Gor Mahia ikimenyana na watani wao wa jadi AFC Leopards katika moja ya mechi za Ligi ya Kenya miaka ya 1980.
Mashabiki wa Gor Mahia wako kila mahali dunia kwa sasa.
Na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com
HAPANA
shaka yoyote kwamba Gor Mahia ndiyo timu pekee ya Afrika Mashariki ambayo
imepata mafanikio makubwa katika mashindano ya Afrika baada ya kutwaa Kombe la
Washindi Afrika mwaka 1987, ambalo sasa limefutwa.
Mtandao wa www.brotherdanny.com unaendelea kuwaletea uchambuzi wa kihistoria katika mashindano
haya ambayo mwaka 2015 yanafanyika jijini Dar es Salaam.
Katika
mashindano ya Kombe la Kagame, timu hiyo inashika nafasi ya nane kwa kushinda
mechi 24 kati ya 54 ilizocheza, kutoka sare 15 na kupoteza 16, lakini ikifunga
jumla ya mabao 75 na kufungwa 49.
Inashiriki
mara ya 14, lakini katika safari 13 ilizoshiriki imetwaa mara tatu ubingwa
katika miaka ya 1980, 1981 na 1985, imeshika nafasi ya pili mara moja mwaka
1984 na kurudia nusu fainali mara nne mwaka 1975, 1982, 1991 na 1996. Miaka mingine
iliposhiriki ni 1977, 1983, 1986, 1994, na 2014.
Mabingwa
hao wa Kenya hawajapoteza mechi msimu huu huku wakionesha dalili za kutangaza
ubingwa mapema kabisa.
Timu hiyo
inajivunia hazina ya wachezaji wenye vipaji wakiwemo Khalid Aucho, George
Odhiambo, Micheal Olunga, Mnyarwanda Meddie Kagere na walinda mlango Boniface
Oluoch na nahodha Jerim Onyango. Pia yumo mlinzi wa Uganda Cranes Godfrey
Walusimbi. Inanolewa na Mskochi Frank Nutall anayesaidiwa na mzalendo kipa wa
zamani Mathew Ottamax.
Wachezaji
wengine ni Kevin Oluoch, Musa Mohammed, Collins Okoth,
Ronald Otieno, Timothy Otieno, Ali Abondo, Abouba Sibomana (Uganda), Abdoul
Nizigiyimana (Rwanda), Dirkir Glay (Liberia), Jerry Santos, Martin Werunga, Charles
Bruno, Erick Ochieng, Haron Shakava, Ernest Wendo, Khalid Aucho (Uganda), Boniface
Oluoch, Israel Emuge (Uganda), Simon Pierre (Cameroon), David Juma, Bernard
Odhiambo na Innocent Wafula.
Ipo katika
Kundi A pamoja na Yanga, Al Khartoum ya Sudan, KMKM ya Zanzibar na Telecom ya
Djibouti.
Historia yake
Gor Mahia, ambayo nchini Kenya inafahamika
kwa majina mengi ya utani ya Kiluo kama K'Ogalo (Nyumba ya Ogalo), Mayienga (Tetemeko),
Sirkal (Serikali) na Taya (Mwanga) ilianzishwa rasmi Februari 17, 1968. Inautumia
Uwanja wa City wenye uwezo wa kuingiza wazamaji 15,000 pale Nairobi.
Klabu hiyo ambayo ina upinzani wa jadi (wa
kikabila) na Afc Leopards (zamani ikiitwa Abaluhya FC) imepata kutwaa ubingwa
wa Kenya mara 14, ikiipiku AFC Leopards kwa msimu mmoja. Pia imetwaa Kombe la
Rais la KFF mara 10.
Ndiyo timu pekee kutoka ukanda wa Cecafa
kutwaa taji la klabu za Afrika mpaka sasa, baada ya kushinda Kombe la Washindi
Afrika mwaka 1987 ikisaidiwa sana na mabao ya vichwa vya Peter Dawo.
Kuanzishwa kwa klabu hiyo kulitokana na
muungano wa klabu za Wajaluo – Luo Union na Luo Sports Club (Luo Stars) – na ilitwaa
ubingwa katika msimu wake wa kwanza tu kuingia 1968.
Baadhi ya waasisi wake ni Tom Mboya na
Jaramogi Oginga Odinga. Klabu hiyo ilipewa jina kumuenzi mganga wa jadi maarufu
kutoka Homa Bay katika nadharia za Kiluo, ambaye jina lake la utani lilikuwa Gor
Mahia ("mahia" ni neno la Kiluo ambalo maana yake ni "miujiza")
kwa sababu alikuwa maarufu kwa kufanya miujiza. Jina maarufu la utani la klabu
hiyo, K'Ogalo, pia linatokana na mganga wa jadi, ambaye jina lake halisi lilikuwa
Gor Wuod Ogada nyakwar Ogalo (Gor mwana wa Ogada mjukuu wa Ogalo), na alikuwa
akifahamika kama Gor Makogalo, au Gor K'Ogalo kwa kifupi, likimaanisha "Gor
kutoka ukoo wa Ogalo".
Hata hivyo, klabu hiyo ilikuwa imeanzishwa
mapema zaidi katika miaka ya 1910, na ikashiriki katika mashindano ya mitaani
huko Kenya Magharibi. Makundi mbalimbali yalitumia jina la Gor Mahia kwa
nyakati tofauti.
Mwaka 1976, Gor Mahia ilitwaa ubingwa bila
kupoteza hata mchezo mmoja ikijivunia ‘uchawi’ wa kocha mchezaji Allan Thigo. Alikuwa
anasaidiwa na nyota kama Festus Nyakota, James Ogolla na wachezaji wapya Jerry
Imbo aliyesajiliwa kutoka Black Mamba na mshambuliaji mashuhuri Maurice Ochieng
kutoka Polisi Kenya. Kipa George Ayuka alikuwa hafungiki msimu mzima. Maurice
Ochieng alimaliza msimu akiwa amepachika mabao 20, mbele ya mkongwe William
"Chege" Ouma aliyepachika mabao 16.
Kikosi cha mwaka 1976 ni moja ya vikosi
imara ambacho timu hiyo imepata kuwa navyo. Kilihusisha wachezaji nyota kama Masanta
Osoro, Paul "Cobra" Oduwa, Festus Nyakota, Duncan Aluko na Duncan
Migan, wote walikuwa wakiichezea timu ya taifa. Waziri wa sasa wa Barabara wa
Kenya, Chris Obure, pia aliichezea Gor katika miaka ya 1970.
Gor Mahia iliichapa AFC Leopards bao 1-0 kutwaa
ubingwa wa ligi mwaka 1983 na mwishoni mwa mechi hiyo, Rais Daniel arap Moi
akakabidhi taji kwa nahodha Peter Otieno Bassanga.
Gor Mahia ilitwaa kombe jipya la Dhahabu la
Moi mwaka 1986 kwa kuichapa Bandari 1-0 kwenye fainali. Bao la dakika za
majeruhi la Hezborn Omollo liliipatia ubingwa kwenye Uwanja wa Nyayo. Kikosi imara
cha Bandari kikinolewa na Mohammed Kheri kilikuwa kinashiriki kwenye Ligi ya
Kanda ya Pwani. Kwa kutwaa taji hilo Gor ikapata nafasi ya kushiriki kwenye
Kombe la Washindi Afrika mwaka 1987.
Mafanikio:
Kombe la Washindi: Bingwa 1987
Ubingwa wa Cecafa: Mara 3
1980, 1981, 1985
Ubingwa wa Kenya: 14
1968, 1974, 1976, 1979, 1983, 1984, 1985,
1987, 1990, 1991, 1993, 1995, 2013, 2014
Kombe la Chalenji Kenya/Kombe la Dhahabu la Moi/Transparency
Cup/President's Cup/Kombe la KFF/Kombe la FKL: 10
1976, 1981, 1983, 1986, 1987, 1988, 1992,
2008, 2011, 2012
Kombe Kubwa la Kenya (Super Cup): 3
2009, 2013, 2015
Kombe la Shirikisho la CAF: Imeshiriki
mara 3
2009 – Raundi ya Awali
2012 – Raundi ya Awali
2013 – Raundi ya Kwanza
Klabu Bingwa Afrika: Imeshiriki
mara 8
1969: Robo Fainali
1977: Raundi ya Pili
1980: Raundi ya Pili
1984: Ilivunjika katika Raundi ya Pili
1991: Raundi ya Kwanza
1992: Robo Fainali
1994: Raundi ya Kwanza
1996: Raundi ya Kwanza
Kombe la CAF: Imeshiriki
mara 2
1993 – Robo Fainali
1998 – Raundi ya Kwanza
Kombe la Washindi: Imeshiriki
mara 7
1979 - Fainali
1981 – Robo Fainali
1982 – Ilijitoa Raundi ya Kwanza
1983 – Raundi ya Awali
1987 - Mabingwa
1988 – Robo Fainali
1989 – Nusu Fainali
KUMBUKUMBU HIZI ZIMEANDALIWA
NA MTANDAO WA www.brotherdanny.com. Tafadhali ukirejea weka chanzo cha habari.
No comments:
Post a Comment