Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 19 November 2013

NYAYO ZA CHIFU MKWAWA (4)

Mti wenye miaka zaidi ya 100 katika eneo la Lundamatwe ambapo mganga wa jadi Ngondo Kimamula aliwatengenezea dawa wapiganaji wa Mkwawa kabla ya kumpiga Mwamubambe Mwalunyungu.
Eneo ambalo inaelezwa kwamba ndiko vichwa vta wapiganaji wa Mwambambe vililundikwa baada ya kuuawa na wapiganaji wa Chifu Mkwawa.
Makaburi ya ukoo wa Ngondo Kimamula Mbugi katika eneo la Lundamatwe.

Na Daniel Mbega

Ndugu zangu,
Tunaendelea na simulizi ya historia ya kufuatilia ‘Nyayo za Chifu Mkwawa’. Tumeona jinsi ambavyo baada ya kifo cha Chifu Munyigumba mkwewe Mwambambe Mwalunyungu alivyomuua baba yake mdogo Chifu Mkwawa, Mtwa Mhalwike na yeye akajitangazia mtawala wa himaya ya Wahehe, ingawa wakati huo walikuwa bado hawajaanza kuitwa ‘Wahehe’.
Tumeona pia namna wazee walivyoamua kumkimbiza Chifu Mkwawa na kumficha Dodoma (Idodomhya) kuepuka asije akauawa na Mwambambe.
Kwa hiyo basi, baada ya Chifu Mkwawa kukimbizwa, Wahehe hawakufurahishwa na utawala wa Mwambambe ambaye mpaka sasa anachukuliwa kama adui mkubwa zaidi katika historia ya kabila hilo kuliko hata Wajerumani. Hivyo, wakapanga mbinu za siri kumrejesha Mtwa Mkwawa kutoka uhamishoni.
Mtwa Mkwawa, wakati huo akiwa amejifunza mbinu za juu za kivita kwa msaada wa Chifu wa Wagogo, akaamua kurejea na kuunda jeshi lake ili kupambana na Mwambambe katika harakati za kuurejesha utawala huo.
Hata hivyo, katika mapigano hayo, wapiganaji wengi wa Mtwa Mkwawa waliuawa na Mwambambe, mtu ambaye anadaiwa kuwa alikuwa akitumia zaidi mitishamba kushinda vita nyingi, dawa ambazo inaelezwa kwamba ndizo alizokuwa anatumia ndizo zilizokuwa zikitumiwa na Mtwa Munyigumba na Mwambambe mwenyewe ndiye aliyekuwa akielekezwa kuzitafuta porini.
Kutokana na wapiganaji wengi kuuawa na Mwamubambe, wapiganaji wengine walikuwa wakilia na kupiga kelele; “Hee Hee Hee! Mtwa tuisila!” wakimaanisha; “Hee Hee Hee! Mtwa tunakwisha!” Hapa hasa ndipo lilipoanza jina la kabila la Wahehe kutokana na kelele walizokuwa wakizipiga.
“Wafuasi wake walikuwa wanakufa sana. Siku moja Mkwawa akajiwa kwenye ndoto na baba yake Munyigumba ambaye alimwambia kwamba hilo jitu hawataliweza. Lilikuwa likichomwa mikuki linachomoa na kuwarushia wao na kuwaua,” anasema Malugala Mwamuyinga.
Inaelezwa kwamba, Munyigumba alipomtokea Mkwawa kwenye ndoto akamwambia, roho ya Mwamubambe iko kwenye kidole au kwenye kisigino. Hata wakifanya namna gani hawawezi kumuua. Hivyo akamtaka amtafute Mkimayena Mwakinyaga amwambie akamchome Mwambambe kwenye kisigino au kidole.

Lundamatwe
Mwambambe alikuwa na jeshi kubwa na wafuasi wengi wenye uwezo wa vita, Mtwa Mkwawa akalazimika kujipanga upya ili kuwapiga na kuyarejesha maeneo yote yaliyokuwa yametwaliwa na Mwambambe.
Mapambano makali kabisa ya Mkwawa na wafuasi ya Mwambambe yaliianzia eneo ambalo leo hii linafahamika kama Lundamatwe (Lundika Vichwa), lakini yapata kilometa mbili kutoka Barabara Kuu ya Tanzam upande wa kusini.
Hapa palikuwa nyumbani kwa mganga Ngondo Kimamula Mbugi, pembezoni mwa Mto Ruaha. Inaelezwa kwamba, mganga huyo aliamua kuchukua jukumu la kuwaandaa wapiganaji wa Mkwawa kukabiliana na maadui zake.
Wapiganaji wa Mkwawa baada ya kuganguliwa wakaondoka kupambana na Mwambambe na wafuasi wake ambapo waliwapiga na kuwaua zaidi ya wapiganaji 1,000.
Mwambambe alipona mambo yamemzidia akatimua mbio, lakini wapoganaji wa Mkwawa wakaanza kumfukuza.
Kwa vile Mkwawa alikuwa ameelekezwa na baba yake ndotoni kuhusiana na Mwambambe, akaamua kumtuma Mukimayena Mwakinyaga, ambaye alikuwa mganga wa kienyeji, ili akamuue.
Mwakinyaga akaenda na kumkuta Mwambambe anakunywa pombe. Mbele ya umati wa watu, akamchoma mkuki kwenye kidole. Mwambambe akadondoka chini na kuanza kutapatapa bila kukata roho.
“Mwamubambe akamuuliza Mwakinyaga, ‘Umenifanya nini?’ Mwakinyaga akasema, ‘Aah ni mikuki tu’. Basi alipoona mambo yamekuwa magumu, akamwambia; ‘Kaniitie Mkwawa aje’. Mkwawa alipofika Mwambambe akamwambia; ‘Wakorofi kama mimi wapo wengi ndani ya utawala wako, kwa hiyo sasa ukazane’.
“Kwenye ndoto, baba yake alikuwa amemwambia Mkwawa kwamba akishafika aukite mkuki wake chini. Basi Mkwawa akaukita mkuki chini. Ndipo Mwambambe akakata roho,” anaeleza Mwamuyinga.
Mwamuyinga anasema kwamba, kwa vile Mwambambe alikuwa amewatesa na kuwaua Wahehe wengi, baada ya kufa ikabidi, kwa hasira, wananchi wale wamkatekate vipande vipande na kuila nyama yake ili lisiwepo kabisa kumbukumbu lake.
Baada ya hapo Mtwa Mkwawa akaendesha mapambano ya kuyakomboa maeneo yote yaliyokuwa chini ya utawala wa Munyigumba, kampeni ambayo iliendelea moja baada ya nyingine kwa mafanikio makubwa kuliko hata awali.

Tutaendelea…

No comments:

Post a Comment