo Mchungaji Msigwa akiwa hajawaza kuingia kwenye siasa za majukwaani.
Mchungaji Msigwa anapaswa kutambua kwamba, kinachoendelea ndani ya Chadema siyo cha kufurahia. Mvutano wa Zitto na uongozi umekuwepo kitambo na ndiyo maana wakati alipotaka kupambana na Freeman Mbowe kwenye nafasi ya uenyekiti mwaka 2009, wengi wakapiga kelele. Hivyo, vita hivi vya sasa ni marudio tu wakati Chadema inapoelekea kufanya uchaguzi wake mkuu mwaka 2014.
Mbunge huyo wa Iringa Mjini anapaswa kujikumbusha maneno ya Kikongo yasemayo: “Etutana Yango na Yango!” yaani “Wanajuana Wenyewe kwa Wenyewe!”
Ukitaka kuruka shuruti uagane na nyonga! Sidhani kama Mchungaji Msigwa analitambua hili kiasi cha kuingia kwa miguu miwili kumshambulia Zitto Kabwe, ambaye kwa hakika ni miongoni mwa makamanda wa Chadema ‘waliomsaidia’ kujenga imani kwa wakazi wa Iringa Mjini kwa kuhudhuria mikutano kadhaa iliyojaza watu wengi. Naamini kabisa kwamba, kama leo Mchungaji Msigwa ataita mkutano wa hadhara – achilia mbali Mwembetogwa na Kihesa – hataweza kujaza umati kama anaojaza wakija akina Zitto.
Pamoja na ukweli kwamba anayo haki ya Kikatiba ya kutoa maoni yake, lakini lazima atambue kwamba sasa amejiingiza katika vita ambavyo siyo tu vitamharibia yeye ndani ya Chama, bali hata katika Jimbo lake.
Tayari watu wameanza kusema kwamba anamshambulia Zitto ili apate nafasi zaidi ndani ya chama. Maneno haya hayana heri – hata kama kweli atapata nafasi ya juu – kwani itakavyokuwa watu watasema naye anahusika kuondolewa kwa Zitto.
Si tayari watu wamezusha kwamba Mchungaji Msigwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara (nafasi ya Zitto)? Je, anadhani hiyo ni sifa ama kumdidimiza?
Ushauri wangu wa Mchungaji Msigwa ni kwamba, kipindi kilichopo siyo cha ‘kununua ugomvi’ bali cha kuangalia kwamba nyumba aliyopo ni ya vioo, hivyo hapaswi kurusha mawe kwa wengine. Maana yangu hapa ni kwamba, hakuna mpinzani ambaye aliwahi kukaa katika Jimbo la Iringa Mjini kwa vipindi viwili. Kama anabisha amuulize Mfwalamagoha Wulanziwang’ombe Kibaasa aliyeingia kwa mhemuko wa NCCR-Mageuzi chini ya Mrema 1995 lakini akashindwa kurejea 2000 kutokana na vurugu-mechi zilizotokea na kumfanya Mrema akimbilie TLP.
Ahadi nyingi alizozitoa Mchungaji Msigwa hazijatekelezwa na ingawa mwenyewe amesema asipotekeleza basi asichaguliwe, lakini anaweza kujikuta hatimizi ahadi hizo kwa kuzama kwenye ugomvi usio wake. Nasema siyo wake kwa sababu anapaswa kuchunguza kwa undani hayo yote yanatokea wapi!
Ahadi yake ya maji bado haijatekelezwa. Mfano hai ni pale Nduli kuliko na uwanja wa ndege, ambako wananchi wanalia hawana maji na wamekuwa wakidanganywa kila siku.
Haya ni mawazo yangu tu.


No comments:

Post a Comment