Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 26 May 2015

LOWASSA ASEMA, NINGEBAKI KWENYE UWAZIRI MKUU NINGEPUNGA TU MKONO NA KUZOA KURA ZOTE!

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, nyumbani kwake, Dodoma Jumatatu, Mei 25, 2015. Picha na Edwin Mjwahuzi wa Mwananchi.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyayi Lowassa amesema kama angalikuwa Waziri Mkuu mpaka sasa, na kwa kasi waliyokuwa wanakwenda nayo baada ya awamu ya nne kuingia madarakani, asingepiga kampeni mwaka huu bali angepunga mkono tu na kuzoa kura zote.

Akizungumza na wanahabari nyumbani kwake mjini Dodoma Jumatatu Mei 25, 2015, Lowassa alisema anaamini kasi waliyoanza nayo katika awamu ya nne ilikuwa kubwa na kwamba kero nyingi za wananchi zingekuwa zimepungua kwa kiasi kikubwa, hivyo kuwa rahisi kwake kuzoa kura nyingi.
"Naomba nisimalize uhondo wa Jumamosi, lakini niseme tu kwamba kwa kasi ile tuliyokuwa nayo, kama ningekuwa bado madarakani, ningepita tu mitaani na kupungua mkono na kuzoa kura zote," alisema.
Lowassa, ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM) alisema hana mpango wa kuhama chama nhicho na ikiwa kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama yeye.
Lowassa, ambaye Jumamosi Mei 30, 2015 anatarajia kutangaza rasmi nia yake ya kugombea urais kupitia CCM mjini Arusha, alisema: “Sina mpango wa kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu nimemaliza Chuo Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM. Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi.”
Kuhusu sakata la Richmond, ambalo lilimfanya ajiuzulu uwaziri mkuu, Lowassa alisema tatizo kubwa halikuwa kuhusu mitambo hiyo ya umeme ila uwaziri mkuu.
“Ajenda haikuwa kuhusu Richmond, ila uwaziri mkuu ndiyo maana niliwaachia. Tunajifunza  nini katika hilo, wakubwa wawili wa Marekani, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje (Hillary) Clinton na Rais wake (Barack) Obama, wote wamekuja Tanzania na wamethibitisha kuwa ile mitambo ni mizuri. Lakini jingine tulilojifunza katika ubishi ule umeisababisha nchi hasara ya Dola 120 milioni,” alisema Lowassa.
“Moja ya ushauri wangu wakati ule ilikuwa ni kutaka kuvunja mkataba wa Richmond nikaita wataalamu, nikawaelezea kuhusu habari za magazeti kuwa zinasema hawa jamaa (Richmond) hawana fedha, hebu angalieni, nikaita wataalamu na mwanasheria mkuu, nikawaambia kuna hii habari kuweni makini, pamoja na hayo nikaweka kwa maandishi kwa mwanasheria mkuu, pia kulikuwa na timu ya mashauriano ya Serikali iliyokuwa chini ya makatibu wakuu nao walikuwa na vikao vyao, ilikuwa inaongozwa na (Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Gray Mgonja) nao wakakutana chini ya Katibu Mkuu Kiongozi na baada ya kukutana wakatoa uamuzi ambao sina haja ya kuujadili. Lakini ubishi ule umetugharimu Dola 120 milioni.
“Nilipotaka mkataba uvunjwe nilikuwa nimetoa uzoefu wangu kwani kabla ya kuwa waziri mkuu nilikuwa nimekuwa waziri wa maji na mifugo ambako nilivunja mkataba wa kampuni ya Kiingereza iliyokuwa imewekeza katika mradi wa maji Dar es Salaam ya City Water.
“Chini ya uongozi wa Rais (Benjamin) Mkapa tukagundua hawa jamaa (City Water) ni matapeli…tulifanya kikao saa tisa alasiri, tukachukua kibali cha kumkamata yule Mzungu wa City Water na tukamfukuza akaondoka siku hiyohiyo kwa ndege kurudi kwao, tulifanya saa tisa alasiri ili asiende mahakamani kupata zuio, kwa hiyo tulivizia muda huo ili asije kwenda kupata zuio.
Nini tofauti ya Lowassa nje ya Serikali na ambaye angeendelea kuwa waziri mkuu na kisha kugombea urais? “…Naamini kuwa kama tungeanza kwa kasi ile tuliyoanza nayo nikiwa waziri mkuu, sasa ningepita napunga mkono ningepata kura zote… lakini kinachonisikitisha tumekuwa hatufanyi maamuzi magumu au rahisi, kila kitu kinakwenda legelege. Rais amefanya jitihada kubwa, lakini kuna mambo katika nchi hayaendi, matokeo yake Uganda, Kenya na Rwanda zinatupita sasa, haifai, lakini nawaachia uhondo nitaelezea vizuri Jumamosi, Arusha.”
Alipoulizwa ana utajiri kiasi gani na fedha anazochangia kwenye harambee makanisani na misikitini zinatoka wapi, Lowassa alisema anatamani angekuwa tajiri, lakini anachukia umaskini.
“Tatizo siku hizi kuna maneno mengi, kila nyumba nzuri wanasema ya Lowassa. Mimi nina nyumba chache na ng’ombe kati ya 800 na 1,000. Kwetu Umasaini unapokuwa kiongozi unapewa ng’ombe ili usipate taabu kwa ajili ya kuwakarimu wageni wanapokuja wala usiwe ombaomba au usichukue rushwa. Lakini kama kuna mtu mwenye shaka na utajiri wangu aende Sekretarieti ya Maadili kule ataona kila kitu,” alisema.
“Nachukia umaskini, napenda utajiri, natafuta uongozi wa nchi hii ili kuwasaidia Watanzania kuwa matajiri na si kukumbatia umaskini. Hii kudanganya watu kwamba nikiwa maskini ndiyo nafaa kuwa kiongozi ni ujinga ambao inabidi tuuache. Nataka watu wawe matajiri, tuache kuwabeza matajiri, matajiri wawe ni mfano kwa wengine, watu kama (Reginald) Mengi, (Said) Bakhressa na (Nazir) Karamagi wanatakiwa kuwa mfano kwa wengine, tungekuwa na watu kama hawa 20,000, nchi hii ingekuwa haikopi nje. Naukataa umaskini na nauchukia umaskini. Nakataa umaskini na ninataka watu wanihukumu kwa hilo,” alisema.
Kuhusu kushiriki harambee nyingi na anakopata fedha alisema: “Sina fedha ila nina marafiki wengi, nikipata mwaliko wa kuchangia nawatafuta marafiki zangu wanachanga. Mfano ‘juzi’ nilipomwakilisha Makamu wa Rais mjini Arusha, marafiki zangu walichangia Sh100 milioni, Makamu wa Rais alichangia Sh10 milioni na watu wa Arusha wakatoa Sh100 milioni. Hizo hazikuwa fedha zangu, ila ni watu walichangia. Nafurahia kufanya harambee, harambee zangu zinasaidia misikiti, makanisa na shule, hivi ni vitu vya maendeleo ya watu, nawashauri na wabunge wafanye hivyo kwenye majimbo yao. Hata shule za kata zilichangiwa kwa harambee, tusionee aibu ni jambo jema,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment