Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 31 May 2015

UJUMBE KATIKA MUZIKI: KWELI DUNIA MSONGAMANO KAMA ANAVYOSEMA SUPREME NDALA KASHEBA!

Supreme Freddie Ndala Kasheba akiwa na swahiba wake enzi hizo Kikumbi Mwanza Pango 'King Kiki'.
Sikiliza kibao cha 'Dunia Msongamano'

Na Daniel Mbega
HABARI za leo wanabaraza wenzangu popote pale mlipo. Natumaini kila mmoja wetu yu bukheri wa afya kwa uwezo wa Jehova.

Maradhi humpata mtu yeyote yule, na kwa hakika kuugua siyo kufa! Lakini inashangaza baadhi ya walimwengu, tena wakati mwingine wale ambao ni watu wa karibu yetu kabisa, hutokea kuombea kwamba fulani afe. Wengi hugeuka watabiri kila wanaposikia fulani anaumwa, na moja kwa moja mawazo yao huwapelekea kuamini kwamba watu hao hawatapona bali watakufa!
Fikiria mtu anasikia kwamba unaumwa, lakini bila kujua kinachokusibu, anapokuja kukujulia hali badala ya kukufariji anakwambia; “Mimi na mke wangu tumekubaliana kuzikwa hapa hapa Dar, wewe umepanga kuzikwa wapi?!”
Labda pengine, kama ni ninyi mngemjibu vipi mtu huyu, ambaye kwa vyovyote vile mnamtegemea kama mmoja wa wazazi ama ndugu wa karibu anayeweza kuwa wa msaada kwako.
Lakini watu wa aina hii ni wengi sana ndani ya jamii yetu na inaonekana wamepitiwa hata na maneno ya wimbo wa Salamu kwa wagonjwa ulioimbwa na Omar Kungubaya miaka ile ya 1970 yasemayo; “…Ajuaye Bwana Mungu kwa mzima kuwa mfu, mgonjwa kuwa salama…”
Binafsi naamini kwamba kila nafsi itaonja mauti, kwa sababu sisi sote ni mavumbi na mavumbini hatuna budi kurejea. Hivyo, mwenzenu siogopi kufa bali nahofia kuishi! Nafsi iliyokufa ina heri kuliko inayoishi. 
Ninachokihofia zaidi ni kwamba nitakuwa katika kundi gani baada ya kufa. Daima wenye hekima humuomba Mungu awaongoze katika haki na kuwaombea wengine washike mwenendo mwema, si ndivyo jamani?
Hii ndiyo sababu iliyonifanya nikikumbuke kibao cha al-marhum Freddie Ndala Kasheba ‘Supreme’ alichokiimba mwaka 1982 akiwa na Orchestra Safari Sound ‘wana-Dukuduku’ kisemacho Dunia Msongamano; “…Mawazo yamenijia leo, Ya Mzee wangu alokuwa akisema, Dunia ni msongamano wa watu wenye akili tofauti, Ukitaka kuishi vema lazima uwe na utulivu, Ukitaka kuishi vema fikiri kabla ya kujibu, Jifunze kwa walimwengu, na walimwengu wajifunze kwako, Dunia ni kuona mambo, Na halafu kuyasahau…”
Ni kweli kabisa, dunia ni msongamano kwa sababu imejaa watu wengi wenye mawazo tofauti kama hawa waheshimiwa, ambao wanadhani kwamba mtu akiugua basi atakufa tu, tena yawezekana kabisa wakawa wamempangia siku, saa na namna kifo chake kitakavyokuwa.
Watu wa aina hii tunawashuhudia jamani, hawaendi kuwaona wagonjwa mpaka kwanza waulizie; “Anaumwa nini?” “Vipi amekonda?” “Sijui kama atapona, hivi umemuona Danny alivyo? Na ule wembamba wake kabaki kama chelewa?” Basi hukumu hizi na nyingine nyingi ndizo hutawala mawazo ya watu hawa, na hata pale wanapokuwa wanakwenda kuwatazama wagonjwa huwa ni kama maigizo fulani tu kwao, yaani kana kwamba wamekwenda kuthibitisha hisia zao kwamba watu hao hawatapona! Utadhani wao ni maswahiba wa Mungu na wanajua mipango yake!
Kweli naamini maneno ya Kasheba; “…Dunia msongamano, Kasema baba, Nimeyaona leo nakubali mie, Wengine hupendelea kufurahia, Wanaposiikia fulani kafa, Kufa kwa binadamu hupangwa na Mungu, Namuomba Mwenye Enzi anipe maisha eeh.”
Wapo watu mabingwa wa kupima homa kwa viganja! Wakatimwingine joto la mwili linaweza kuwa kwa sababu ya jua, lakini watasema ‘unaumwa malaria’! Wanatumia darubini za macho!
Hebu burudikeni na kibao hiki, lakini kusema kweli nahitaji sana mchango wenu katika mada hii.

AAhhhh DUNIA MSONGAMANO
Mawazo yamenijia leo,
Ya Mzee wangu alokuwa akisema,
Dunia ni msongamano wa watu wenye akili tofauti,
Ukitaka kuishi vema lazima uwe na utulivu,

Ukitaka kuishi vema fikiri kabla ya kujibu,
Jifunze kwa walimwengu, na walimwengu wajifunze kwako,
Dunia ni kuona mambo,
Na halafu kuyasahau

Kibwagizo:
Dunia msongamano,
Kasema baba,
Nimeyaona leo nakubali mie,

Wengine hupendelea kufurahia,
Wanaposiikia fulani kafa,
Kufa kwa binadamu hupangwa na Mungu,
Namuomba Mwenye Enzi anipe maisha eeh


NI KILA JUMAPILI USIKOSE KUPITIA WAVUTI HII YA www.brotherdanny.com KWA UCHAMBUZI WA MUZIKI. LAKINI TEMBELEA WAVUTI HII KILA SIKU KWA HABARI MBALIMBALI ZA KISIASA, KIJAMII NA MICHEZO ZIKIWEMO KUMBUKUMBU MBALIMBALI. UNAWEZA KUWASILIANA NAMI KWA SIMU/WHATSAPP/TELEGRAM 0656 331 974.

No comments:

Post a Comment