Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 28 November 2013

NYAYO ZA CHIFU MKWAWA (6)

Na Daniel Mbega

Ndugu zangu,
Kwanza kabisa niwieni radhi kwa kushindwa kuendelea na simulizi yetu ya kufutilia Nyayo za Chifu Mkwawa kwa siku kadhaa. Hii imetokana na sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wangu.
Hata hivyo, karibuni tuendelee na simulizi yetu.
Tuliona jinsi Chifu Mkwawa alivyoirejesha himaya mikononi mwake kutoka kwa Mwambambe Mwalunyungu. Kadhalika tuliona Wajerumani walivyoingia Tanganyika na kuanza kuwashambulia watawala wa jadi kama Abushiri wa Pangani na sasa walikuwa wanaelekea Bara, wakipanga kwenda kupambana na Chifu Mkwawa wa Uhehe.
Vikosi hivyo, chini ya von Zelewiski, viliondoka Kilwa Julai 22, 1891 vikipitia himaya ya Ngoni Mafiti kuelekea Kisaki hadi Myombo karibu na Kilosa, ambapo viliwasili Lugalo Agosti 16, 1891. Huko njiani vikosi hivyo vilikuwa vimeteketeza vijiji kadhaa na havikukutana na upinzani mkali. Walikuwa wamewaona Wahehe wenye silaha njiani, lakini walikimbia baada ya kuwafyatulia risasi. Hali hiyo inaonekana ndiyo iliyompa ujasiri von Zelewiski wa kusonga mbele akiamini kwamba Wahehe wangelazimishwa kusalimu amri.    
Jeshi la Mkwawa
Mtwa Mpangile, mdogo wake Chifu Mkwawa, ndiye aliyekuwa kamanda wa jeshi la Wahehe. Ndiye aliyeongoza jeshi hilo katika vita vya Lugalo. Kama ilivyokuwa kwa wapiganaji wote wa Kihehe, Mpangile alikuwa na uzoefu mkubwa wa vita ingawa ni vite dhidi ya makabila mengine, lakini siyo kwa jeshi imara lenye mbinu kama la Wazungu.
Tofauti na makabila mengine ya Kiafrika ambayo machifu wao ndio waliokuwa mstari wa mbele, Wahehe walikuwa na mbinu kama za Wazungu kwa kumwacha chifu wao nyuma akiamuru namna ya kushambulia.
Jeshi la Wahehe kwenye vita vya Lugalo lilikuwa na wapiganaji 3,000. Ndilo lililokuwa imara zaidi kulinganisha na makabila mengine yote yaliyolizunguka.
Ushindi dhidi ya makabila mengine ya jirani ulikuwa umewapa ujasiri mkubwa na uzoefu wa vita na kwa hakika walikuwa wamejitolea kuhakikisha wanapambana kufa au kupona kuhakikisha wanailinda nchi yao dhidi ya wavamizi wa kigeni.
Wengi kati ya wapiganaji wa Kihehe walikuwa na mikuki na ngao zilizotengenezwa kwa ngozi kama zile zilizokuwa zikitumiwa na Wazulu. Wengine walikuwa na mashoka.
Chifu Mkwawa alikuwa anafahamu kwamba majeshi ya Wajerumani yalikuwa yanakuja kwenye himaya yake. Taarifa zilikuwa zimemfikia mapema mno na kuifahamu mikakati yao yote. Vijana wake mashujaa waliviona vikosi vya Wajerumani wakati vikikaribia Uhehe na kupeleka taarifa za uwezo wa jeshi hilo la Wazungu, hivyo alikuwa amejiandaa kuwakabili.

Tutaendelea…

No comments:

Post a Comment