Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 20 November 2013

NYAYO ZA CHIFU MKWAWA (5)

Askari wa Kijerumani

Na Daniel Mbega

Ndugu zangu,
Tunaendelea na simulizi ya historia ya kufuatilia ‘Nyayo za Chifu Mkwawa’. Baada ya kufanikiwa kuurejesha utawala kwenye himaya yake mwaka 1890 kufuatia kumtwanga Mwambambe Mwalunyungu aliyekuwa na walugaluga kutoka Tabora, Chifu Mkwawa aliendelea kuuimarisha utawala huo kwa ujasiri mkubwa akiwazuia Wamasai wasiende kusini pamoja na kupambana pia na biashara ya utumwa iliyokuwa ikiendeshwa na Waarabu.
Wakati huo alikuwa ameimarisha urafiki wake wa kibiashara na Waarabu katika Pwani ya Tanganyika, ambao walimpatia bunduki pekee aliyokuwa akiitumia mwenyewe.
Hata hivyo, mapambano mengine makubwa zaidi yalikuwa yanajongea ambayo yangehitaji ujasiri mkubwa kuyakabili.
Kufikia mwaka 1890 majeshi ya Ujerumani, maarufu kama Wissmanntruppe (Kikosi cha Wissmann), yalikuwa yamefanikiwa kuyashinda majeshi ya upinzani ya Abushiri na kuitwaa Pwani yote ya Tanganyika (wakati huo ikijulikana kama German East Africa). Mnamo mwezi Mei 1891 Kikosi cha Wissmann kilibadili jina na kuitwa Kaiserliche Schutztruppe na von Wissmann akastaafu kwenye jeshi hilo la Afrika akimwachia Luteni Emil von Zelewski kuliongoza.
Njia zote za misafara ya kibiashara ya pwani hazikuwa salama kutokana na kushambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa makabila ya maeneo hayo, hususan upande wa kusini wa koloni lao kutoka kwa makabila mashuhuri kwa vita kama Wangoni, Wagogo na Wahehe ambao walipora misafara hiyo.
Wakati huo Wahehe walikuwa wameimarisha himaya yao kutoka Iringa ilikokuwa ngome ya Chifu Mkwawa kuelekea pwani ambako Wajerumani walikuwa wameishikilia. Kutoka kwenye kabila lililotawanyika kwenye miaka ya 1850 chini ya Chifu Munyigumba, sasa Wahehe walikuwa himaya kubwa chini ya Mkwawa.
Wakati wa kiangazi cha mwaka 1891 von Zelewski aliamua kupambana na hali hiyo kwa kutumia nguvu ya jeshi kuanzia Kilwa kuelekea Bara.
Awali Emil von Zelewski alikuwa mwanajeshi wa Kikosi cha 99 cha Jeshi la Nchi Kavu cha Rhineland kabla ya kuhamishiwa kwenye Kampuni ya German East Africa mwaka 1886 na hatimaye kwenye kikosi cha Wissmanntruppe mwaka 1889. Alikuwa amefanikiwa kuongoza kikosi cha  Wissmanntruppe yeye binafsi na kwa kushirikiana na vikosi vya Wissmann katika matukio mengi wakati wakipambana na Abushiri kule Pangani. Alikuwa na uzoefu wa kutosha katika vita na kiongozi makini.

Muundo wa jeshi lake
Jeshi la von Zelewski lilikuwa na gadi nne ambazo kila moja ilikuwa na askari 90 walioongozwa na maofisa wa Kijerumani na NCO mmoja. Gadi moja iligeuka na kurudi na kuacha gadi tatu kukabiliana na Wahehe. Gadi namba 5 iliongozwa na Luteni von Zitzewitz akisaidiwa na von Tiedewitz, ambapo ilikuwa na askari kutoka Sudan, Gadi namba 6 iliongozwa na Luteni Tettenborn aliyesaidiwa na Feldwebel Kay na ilikuwa na Wasudani pia, wakati Gadi namba 7 iliongozwa na Luteni von Pirch akisaidiwa na Schmidt ambayo iliundwa na askari wa Kizulu.
Pia kulikuwa na kikosi cha bunduki ambacho kiliongozwa na von Heydebreck akisaidiwa na Thiedemann, Herrich na Wutzer wakati ambapo kitengo cha tiba kiliongozwa na Dk. Buschow na Hemprich.
Jeshi la von Zelewiski lililokuwa na maofisa 17 wa Kijerumani, lilikuwa na vyakula vingi pamoja na ng’ombe wao. Kulikuwa na Wapagazi 170 wa Kiafrika ambao kazi yao ilikuwa ni kubeba mizigo, punda 27, ng’ombe 20 na kondoo na mbuzi 60.
Nguo walizotakiwa kuvaa maofisa wa Kijerumani zilikuwa za khaki na kofia nyeupe ngumu (helmet) ambazo zilikuwa zimeidhinishwa na Ofisi ya Ukoloni jijini Berlin kwa ajili ya Jeshi la Afrika Mashariki mwezi Juni 1891. Lakini nguo hizo zilifika Kilwa mwezi Julai 1891 wakati jeshi la von Zelewiski likiwa limeondoka. Kwa hiyo, von Zelewiski na maofisa wake wa Kijerumani walivaa sare za enzi za Jeshi la Wissmann zilizokuwa na michirizi ya njano mikononi. Wale askari wa Kiafrika walivaa kofia nyekundu za tarbush na sare za khaki.
Wapagazi na watu wengine kwenye msafara huo walivaa nguo kama zilizokuwa zikivaliwa na watu wa makabila mengine wakiwemo Wahehe wenyewe na hawakuwa na kofia wala viatu.

Askari walikuwa na bunduki aina ya Mauser Jägerbüchse 71 pamoja na S71 ambazo pia zilitumiwa na maofisa wadogo wa Kijerumani. Makambanda wao walikuwa na bastola kubwa aina ya 1879 Revolver. Wapiganaji wa Kiafrika wao walikuwa na silaha za jadi ikiwemo mikuki.
Tutaendelea...

No comments:

Post a Comment