Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 31 May 2015

MATOKEO YA AJABU: ORODHA NNE ZAIVURUGA SIMBA, SAID SUED ‘SCUD’ AIBOMOA MSIMBAZI

Kikosi cha Simba cha mwaka 1991. Kutoka kushoto waliosimama: Mackenzie Ramadhan, Issa Kihange, Bakari Idd, Hassan Banda, Jamhuri Kihwelo 'Julio', Itutu Kigi 'Road Master', Zamoyoni Mogella 'Golden Boy', Twaha Hamidu, Mavumbi Omari, ...., Meneja Abdul Yussuf Hazali.
Waliochuchumaa: Ayoub Mzee 'Giant Killer', Hassan Affif, Method Mogella 'Fundi', Ally Machella, Raphael Paul 'RP', Khalfan Ngassa, Idd Pazi 'Father' na mmoja wa wanachama wa klabu hiyo. (Nisahihisheni kama nimekosea).

Na Daniel Mbega

LIGI ya Tanzania Bara ilianza rasmi Januari 26 na kumalizika Septemba 21, 1991. Kwa kweli ilikuwa ligi ngumu lakini hatma ya yote ilikuwa Yanga kutwaa ubingwa huo uliokuwa ukishikiliwa na watani wao wa jadi, Simba, ambayo ndiyo iliyoinyang'anya Yanga ubingwa mwaka 1990.
Baada ya kufanya usajili mzuri ambao ulikuwa kama wa kuziba mapengo, Simba ilionekana kujizatiti huku ikiwa na makocha wanne na meneja mpya wa timu, Azim Dewji.
Simba ilicheza mechi kadhaa za majaribio, ambapo ilipoteza mechi mbili tu ilipofungwa na Timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes 1-0 na kufungwa na Pilsner 2-1 katika Kombe la JATA.
Katika mafanikio yake ya mechi za majaribio, Simba iliweza kushinda mechi zote tatu ilizocheza katika ziara yake ya Kanda ya Ziwa na ilitoka sare na KCC ya Uganda 1-1, kabla ya kuishindilia Pilsner 4-0 na pia kuzifunga Kikwajuni 2-0 na MECCO 3-0 katika Uwanja wa Karume halafu ikaenda Zanzibar ambako iliichapa tena Kikwajuni 3-0 na kutoka sare ya 1-1 na mabingwa wa zamani wa Muungano, Malindi.
Kwa upande wa Yanga, nayo ilifanya usajili ambao ulilenga katika kuwa na wachezaji chipukizi wanaoujua mpira badala ya kufuata majina. Pia ilikuwa imepata uongozi mpya na Mkurugenzi mpya katika juhudi zake za kutaka kufanya vizuri msimu huo.
Katika mechi zote za majaribio ambazo Yanga ilicheza, ilifungwa mechi moja tu na Uganda Cranes kwa magoli 2-1. Baada ya hapo ilianza mtindo wa kushinda na kutoka sare na kubeba vikombe viwili.
Katika michezo yake mingine ya kujipima nguvu baada ya kufungwa na Waganda, Yanga ilifungana 1-1 na Reli na ikafungana pia 1-1 na KCC mjini Dar es Salaam kabla ya kwenda Tanga ambako iliifunga African Sports 3-1 na kutoka suluhu na Coastal Union.
Katika mechi za kugombe Kombe la JATA, Yanga iliitoa Reli na kuingia fainali ambako iliifunga Pilsner 2-1 na kutwaa kombe hilo. Halafu katika mashindano ya Kombe la Mfuko wa Pemba ambayo yalifanyika Zanzibar, Yanga iliifunga Small Simba 2-1 na kuingia fainali ambako iliifunga Malindi 1-0 na kutwaa kombe hilo.
Katika mechi nyingine ambazo Yanga ilicheza mjini Dar es Salaam iliweza kuzifunga Kikwajuni 2-1, MECCO 4-0 na Small Simba 2-0. Pia iliifunga tena Reli 2-1 mjini Morogoro.
