Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 29 May 2015

SIKU 6 ZA KISHINDO URAIS CCM!



NA RESTUTA JAMES
 Zikiwa zimebaki siku sita kabla ya kuanza kwa mchakato wa uchukuaji fomu za urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), makada wanaotajwa na ambao wameonyesha nia ya kuwania mafasi hiyo, wameanza kupigana vikumbo kutangaza nia na kueleza sababu za wao kuomba nafasi hiyo.

 
Mshikemshike wa harakati hizo utaanza kutikisa kuanzia Jumamosi hii na hali itakwenda hivyo kwa wiki kadhaa kutokana na wale watakaotangaza nia na kuanza kuchukua fomu.
 
Makada kadhaa wa CCM wanaotajwa kutaka kuwania urais kupitia chama hicho jana walizungumza na NIPASHE kwa nyakati na kuelezea kuhusu suala hilo.
 
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, alisema anakusudia kutangaza nia ya kuwania urais Jumapili hii, jijini Mwanza.
 
“Karibu Mwanza ndipo nitakapotangazia nia na hapo pia nitasema ni lini nitaenda kuchukua fomu,” alisema.
 
Kada mwingine mkongwe ambaye atatangaza nia wiki ijayo ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye aliliambia NIPASHE kuwa atafanya hivyo Jumanne ijayo, jijini Dar es Salaam.
 
“Nitatangaza nia tarehe mbili, saa 5:00 Hyatt Kempisk na nitachukua fomu tarehe 4, Dodoma,” alisema.
 
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, aliomba muda wa saa 24 ili afanye maamuzi sahihi baada ya kuzungumza na mama yake mzazi.
 
“Naomba unipe saa 24 ili niongee kwanza na mama; nataka niongee na mama usiku huu ili nione kama baraka zake bado zipo halafu unipigie kesho nitakuwa na jibu kama nitachukua fomu au la,” alisema.
 
Alisema ana amini baraka za wazazi ni muhimu katika kuwania nafasi hiyo kubwa hivyo ni lazima amshirikishe kabla hajachukua hatua yoyote.
 
Naye Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamis Kigwangalah, aliiambia NIPASHE kwamba bado hajapanga siku ya kuchukua fomu lakini nia yake ya kuwania kiti hicho bado ipo pale pale.
 
Alisema Jumatatu Juni Mosi, mwaka huu atazungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma ambako pamoja na mambo mengine atazindua kitabu chake kinachoeleza vipaumbele vyake.
 
“Bado sijapanga siku ya kuchukua fomu ila Jumatatu nitazungumza na waandishi wa habari, siyo kutangaza nia lakini ninazindua kitabu, ninaelezea vipaumbele vyangu halafu nitathibitisha nia yangu kwamba iko imara na naamini nitakuwa nimefikia muafaka wa ni lini nitachukua fomu,” alisema.
 
Alisema katika mkutano huo pia atajibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari kuhusu vipaumbele vyake ikiwa atachaguliwa kupata wadhifa huo.
 
“Kwenye mkutano huo nitafafanua kipaumbele changu kikuu cha ajira kwanza, cha pili cha kutoa huduma za kijamii zilizo bora na za uhakika, cha tatu utawala bora na namna vinavyohusiana na Tanzania tuitakayo,” alisema.
 
Naye Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema akiwa tayari kutangaza nia na kuchukua fomu ‘atatoa taarifa’ na kwamba kila mgombea ana ratiba yake kuhusu kinyang’anyiro hicho.
 
“Bosi wangu hebu subiri kwanza, mimi sitatangaza kwa siri nitawaambia; kwa hiyo nikiwa tayari nitawaambia,” alisema Dk. Nchimbi alipoulizwa ni lini atatangaza nia au kuchukua fomu.
 
Wakati makada hao wakijipanga kutangaza nia hiyo, taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii zinaeleza kuwa kada mwingine ambaye ameshajitangaza kujitosa kwenye urais, Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuzungumzia uamuzi huo Jumapili hii.
 
Taarifa hizo zinaeleza kuwa Nchemba atatangaza nia na kueleza tarehe ambayo atachukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
 
Makada hao watafuatiwa na mtoto wa baba wa Taifa, Charles Makongoro Nyerere, ambaye amepanga kutangaza nia kijijini Mwitongo, Butiama, Jumatatu wiki ijayo Juni Mosi.
 
Mwingine atakayetangaza nia Jumatatu Juni Mosi ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya ambaye pia atachukua fomu mjini Dodoma Jumatano ijayo Juni 3.
 
Wengine waliotangaza nia na wanaotajwa kuteuliwa na CCM kuwania urais ni kada mkongwe wa chama hicho, Amina Salum Ali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na  Prof. Sospiter Muhongo.
 
Hata hivyo, makada hao watatanguliwa na kada mwingine ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, ambaye amepanga kutangaza nia ya kuwania urais Jumamosi hii katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
 
Lowassa amepanga kutangaza nia hiyo na mkutano wake wa siku hiyo utarushwa moja kwa moja na televisheni na radio kadhaa nchini.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment