![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhC0zc6VWn1IrJAvrQp_zZOS3J6Z5mH6l7jp8H8Rbl5typQAeg_xKb6iiBaJXPANFcGi5PcSxTCt3Y3DVW5jFc6LXFAQmnUALD0p6GMqlcrTQhhjfbPNaGVe4bG-lOv39CUuEM4qXNTtVg/s640/3A.jpg)
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Bernard Membe (kushoto) akipongezwa na Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa kwa kuingia kwenye 'tano bora' mjini Dodoma hivi karibuni.
Na Daniel Mbega, Dodoma
NDOTO za
kachero Bernard Kamilius Membe (62) za kuwa raia namba moja wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania zimekatika ghafla.
Ni sawa na
kumshtua ‘teja’ wa dawa za kulevya ambaye baada ya kujidunga sindano anasinzia
akiota kujenga ghorofa linaloelea angani huku yeye akiwa na mabawa, lakini
anaposhtuliwa na kujikuta yuko pale pale kijiweni, humchukia kila
aliyemzunguka, hususan yule aliyemwamsha.
Naam. Julai
11, 2015 Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi imeleta mapinduzi kwa kumwengua
Bernard Membe kutwa moja tu baada ya hali ya hewa mjini hapa kubadilika
kufuatia kuenguliwa kwa Edward Lowassa na kusababisha kikundi cha vijana
wasiozidi 100 kufanya fujo za hapa na pale.
Kuenguliwa
kwa Membe, ambaye tangu mwaka 2011 alisema alikuwa akisubiri kuoteshwa ndoto
ili awanie urais, kumeleta faraja kwa makundi mengi ndani ya chama hicho na pia
walau kuleta utulivu hasa baada ya kusikia kwamba walioingia tatu bora ni Dk.
John Pombe Magufuli aliyeongoza kwa kupata kura 290, Balozi wa Kudumu katika
Umoja wa Afrika Amina Salum Ali aiyepata kura 284 na Dk. Asha-Rose Migiro
aliyepata kura 280.
Membe aliburuza
mkia kwenye hatua hiyo baada ya kupata kura 120 nyuma ya January Makamba
aliyepata kura 124.
Lakini
duru za siasa zinasema kuenguliwa kwa Membe kumekuwa faraja kwa ‘maadui zake
11’ ambao walikuwa na hofu kwamba kama angepitishwa na CCM, basi wangetafuta
mahali pa kukimbilia.
Akihojiwa
katika kipindi cha Dakika 45 cha runinga ya ITV mnamo Julai 16, 2012, Membe,
akiongea kwa hisia na uwazi kuhusu maisha yake ya kisiasa pamoja na mvutano
uliopo kati yake na mahasimu wake, alisema ana maadui 11 na kuapa kwamba mwaka
2016 ‘wangekimbilia Kenya’, pengine akijua kwamba wakati huo yeye ndiye
angekuwa rais.
Maadui wa
Membe, kwa mujibu wa maelezo yake, ni wale wote wanaomzushia kashfa ambapo kati
ya 11, wawili ni waandishi wa habari na kwamba ipo siku angewataja kwa majina
na sura zao kwani kwa wakati huo alikuwa akikusanya taarifa za kila mmoja na
kutengeneza ‘dossier’ ili hatimaye awataje hadharani.
‘Kisasi’
hicho kimetajwa kwamba huenda ni sababu mojawapo ambayo iliyomuondoa kwenye
kinyang’anyiro hicho kwa maelezo kwamba CCM inaona siyo vyema kuwa na kiongozi
mwenye visasi.
Hata
hivyo, sababu kubwa iliyobainishwa na vyanzo vya habari kutoka ndani ya duru za
siasa kwenye CCM ni ‘ushemeji’ wake na Rais Jakaya Kikwete, ambao umeelezwa
kuwa ndio uliochangia akaingia kwenye ‘tano bora’.
Kikundi
cha vijana waliokuwa wakiimba na kudai kwamba ni wafuasi wa Lowassa, kilieleza
hisia zake kuwa “Membe ameingia tano bora kwa kubebwa kwa sababu ni shemeji wa
Rais Kikwete.”
Dhana ya
‘ushemeji’ inakuja kutokana na mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, kutoka mkoani
Lindi ambako ndiko anakotokea Membe na familia namba moja imekuwa karibu na
Waziri huyo wa Mambo ya Nje.
Vyanzo vya
ndani ya CCM, hususan Kamati ya Maadili na Usalama pamoja na Kamati Kuu,
vinadokeza kwamba kulikuwepo na kutokuelewana baina ya wajumbe kuhusu Membe,
ambaye hata wazee wa chama hicho walionyesha mashaka yao ya wazi.
Inaelezwa
kwamba, hiyo ndiyo sababu pia ya makada watatu wa chama hicho, Dk. Emmanuel
Nchimbi, Adam Kimbisa na Sophia Simba kutangaza kujitoa kwenye Kamati Kuu
wakipinga namna mambo yalivyoendeshwa.
Hata
hivyo, taarifa zinasema makada hao watatu Jumamosi walifuatwa na viongozi wa
juu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) kuombwa wafute kauli yao na warejee kwa wenzao
ili wakijenge chama.
Kelele
zilizokuwa zikiendelea nje ya ukumbi Jumamosi kutoka kwa vijana wanaomuunga
mkono Lowassa, kwamba wanakitaka chama chao au watarudisha kadi za chama na
kuelekea upande mwingine, nazo zinatajwa kuwa ni sababu ya kuenguliwa kwa Membe
kwa hali haikuwa nzuri, si hapa Dodoma tu, bali hata katika miji mingine.
Tangu
mwaka 2014, ilielezwa kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya
habari kwamba familia ya Rais Jakaya Kikwete (hasa Mama Salma na Ridhiwani) ndiyo
ilikuwa nyuma ya kampeni za Membe na kwamba haikushangaza wakati jina lake
lilipoingia kwenye tano bora.
Wengine
waliokuwemo kwenye timu hiyo ni Lazaro Nyalandu, ambaye pamoja na kujitokeza
kugombea alikuwa kama anayeweka ‘foleni’ tu ili kupunguza kura kwa baadhi ya
watu.
Wamo pia
Paul Makonda na Jack Steven Gotham anayedaiwa kuwa ndiye aliyekuwa akiratibu
zoezi la kukusanya fedha
Miaka
mitatu nyuma Membe aliripotiwa na gazeti la RAI
kwamba alikuwa akilitumia vibaya jina la Rais kwa kitendo chake cha kupita
katika nchi za Kiarabu kuomba fedha na magari, hususan Muungano wa Falme za
Kiarabu (UAE).
Ilielezwa
kwamba, Membe alikuwa akitumia wadhifa wake serikalini na uhusiano kati ya
watawala wa UAE na Tanzania kufanikisha azma hiyo.
Familia ya
kifalme ya nchi hiyo chini ya Sheikh Mohammed bin Al Maktoum, mbali na
mahusiano ya kidiplomasia, wamekuwa wawekezaji katika sekta ya uwindaji wa
kitalii nchini kwa zaidi ya miongo minne.
Pamoja na
Membe kuzikanusha tuhuma hizo na nyingine nyingi, lakini bado kuna watu
wanaamini hiyo ni kashfa ambayo haikuwa na nafasi ya kumpa madaraka makubwa.
No comments:
Post a Comment