Sasa Yanga na Simba walikuwa wanapambana Jumamosi Mei 18, 1991 kuwania pointi tatu za mechi ya duru la kwanza la Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Timu ya Yanga ilikuwa imejichimbia huko Zanzibar kwa wiki nzima, ambako ilicheza mechi tatu za kirafiki na kupata ushindi mara mbili na kupoteza moja. Simba kwa upande wake ilikuwa imepiga kambi Jijini Dar es Salaam katika maeneo ya Chuo Kikuu (Mlimani), ambako ilikumbwa na mkasa wa kuibiwa jezi katika mazingira yasiyojulikana.
Vinginevyo pambano hilo lilikuwa likizungumziwa kwa mapana na marefu na hata Waziri anayehusika na Michezo, Elimu na Utamaduni, Charles Kabeho, alifikia kushirikishwa katika suala la kiingilio.
Yanga ilikuwa na wachezaji wapatao saba katika mechi hiyo ambao hawakuwepo katika mechi ya mwisho na Simba mwaka 1990, nao ni golikipa Stephen Casmir Nemes, mabeki Selemani Mkati, Willy Mtendawema, na washambuliaji John Mngazija na Said Sued 'Scud', winga Abubakar Salum 'Sure Boy' na mchezaji wa kiungo Issa Athumani Mgaya 'Amiri Jeshi', ambaye hata hivyo, alikuwa analalamikiwa na Simba na kulikuwa na wasiwasi kama angechezeshwa.
Nemes, Mkati na Mngazija waliwahi kucheza dhidi ya Simba wakiwa katika timu nyingine msimu wa 1990, wakati Abubakar Salum aliwahi kucheza dhidi ya Simba akiwa na Yanga kwenye miaka ya nyuma kabla ya kwenda kuichezea AFC Leopards ya Kenya.
Wachezaji ambao hawakuwepo kwenye kikosi hicho, lakini walikuwepo kwenye kikosi cha Oktoba 20,1990 kilichoifunga Simba, ni Makumbi Juma Baruani 'Homa ya Jiji' aliyeachwa kwenye usajili na Joseph Machella aliyezuiwa na FAT kutokana na usajili wake kuwa na utata.
Kwa upande wa Simba, wachezaji wapya walikuwa golikipa wa zamani wa timu hiyo Idd Pazi 'Father', Issa Kihange, Bakari Iddi, Jamhuri Kihwelu, Khalfan Ngassa, Gebo Peter na Azizi Nyoni. Wote hao walikwishacheza dhidi ya Yanga wakiwa katika timu nyingine msimu wa 1990. Gebo alikuwa mwiba mkali kwa Yanga alipokuwa akiichezea Sigara, na siku hiyo alitarajiwa kufanya maajabu mengine.
Siku moja kabla ya mchezo, Kaimu Katibu Mkuu wa FAT, Msafiri Mekelemi, alikuwa amesema kwamba, mipango yote kuhusu pambano hilo ilikuwa imekamilika na tiketi zilianza kuuzwa kuanzia saa 3.00 asubuhi pamoja na kuwepo ulinzi wa kutosha.
Wakati timu hizo zinapambana siku hiyo, Yanga ilikuwa ikiongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 18 kutokana na mechi 14 ilizocheza ikiwa imeshinda sita, kutoka sare sita na kupoteza mbili. Simba ilikuwa ikishikilia nafasi ya nne ikiwa na pointi 16 nyuma ya Coastal Union na Tukuyu Stars zilizokuwa na pointi 17 kila moja. Hata hivyo, Simba ilikuwa imecheza mechi 12, kushinda tano, kutoka sare sita na kupoteza moja.
Mtabiri mmoja mashuhuri wa Dar es Salaam, Dk. Philip Kajula, alikuwa ametabiri tangu Mei 15 kwamba, Simba ingeifunga Yanga magoli 3-0. Hivyo, mashabiki wengi wa Simba walikuwa wamemiminika kushuhudia timu yao ikishinda kama ilivyokuwa imetabiriwa.

