Shekh Sharif Matongo, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ndoto aliyoota juu ya Tanzania mwaka 2015 jijini Dar es Salaam jana. PICHA: HALIMA KAMBI
Siku chache baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kutangaza nia ya kuwania nafasi ya Urais katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Shekh Sharif Matongo ameibuka na kusema kuwa mmoja wa kiongozi mkubwa anayewania nafasi hiyo katika chama hicho atafariki dunia.
Kabla ya Nyalandu waliotajwa kuanza kampeni za kuwania nafasi hiyo ya kurithi mikoba ya Rais Jakaya Kikwete, ambaye anakamilisha miaka yake 10 ya kuliongoza taifa hili ni Waziri wa mawaziri wakuu wastaafu, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa.
Wengine wanaotajwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Stephen Wasira; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Mbunge wa Songea Mjini; Dk. Emanuel Nchimbi na Waziri wa Sheria na Katiba Dk. Asha-Rose Migiro.
Waliotangaza nia katika maeneo tofauti ndani na nje ya nchi ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala.
Sheikh Sharif, alitoa utabiri huo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na Waandishi wa habari juu ya ndoto ziliyomjia usiku na kuoteshwa mambo zaidi ya matano yatakayo ikabili nchi mwaka huu.
Alisema atakayefariki dunia ni yule mgombea anayewania nafasi ya urais ambaye alishawahi kuwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali kupitia CCM.
“Ndoto yangu nilioteshwa sikukaa nayo peke yangu niliwaeleza masheikh mbalimbali na kupata ushauri kutoka kwa Mufti wa Abuu Dhabi, Mufti wa Nigeria na wengine wote wakaniambia suala hilo nisikae nalo niwashirikishe watanzania wenzangu,’’alisema Sheikh Sharif.
Alizitaja sifa za rais atakayeshinda katika kinyang’anyiro hicho kuwa ni yule ambaye alishawahi kuishi nje ya nchi kwa muda mrefu kwa mujibu wa ndoto hizo.
Alifafanua kuwa mbali na mgombea huyo kufa ambaye hakumtaja jina lake, pia vijana wengi watashinda katika uchaguzi ujao na kwamba wazee wengi watashindwa.
“Uchaguzi ujao ambao nimeoteshwa pamoja na mambo mengine yatakayotokea mwaka 2015, vijana wengi watashinda katika uchaguzi ujao na wazee wataangushwa sana,” alisema Sheikh Sharif.
Pia alisema katiba inayopendekezwa itapita licha ya vurugu zitakazotokea ambazo zitaibuliwa na vijana katika mchakato huo ambao utaanza mapema mwaka huu.
Akizungumzia hali ya usafiri, alisema bahari itachafuka na chombo kimoja kitazama kutokana na machafuko hayo.
Alisema ndoto nyingine ni kutokea kwa mvua kubwa itakayosababisha madhara makubwa vikiwamo vifo vya watu pamoja na uharibifu wa miundombinu pamoja na magonjwa ya watoto yatakayosababisha vifo.
“Ndoto hizi ni lazima zizingatiwe kutokana na kwamba nilipata ushauri wa watu wengi wenye kuaminika katika jamii katika mataifa mbalimbali ulimwenguni. Na serikali isidharau katika haya yote niliyosema na pindi yanapotokea matatizo madogo madogo wachukue hatua,” alisema Sheikh Sharif.
Utabiri wa Sheikh Sharif umekuja siku chache baada ya mrithi wa Mnajimu na Mtabiri wa Afrika Masharik Kati na Kusini, Marehemu Sheikh Yahaya Hussein, Alhaj Maalim Hassan Yahaya Hussen, kutabiri kufariki kwa mgombea wa urais katika kinyang’anyiro za uchaguzi mkuu mwaka huu.
Aidha Mnajimu huyo alieleza kuwa mgombea huyo ambaye ni mzee kwa umri anayetajwa kuwepo katika sakata la kusaka urais ndiye atakaye fariki.
Katika utabiri huo wa mgombea ambaye hakumtaja jina alisema atadondoka jukwaani na kukutwa na mauti.
Sheikh Sharif Matongo, alizaliwa mwaka 88 na aliweza kuongea akiwa na miezi tisa tangu kuzaliwa kwake.
Sheikh Sharif ambaye alidai kuwa yeye siyo mtabiri bali ni mbeba maono, tayari amesilimisha watu zaidi ya 672,000.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akizungumzia hali hiyo ya watu na wanajimu mbalimbali kutabiri kuhusu uchaguzi huo, alisema huo ni utabiri hauwezi kuwa ukweli.
Alisema, utabiri kama huo hauamini na kwamba kinachotokea na maono ya mtu ambayo hayawezi kuathiri chochote.
“TB Joshua 2010 alitabiri utabiri ambao haukutimia, hivyo siamini katika hili na hatuoni haja ya kuendelea kuamini vitu kama hivi, wala hatuombea yatokee hayo,” alisema Mbowe.
Alisema hakuna demokrasia ya kweli inayotokana na utabiri kama huo, hivyo haamini kama inaweza kuwa hivyo kwani hayo ni maneo na siyo matendo ambayo yapo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM), Sixtus Mapunda, alisema yeye haamini utabitiri wa aina hiyo.
Alisema pia hauwezi kuathiri uchaguzi ujao kwa sababu haamini hivyo na kama unaweza kumuathiri mgombea ni kutokana na imani ya mgombea mwenyewe.
“Mimi siyo mtabiri na siamini utabiri wowote, kama kiongozi ataogopa utabiri huo ni yeye mwenyewe na imani yake. Kila mgombea anatakiwa ajue namna ya kukabiliana na utabiri wa namna hiyo,” alisema Mapinda.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment