Mabingwa mara tano wa michuano ya Kombe la Vilabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati timu ya Gor Mahia kutoka nchini Kenya, leo imeshinda mchezo wake wa pili mfululizo baada ya kuichapa KMKM ya Visiwani Zanzibar kwa mabao 3-1.
Mabao ya Gor Mahia yalifungwa na mshambuliaji Meddy Kagere bao moja, Michael Olunga aliyefunga mabao 2, huku bao la kufutia machozi la KMKM likifungwa na Matheo Anthony.
Katika mchezo wa awali uliochezwa saa 8 mchana, Khartoum ya Sudan iliichapa timu ya Telecom ya Djibout kwa mabao 5- 0, mabao ya Khartoum yalifungwa na Wagdi Abdallah, Ousmaila Baba, Murwan Abdallah, na Salah Bilal aliyefunga mabao mawili.
Kwa matokeo hayo ya leo Gor Mahia wamefikisha pointi 6, wakifuatiwa na Khartoum yenye pointi tatu sawa na KMKM wakipishana kwa idadi ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Wakati huo huo kesho siku ya jumanne waandishi wa habari walioomba vitambulisho vya kufanyia kazi (Accreditation) wanaombwa kufika ofisi za TFF zilizopo Karume kuchukua vitambulisho vyao.
Waandishi mnaombwa kuchukua vitambulisho hivyo kuanzia saa 5 kamili asubuhi mpaka saa 6 kamili mchana, kwani vitambulisho vya muda vilivyotolewa havitatumika tena.
Kuanzia michezo ya kesho jumanne kila mwandishi atapaswa kutumia kitambulisho kilichotolewa maalum kwa ajili ya michuano hiyo kuingilia uwanjani.
No comments:
Post a Comment