Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 30 May 2015

KUMBUKUMBU ZANGU: PAMBA FC ‘WANA KAWEKAMO TOUT PUISANT LINDANDA’ NDICHO KILIKUWA CHUO CHA SOKA TANZANIA

Kikosi cha Pamba cha miaka ya 1980. Nawatambua baadhi kwenye picha (nisahihisheni). Waliosimama kutoka kushoto: Madata Lubigisa, Rajabu Musoma, Beya Simba 'Nissan Patrol', Nteze John, Kitwana Selemani, Philemon 'Fumo' Ferdinand Felician, Paschal Mayala na Paul Rwechungura. 
Walioketi kutoka kushoto: George Gole, Khalfan Ngassa, Ally Bushiri, Alphonce Modest Pambamotosapi, Mao Mkami 'Ball Dancer', Selehe Mohammed, Hamis Nyembo na Nico Bambaga 'Machine'. Wachezaji wanne katika kikosi hiki - Musoma, Nteze, Ngassa na Modest - waliichezea Simba na wawili kati yao - Fumo na Bambaga - walichukuliwa na Yanga.

Na Daniel Mbega
KHALID Bitebo ‘Zembwe’, James Ng’ong’a, Anthony Nyembo, Madata Lubigisa, Ibrahim Magongo, Joram Mwakatika, Juma Mhina, Beya Simba, Abdallah Bori, Khalfan Ngassa, John Makelele ‘Zig Zag’, George Magere Masatu, Juma Amir Maftah, David Mwakalebela, Kitwana Selemani, Mao Mkami, Msonga Rashid, Hamza Mponda, Raphael Paul, George Gole, Paul Rwechungura, Andrew Godwin, Hussein Marsha ‘Smart Boy’, Nteze John Lungu, Bitta John, Deo Mkuki, Nico Bambaga ‘Machine’, Philemon ‘Fumo’ Felician… Orodha yao ni ndefu sana, lakini wote ni miongoni mwa wachezaji waliovuma sana katika soka ya Tanzania kwa miaka mingi.
Wachezaji wote hao, na wengine wengi, walivuma sana hasa walipokuwa na klabu ya Pamba FC ya Mwanza, ambayo ilifahamika zaidi kama Tout Puisant Lindanda wana Kawekamo.
Timu hiyo iliyovuma sana katika soka ya Tanzania kuanzia miaka ya 1970 mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1990 kabla haijabomolewa na klabu za Simba na Yanga, ilijivunia kitu kimoja kikubwa; kuwa na uwezo mkubwa wa kuibua na kuvipika vipaji vya wachezaji wengi, ambao walikuja kutamba hata kwenye timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Haikuwa ajabu katika miaka ya 1980 kuona kwamba timu ya mkoa wa Mwanza, Mwanza Heroes, ilikuwa ikiundwa na wachezaji wengi kutoka Pamba na wachache tu kutoka Toto African, Co-operetive United na nyinginezo.
Ni kutokana na kutoa wachezaji wengi nyota ndiyo maana Pamba ikaitwa ‘Chuo cha Soka Tanzania’, hususan baada ya Yanga kuuvunja mfumo wake wa kuwalea vijana wadogo ambao awali ulikuwa umeibua vipaji vya akina Juma Pondamali, Mohammed Adolph Rishard, Juma Matokeo, Sunday Manara, Kassim Manara, Mohammed Mkweche, Mohammed Yahya ‘Tostao’, na wengineo wengi.
Na katika kipindi cha uhai wake, Pamba ilikuwa timu ya kuogopwa kutokana na kandanda yake safi kiasi cha timu kongwe kama Simba na Yanga kuihofu kila wakati zilipokutana nayo. Ndio wakati ambao tulikuwa tukishuhudia ‘Big Match’! Yaani mechi kubwa ambayo iliwaweka wapenzi wengi roho juu wakiwa hawajui nani angeibuka mshindi.
Lakini unapozungumzia mafanikio ya timu hiyo tangu kuanzishwa kwake miaka ya 1960 mwishoni, basi yalipatikana mwaka 1990 wakati timu hiyo ilipofanikiwa kuunyakua ubingwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ulikuwa ni mwaka huo huo ambao timu hiyo ilibatizwa jina la utani la Wana Kawekamo, yaani Watoto wa Kawekamo.
Pamba ilipewa jina hilo na wapenzi ake ambao waliunganisha mafanikio hayo ya timu yao na ziara ya Baba Mtakatifu Papa John Paulo II nchini Tanzania.
Katika ziara yake nchini Tanzania mwaka huo, Papa John Paulo II alitembelea pia mkoa wa Mwanza na kutumia viwanja vya Kawekamo vilivyoko eneo la Nyamanoro kuendesha misa iliyovutia maelfu ya watu. Sasa mashabiki wakasema kwamba, mafanikio ya Pamba yalitokana na baraka za Baba Mtakatifu.
Ingawa Pamba ilitwaa ubingwa huo mwaka 1990, lakini huko nyuma ilikuwa moto wa kuotea mbali japokuwa haikuwahi kutwaa ubingwa, ikiukosa kwa ncha tu karibu mara mbili. Na kwa kudhihirisha umahiri wake, mwaka 1991 katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika timu hiyo iliweza kuiadabisha klabu bingwa ya Madagascar Anser Baluer kwa jumla ya mabao 13-0 katika raundi ya kwanza, rekodi ambayo ilichukua miaka mingi kuvunjwa.
