Baadhi ya wachezaji hawa wa Simba walikuwemo kwenye kikosi cha mwaka 1985 kilichoihenyesha National Al Ahly kule Mwanza.
NA DANIEL MBEGA
KLABU ya Simba ina rekodi nzuri katika michuano ya kimataifa. Hilo halina
ubishi. Na linapokuja suala la kupambana na klabu za Afrika Kaskazini (The
Maghreb) Simba ndio wameweza kuzionyesha
ubabe, japo kwa kiasi fulani, tofauti na klabu nyingine za Tanzania.
Mwaka 1985 Simba ndio walikuwa wanaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya
Kombe la Washindi Afrika. Katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza kwenye
uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Simba iliitandika Eritrea SF ya Asmara, Ethiopia
(wakati huo kabla Eritrea haijajitenga kutoka Ethiopia) kwa
magoli 5-0. Mchezo huo ulifanyika Machi 2.
Ziliporudiana
wiki mbili baadaye mjini Addis Ababa, yaani Machi 16, Simba ilifungwa goli 1-0.
Hata hivyo, ilisonga mbele kwa ushindi wa magoli 5-1. Sasa ilikuwa na kibarua
kigumu cha kupambana na mabingwa watetezi wa kombe hilo, National
Al Ahly ya Misri katika hatua ya raundi ya pili.
Mchezo
wao wa kwanza ulifanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Aprili 27, na
Simba ikaushangaza ulimwengu kwa kuifunga National 2-1. Simba siku hiyo
iliwakilishwa na Moses Mkandawire, Kihwelu Mussa, Athumani Maulid, Shaaban
Mussa, Thobias Nkoma, Ramadhani Lenny, Sunday Juma, Mtemi Ramadhani/Ezekiel
Greyson 'Juju Man', Malota Soma, Zamoyoni Mogella na Douglas Muhani/Twaha
Hamidu.
National Al Ahly iliwakilishwa na Ekramy El-Shahat, Midhat Ramadhani, Mohamed Saleh, Hamis
Abu-Radi, Rabii Yasin, Magdi Abdulghani, Said Mohamed, Mokhtar Mokhtar, Mahmoud
El-Khatib, Alaah Mahboub na Mohamed Amer.
Mtangazaji
wa Redio ya Misri siku hiyo alisikika akipayuka kwa Kiarabu muda mfupi kabla ya
dakika ya 85 ya mchezo; "Wahed Wahed, Al Ahly Wahed, Simba Wahed....aaah,
Sheitwan, gooo!!", yaani "Moja moja, Al Ahly (National) moja, Simba
moja....aaaah, Shetani, gooo!!"
Lilikuwa
ni goli la pili la Simba ambalo mtangazaji huyo alikuwa akililaani vikali.
Baada ya matokeo hayo, wachezaji na viongozi wa National walisikika
wakisema "Cairo Four", yaani
Simba ingefungwa magoli manne huko Cairo katika mchezo wa marudiano.
Katika
mchezo huo, Simba ikiwa imefungwa dakika tano kabla ya mapumziko, iliweza
kusawazisha katika dakika ya 44 na kujipatia goli la ushindi dakika tano kabla
ya mpira kumalizika. Zamoyoni Mogella ndiye aliyeisawazishia Simba kunako
dakika hiyo ya 44.
Baada ya
kupasiana kati ya Kihwelu Mussa, Ramadhani Lenny na Malota Soma, mpira
ulimfikia Zamoyoni Mogella ambaye aliachia shuti kati katikati ya mabeki wa
National. Mpira ulimwamba wa juu na kisha kurejea ardhini kwa nyuzi 90.
Lilikuwa goli safi sana la mwaka 1985.
Goli la
National lililopatikana katika dakika ya 40 lilikuwa zuri na kiufundi. Baada ya
pasi 14, Mahmoud El-Khatib aliachia kiki ambayo ilikwenda moja kwa moja wavuni
huku Moses Mkandawire akiwa amelala upande mwingine.
