Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday 11 November 2013

RAIS KIKWETE, AKINA KAGAME WANAKUONEA GERE WEWE KUAMBATANA NA OBAMA

Rais Kikwete (kulia) akiwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya walipokutana nchini Afrika Kusini.

Mheshimiwa Rais,
Nimesikiliza hotuba yako Bungeni kuhusu msimamo wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ilikuwa nzuri na uliondoa shaka iliyokuwa imetanda miongoni mwa Watanzania na hata wale waliodhani pengine utawakashfu ama kuwalalamikia marais wenzako ndani ya EAC ambao wanakutenga.
Pamoja na ukweli kwamba binafsi sikuitegemea, lakini nimeridhika kwa kiasi kikubwa. Nilitegemea ungezungumzia kuhusu Operesheni ya Kuzuia Ujangili ambayo wabunge wameizuia (pengine kwa hofu kwamba kwa hatua ilipofikia, wale waliokamatwa wanaweza kuwataja miongoni mwao wanaojihusisha upopoaji wa tembo na wanyama wengine kwa maslahi yao). 
Wakati mwingine ukiona wabunge wetu – ambao tumewazowea – wanalivalia njuga jambo fulani, inabidi ujiulize mara mbili mbili kwamba kuna kitu wanachokikusudia, siyo bure. Sitaki kulizungumzia hili kwa sababu hata mwenyewe unakumbuka wakati ule walipoleta kwako hoja ya posho ili usaini – ukala jiwe.
Nilitegemea utazungumzia kuhusu Katiba Mpya pamoja Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, lakini haya yote – kama ulivyosema mwenyewe kwenye utangulizi wako – hayakuwemo kwenye hotuba yako.
Badala yake ukazungumzia mambo manne tu – suala la ardhi, uhamiaji, ajira pamoja na sarafu moja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwamba ndio msimamo wetu, lazima Watanzania wapewe kipaumbele na tusiruhusu maeneo hayo yakaingia kwenye jumuiya, tutakwisha kabisa. Masuala haya hata Mtanzania anayeishi kule nyumbani Kibaigwa anayajua!
Lakini ulipotoa msimamo kwamba Tanzania haikusudii kujitoa kwenye EAC hata kama akina Uhuru Kenyatta, Yoweri Museveni na Paulo Kagame wataendelea kukutenga katika vikao vyao, nilifarijika. Nikakumbuka kwamba hawa jamaa, au niseme hizi nchi – hasa Kenya na Uganda – ndizo zinaelekea kuwa chanzo cha kuvunjika kwa Jumuiya ile ya kwanza mwaka 1977.
Kuna kitu ambacho kwa upeo wa akili yangu nimekiona kufuatana na huu msimamo wa hawa jamaa. Yoweri Kaguta Museveni wakati akipigana msituni hadi kuingia madarakani mwaka 1986 alikuwa akiungwa mkono na Mataifa ya Magharibi, hasa Marekani. Yeye ndiye alikuwa ‘mtu wao’ katika ukanda huu kwa ajili ya kulinda maslahi yao.
Baadaye alipokuja Meja Paulo Kagame, jasusi ambaye alisaidiwa na Tanzania kwa mafunzo kama tunavyosikia, Marekani ikamuunga mkono hasa baada ya mauaji ya Juvenal Habyarimana na Cyprien Ntyaramira mwaka 1994 yaliyofuatiwa na mauaji ya kimbari. Mpaka sasa hakuna anayetaka kuzungumza wala kunyoosha kidole kwa yeyote aliyehusika na njama za kuilipua ndege ya Rais Habyarimana. Hakuna.
Kwa miaka yote hiyo ameungwa mkono na Marekani (iwe kwa siri au hadharani), lakini kitendo chake cha kuendelea kuwaunga mkono waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kimeonyesha kuwakasirisha Marekani na mataifa mengine ya Magharibi ambayo yanamuona amekuwa mwiba. Ugomvi uliopo ni mawe yaliyoko kwenye ardhi ya Congo.
Upepo ukabadilika tena mwaka 2008 wakati Marekani ilipoichagua Kenya (chini ya Emilio Mwai Kibaki) kuwa ndiyo ngome ya vikosi vyake vya kijeshi vya AFRISOM na AFRICOM kupambana na magaidi wa Al-Shabaab na kurahisisha kusaidia majeshi ya UM katika migogoro inayoendelea Afrika. Kagame akawa rafiki wa zamani wa Marekani.
Marekani wakawa na uhakika kwamba kama Raila Odinga angeshinda Urais Kenya, basi maslahi yao yangeweza kuendelea kulindwa. Pamoja na udhaifu wake alionao, lakini Marekani iliamini Odinga angeweza kuwa bora zaidi ya Kenyatta, ambaye mpaka sasa hivi inaonekana hawamkubali huku akiwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa huko The Hague.
Bahati mbaya zaidi, George Walker Bush alionekana kujiandaa kutafuta swahiba mwingine kwenye ukanda huu. Akakuona wewe – kwa maana ya Tanzania – kuwa unafaa kwa kuwa hufungamani na upande wowote. Akaja na kufanya ziara ya siku nne, ikiwa ni ziara ndefu zaidi kwa Rais wa Marekani katika nchi za Kiafrika.
Alipochaguliwa Obama mwaka 2008 na hata mwaka 2012, Wakenya walikuwa na matumaini makubwa kwamba Marekani ‘haitapindua’ kwa lolote kwa kuwa Obama ni Mjaluo wa Kisumu. Walidhani pamoja na kuwa mkuu wa Ikulu ya Marekani, bado angeweza kutoa hisani kwa nchi yake ya asili. Kinyume chake, Obama anaongoza kwa kufuata Katiba na Sera za Marekani.
Alipopanga ya ziara ya Afrika kwa mara ya pili, Wakenya waliamini angekwenda kwao. Lakini angekwendaje wakati Uhuru anatuhumiwa kwa machafuko yaliyosababisha mauaji? Marekani haiamini kama Uhuru hana hatia, pengine mpaka hukumu itakapotolewa.
Badala yake, akakumbuka kwamba mwenzake Bush aliacha swahiba huku, hivyo akaamua kuja Tanzania. Jamaa walipiga kelele weee wakidhani utaratibu huo ungebadilisha, waliposhindwa kushawishi, wakaamua kususia kuja Dar es Salaam wakati Obama alipotua.
Sasa kinachoonekana hapa ni kwamba, wanakuonea gere tu wewe kuwa rafiki wa Marekani. Kuanzia Museveni, Kagame na Kenyatta ambao wanahisi kwamba umewazibia fursa zao kwa taifa hilo kubwa duniani.
Kama zipo sababu nyingine ambazo mimi na Watanzania wenzangu hatuzijui, labda, lakini kwa uelewa wangu, nadhani chuki zao dhidi yako ni gere tu, hakuna kingine zaidi.
Mheshimiwa Rais, mimi nakushauri chapa kazi, wacha waseme weee, watachoka. Watakufa navyo vijiba vya roho.
Wasalaam.

No comments:

Post a Comment