Pamba ilikuwa tishio huko nyuma wakati wa Ligi ya Taifa, kabla ya kuanzishwa kwa ligi ya Tanzania Bara mwaka 1982. Kwa mfano, mwaka 1978 katika ligi kuu ya taifa, Pamba, ikiwa na wachezaji mahiri kama James Ng’ong’a, Anthony Nyembo, Madata Lubigisa, Ibrahim Magongo, Issa Meloo, Khalid Bitebo, na wengineo, ilivisambaratisha vigogo vya soka na kubebeshwa kila aina ya sifa hadi kunyakua taji la timu bora yenye nidhamu katika ligi hiyo.
Kituko kikubwa katika ligi ya mwaka huo 1978 iliyokuwa na timu sita katika hatua ya mwisho kilitokea kwenye Uwanja wa Taifa wakati Pamba ilipomenyana na Yanga. Siku hiyo Pamba ilitandaza soka safi na hadi mapumziko ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 ambayo yalipachikwa na Anthony Nyembo, lakini wakati timu zikienda mapumziko shabiki mmoja wa Yanga alishuka kutoka jukwaani na kukimbilia uwanjani akiwa na kisu mkononi kwa dhamira ya kutaka kumchoma mwamuzi wa mechi hiyo kwa madai kwamba alikuwa akiipendelea Pamba.
Kwa bahati nzuri, Shaaban Katwila, mchezaji wa Yanga, alimdaka na kumdhibiti lakini mkono ulioshika kisu ukateleza na shabiki huyo akataka kumchoma Katwila, na alipogundua kwamba huyo alikuwa ni mchezaji wa timu yake ya Yanga, nguvu zikamwishia akakidondosha kisu chini. Baadaye alitiwa nguvuni na wanausalama.
Yanga walifutika mpira kwapani na kugoma kuendelea na kipindi cha pili kwa madai kwamba walikuwa wakionewa na mwamuzi. Hata kabla ya mechi hiyo, Yanga walikuwa wamelalamika kwamba waamuzi walikuwa wakiwaonea. Wakajitoa kwenye ligi na baadaye wakafungiwa kwa miezi sita.
Baada ya mwaka huo, Pamba ilipotea kidogo na kuiachia nafasi hiyo Pamba ya Shinyanga, lakini ikarejea tena mwaka 1984 baada ya kupanda daraja wakati huo ikiwa bado na baadhi ya wachezaji wake wa mwaka 1978 kama Magongo, Meloo, Bitebo, Lubigisa na wengine walioongezeka kama Joram Mwakatika, Juma Mhina, Beya Simba 'Nissan Patrol', Abdallah Bori 'Maalim', Khalfan Ngassa, Edward Hiza, Kitwana Selemani, Mao Mkami ‘Ball Dancer’, Rwemaho Mkama, na wengineo.
Tangu wakati huo Pamba haikushuka daraja na ikawa tishio kweli kweli kwa timu za ligi daraja la kwanza Tanzania Bara. Timu hiyo ilizitambia Simba na Yanga iwe Dar es Salaam au Mwanza na ndipo mashabiki wake walipoipachika jina jingine la Tout Puisant Lindanda.
Kwa ujumla, Pamba iliyoanzishwa na Bodi ya Pamba Tanzania mwishoni mwa miaka ya 1960 ikijulikana kama Tanzania Lint, ilileta ushindani mkubwa wa soka katika mkoa wa Mwanza ambako kulikuwa na timu nyingine kama Co-operative United, timu kubwa ambayo ilififia baadaye, Toto African ambayo inajulikana kama tawi la Yanga, Nyamaume ambayo ilijulikana kama tawi la Simba, Mwatex iliyokuwa ikimilikiwa na kiwanda cha nguo Mwanza, na baadaye RTC Mwanza, miongoni mwa timu zilizokuwa zikimilikiwa na Kampuni za Biashara za Mikoa.
Lakini utawala wa timu hii ambayo ilichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo makubwa ya soka Tanzania kwa kutoa wachezaji wengi kwenye timu ya taifa, ulivurugwa na Simba, ambayo kuanzia mwaka 1980 iliweza kusajili zaidi ya wachezaji 20, baadhi yao ni John Makelele ‘Zig Zag’, Raphael Paul ‘RP’, David Mwakalebela ‘MP’, Nico Bambaga ‘Machine’, Khalfan Ngassa, George Masatu ‘Field Marshal’, Rashid Abdallah Magongo, Hussein Marsha ‘Smart Boy’, Bitta John, Hussein Bhalo, Juma Amir Maftah, Nteze John Lungu, Deo Mkuki, na wengineo wengi.
Yanga nayo ikafuata mkumbo kwa kuwazoa akina David Mwakalebela, Fumo Felician, Nico Bambaga na wengineo.
Mafanikio yote hayo sasa yametoweka na Pamba imerejea kwenye uwanja wa Nyamagana, au tuseme kwenye ligi ya chini tangu iliposhuka daraja mwaka 1999.
Timu hiyo ilikuwa ishuke daraja tangu mwaka 1996, lakini safari zote mbeleko ya Waziri wa Elimu na Utamaduni wa wakati huo, Profesa Juma Kapuya, iliinusuru baada ya kuingilia mara kadhaa siasa za soka na kuvuruga kanuni za ligi kwa kuibakisha timu hiyo na zingine kama Majimaji na Milambo Ligi Kuu.
Hata hivyo, Pamba bado itaendelea kuheshimika kama moja ya timu zilizokuwa na mafanikio makubwa katika soka ya nchi hii.


WASILIANA NAMI SIMU/WHATSAPP/TELEGRAM 0656 331974
barua-pepe: brotherdanny5@gmail.com
wavuti: www.brotherdanny.com

No comments:

Post a Comment