Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 31 May 2015

ALIYE MSAFI AWE WA KWANZA KUMPIGA MAWE LOWASSA

Mheshimiwa Lowassa akiwa kwenye Kanisa la SCOAN huku Nabii T.B. Joshua akihubiri. Hii ilikuwa Jumapili, Juni 12, 2011
Hii ilikuwa Juni 12, 2011 kama alivyokuwa akionekana ndani ya luninga ya emmanuel.tv

Na Daniel Mbega
MENGI yamesemwa kuhusu kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Edward Ngoyayi Lowassa, Mbunge wa Monduli, tangu kashfa ya Richmond/Dowans ilipoibuliwa bungeni.
Yanaendelea kusemwa kuhusu siri ya utajiri wake na wapi anakopata fedha anazozimwaga kwenye harambee mbalimbali. Wanasema anataka kununua urais.

Yeye mwenyewe wakati akitangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM Mei 30, 2015 pale kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha alisema kwamba anachukia umaskini na asingependa Watanzania waendelee kuukumbatia umaskini.
Wanaomfananisha na Oscar Kambona ambaye alipingana na sera za Mwalimu Julius Nyerere za Ujamaa na Kujitegemea bado wanaendelea kupinga hata uamuzi wake wa kutaka kuwania urais, ikiwa ni mara ya pili tangu alipoonyesha nia mwaka 1995 (yaani miaka 20 iliyopita).
Hakuna anayepinga kwamba Lowassa kama binadamu atakuwa amefanya makosa ndani na hata nje ya uongozi.
Hata hivyo, lazima tuelewe kwamba makosa yamefanywa na wengi ndani ya CCM na serikali yake na kama kuna mtu msafi, asiye fisadi wala mla rushwa, basi ajitokeze hadharani na kumtupia mawe Lowassa.
Lowassa hakuwepo kwenye maamuzi makubwa zaidi wakati ubinafsishaji ulipoanza mwaka 1994 ambapo tulishuhudia orodha ndefu ya mashirika ya umma – RTC na hata viwanda mbalimbali, viliuzwa (waliuziana wenyewe kwa wenyewe) au zilibinafsishwa kwa bei chee hata yale mashirika na viwanda vilivyokuwa vinazalisha kwa faida.
Ndiyo maana mwaka 1995 pale Uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati wa Mei Mosi, Mwalimu Nyerere aliwauliza ni kwa nini walikuwa wanabinafsisha hata mashirika yanayozalisha.
Ndiyo. Ufisadi mwingi umefanyika tangu Azimio la Arusha lilipozikwa Zanzibar mwaka 1991 na kuingia kwa soko holela. Kila mmoja mwenye tamaa ya mali akatamani kujilimbikizia. Akala, akashiba, akavimbiwa lakini hakuna aliyekinai.
‘Waliobahatika’ kugundulika wakastaafishwa ‘kwa manufaa ya umma’ lakini hawakushtakiwa. Wakapewa likizo isiyo na malipo ili waweze kutafuna vyema mali za umma walizozikwapua.
Walipoona ndani ya CCM wamefukuzwa, ama maovu yao yamebainika, wengi wakakimbilia upinzani na kuwa vipaza sauti hasa vya kuitukana CCM hiyo hiyo. Wakaficha makosa yao na kuwaaminisha Watanzania kwamba wao ni wasafi, wameonewa na waliobakia huko ndio wabaya zaidi!
Leo hii wanapomwandama Lowassa kwamba ni fisadi, mwizi na kadhalika, binafsi nabaki nawashangaa.
Mungu mwenyewe anasema: “Kutoka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mwenye akili, amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja…”
Sasa nani ndani ya CCM ama hao walioko upinzani, ambao wengi wao – kama si wote – wametokea CCM, asiye fisadi na mla rushwa? Yupo mwenye mikono safi? Kama yupo, basi namwamuru hatua mbili mbeleeee tembea, chukua jiwe na umpige Lowassa!
Ndugu zangu, mnasahau pia kwamba Mungu yu mwingi wa kusamehe. Anasema, dhambi zenu zijapokuwa nyekundu kama damu zitakuwa nyeupe seluji, zijapokuwa nyekundu kama bendera zitakuwa nyeupe kama sufi!
Lowassa amekwishajipambanua kwamba ametubia makosa yake – kama binadamu na kwa mujibu wa maelekezo ya Mwenyezi Mungu. Amekwenda ‘kuhiji’ Israel mwezi Februari 2008 mara tu baada ya kujiuzulu.
Hakuishia hapo, Juni 12, 2011 alikuwa ndani ya Kanisa la Synagogue Church for All Nations (SCOAN) jijini Lagos, Nigeria la mhubiri maarufu duniani Temitope Balogun Joshua maarufu zaidi kama T.B. Joshua ambako inaaminika kwamba wengi huenda kuombewa.
Wakati akiwa huko wengi wakasambaza taarifa kwamba ‘eti Lowassa ametabiriwa na T.B. Joshua atakuwa rais wa Tanzania’! Watu bwana!
Jamani eee, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Chuki zote hizi zinatokana na yeye kuonyesha nia ya kuwania urais kupitia CCM, sasa watu wamemua kupiga mishale kila kona. Mara Nyerere alimkataa, mara fisadi wa kutupwa, mara sijui nini…!
Jamani, Mfalme Suleiman, ambaye anafahamika kwamba ndiye binadamu pekee aliyekuwa na hekima duniani kuliko yeyote kabla yake ama baada yake, alikuwa na utajiri usio kifani. Taifa la Israel lilikuwa limebarikiwa kwa ajili yake. Kuna dhambi gani tukiwa na rais tajiri?!
Marekani ina viongozi matajiri wengi, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, John Kerry. Kuna dhambi gani hapo?
Kila mmoja ana namna alivyopata utajiri wake, na hata wewe unayesoma makala haya naamini una njia zako za kupata kipato. Kinachotakiwa ni kuomba neema ya Mungu atufunulie tuone kiongozi gani anayefaa.
Tusiwahukumu watu kwa sababu zetu binafsi, na ndiyo maana Nabii Nathan alikataa kuwatia mafuta watoto wakubwa wa Yesse mpaka Daudi alipoletwa. Mteule wa Mungu wa kuliongoza taifa hili katika awamu ya tano atapatikana kwa neema ya Mungu, lakini si kwa majungu na fitna.
CCM ina makada zaidi ya 10 waliotangaza nia. Hebu tuwaachie wanachama wenyewe wamchague wanayeona anafaa kukiwakilisha chama hicho na tusipandikize chuki na siasa za maji-taka.
Taifa hili ni letu sote, tusiliharibu kwa sababu binafsi maana kama tutakosa kiongozi bora taifa litayumba hili.
Ada ya mja kunena, nimesema yaliyo yakini.

No comments:

Post a Comment