Goli la
ushindi kwa Simba lilifungwa na nahodha wake, Mtemi Ramadhani katika dakika ya
85 kutokana na juhudi kubwa za wachezaji wa Simba, ambao pamoja na kucheza
mpira wa kiwango cha chini ukilinganisha na wenzao National walikuwa
wamedhamiria kweli kuibuka na ushindi siku hiyo.
Katika
mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa Gamal Abdel Nasser mjini Cairo Mei
11, 1985 mbele ya mashabiki 80,000, Simba
ilifungwa magoli 2-0 na National na hivyo kutolewa kwa jumla ya magoli 3-2.
Goli la kwanza la National lilifungwa na Mahmoud El-Khatib ‘Bibo’
dakika ya 37 na lile la pili lilifungwa na Zakaria
Nassir dakika ya 59.
Kwenye mechi ya Cairo, timu ziliwakilishwa hivi: Al Ahly: Ekram
El-Shabat, Mohammed Hashis, Rabiya Yassin, Amdi Aburabi, Magdi
Abdelghani/Mohammed Ameir, Zakaria Nassir, Mahmoud el Khatib 'Bibo, Mustafa
Abdul, Alaa Mayhobe, Taher Abuzaid.
Simba:
Moses Mkandawile, Kihwelu Mussa, Athumani Maulid 'Big Man'/Daudi Salum ‘Bruce Lee’, Thobias
Nkoma, Talib Hilal, Ramadhan Lenny, Ibrahim Marekano/Abdallah Mwinyimkuu, Mtemi
Ramadhan, Zamoyoni Mogella, Malota Soma, Sunday Juma.
Siku hiyo
mwamuzi alikuwa K. Teeluckdhaamy aliyesaidiwa na K. Mootiem na D. Desscan.
Tukirudi
katika mchezo wa kwanza mjini Mwanza, Simba siku hiyo iliweka rekodi ya kuwa
timu ya pili ya Afrika (Nje ya Misri) kuifunga National katika kipindi cha kati
ya mwaka 1982 hadi 1985. Tokea mwaka 1982, ni mwaka 1983 tu wakati National
ilipofungwa na Asante Kotoko ya Ghana goli 1-0 mjini Kumasi katika mchezo wa
fainali ya Klabu Bingwa Afrika. Kotoko ilitwaa ubingwa huo kwa goli
lililofungwa na Opoku N'ti, ambaye mwaka huo alikuwa Mwanasoka Bora wa Afrika.
Vinginevyo,
tokea mwaka 1982 mpaka hapo Aprili 27, 1985, National ilikuwa haijafungwa tena
katika mashindano ya Afrika. Kawaida ya timu hiyo ilikuwa ni
kutoka sare ama kushinda ugenini na kushindilia magoli mengi inapocheza
nyumbani.
Miongoni
mwa timu zilizokuwa zinaijua vizuri National ni Yanga, ambayo ilichapwa magoli
5-0 mjini Cairo na kutoka sare ya goli 1-1 Dar es Salaam mwaka 1982 katika
michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Kadhalika
katika mashindano hayo mwaka huo Nkana Red Devils ya Zambia ilifungwa 2-0 huko
Cairo baada ya kutoka sare ya bila kufungana mjini Lusaka, na Asante Kotoko
ilifungwa 1-0 huko Kumasi baada ya kutoka sare ya bila kufungana mjini Cairo.
Goli hilo liliipa National ubingwa wa Klabu Afrika mwaka 1982, ambalo lilifungwa
na Mahmoud El-Khatib, ambaye mwaka huo alikuwa Mwanasoka Bora wa Afrika (Mwaka
1983 alikuwa wa pili). Katika fainali ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 1984,
National iliifunga Canon Yaounde 1-0 huko huko Cameroon na 2-0 mjini Cairo.
NB:
Tembelea www.brotherdanny.com kila
siku kwa habari mbalimbali zilizotafitiwa kwa kina.

No comments:
Post a Comment