Ilivyokuwa mechi yenyewe Mei 18, 1991
Siku hiyo Yanga waliruka seng'enge tena na kufaulu kuwalaza wapinzani wao wakubwa wa soka nchini Tanzania, Simba, ambao wakati huo walikuwa wanajiita 'Taifa Kubwa' tokea walipotwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mapema mwaka huo wa 1991.
Yanga, ambao wakati huo walikuwa wakijiita 'Umoja wa Mataifa', waliwafunga Simba karibu kwa muda ule ule ambao mwezi Mei, mwaka 1990 walifungwa. Said Sued, maarufu kwa jina la Scud, alifunga goli pekee na la ushindi kwa Yanga katika dakika ya saba, dakika moja zaidi kwa muda ambao Mei 26, 1990 Mavumbi Omari aliifungia Simba goli la ushindi (katika dakika ya sita). Hilo lilikuwa goli la tatu kwa Sued msimu huo.
Yanga ilitokea Zanzibar kwa mazoezi ya wiki moja na kuruka seng'enge na kisha kutandaza kandanda la hali ya juu ambalo ilikuwa haijapata kulionyesha kwenye Uwanja wa Taifa katika mechi zake zilizotangulia na kuwazidi Simba katika kila hali ya uchezaji.
Wakati wa pambano la mwisho la mwaka 1990, Yanga iliishinda Simba magoli 3-1 baada ya kupenya kwenye tundu la seng'enge.
Issa Athumani, akicheza mechi yake ya kwanza baada ya kurejea nyumbani kutokana na mkataba wake kufutwa huko Uarabuni katika klabu ya Nad Oman SC, ndiye aliyetoa mchango mkubwa katika goli la ushindi la Yanga.
Issa alimtoka bega Method Mogella 'Fundi' aliyekuwa amembana na kutoa krosi iliyomkuta Sued akiwa kwenye nafasi nzuri kushoto mwa goli la kusini, ambaye aliachia kwa utulivu kiki kali ya chini chini iliyojaa wavuni huku kipa nambari wani wa Tanzania, Iddi Pazi, akiwa amepotea maboya.
Makosa yaliyofanywa na mabeki wa Simba mpaka goli hilo likapatikana ni kule kumfuata Issa wote na kumwacha Sued peke yake. Mpira wa krosi ya Issa uliwapita kwa karibu mabeki kadhaa wa Simba kabla haujamfikia Sued, ambaye hakuwa na papara ya kuupiga ovyo.
Yanga waliutawala kabisa mchezo huo katika dakika zote 45 za kipindi cha kwanza, ambapo kipa wa pili wa Taifa, Stephen Nemes, hakuwa na kazi kubwa na mara nyingi alidaka mipira ya kurudishiwa na mabeki wake au mashuti ya mbali ya washambuliaji wa Simba. Mara nyingi sentahafu wa Yanga, Salum Kabunda 'Ninja', alikuwa akibakia peke yake nyuma kumlinda Nemes bila madhara ya kutisha.
Issa na Sued, ambao walikuwa wakicheza kwenye nambari 10 na 9, walikuwa miiba katika ngome ya Simba, ambayo ilikuwa ikiongozwa na Method pamoja na akina Raphael Paul 'RP', Twaha Hamidu, Frank Kassanga 'Bwalya' na baadaye Jamhuri Kihwelu 'Mrema'.
Simba iliingia uwanjani kuanza kipindi cha pili ikiwa na maarifa mapya, ambapo iliamua kucheza mtindo wa mtu-na-mtu, ambao kwa namna fulani uliwasumbua wachezaji wa Yanga, ambao walianza kupoteana na kuelekea kuwa Simba ingeweza kusawazisha goli hilo wakati wowote ule na washambuliaji hatari wawili wa Simba, Zamoyoni Mogella na Hamisi Gaga 'Gagarino' walicharuka kuelekea kwa Nemes mara kwa mara, lakini mabeki wa Yanga walikaa imara kuondoa hatari hizo na kusababisha kona kadhaa ambazo hazikuzaa matunda.
Hata hivyo, Yanga walifurika tena katika dakika 10 za mwisho na kulitia jamba jamba lango la Simba hadi dakika ya mwisho, huku giza likiwa limeanza kutanda uwanjani, kwani mechi ilichelewa kuanza kutokana na Yanga kuchelewa kuingia uwanjani.
Ingawa uchezeshaji ulikuwa mzuri kwa ujumla, lakini jambo moja la ajabu lililotokea ni kwamba, mwamuzi Taji Bakari kutoka Dodoma, na mshika kibendera wake wa mstari wa kwanza, Joseph Mapunda wa Songea, walikuwa hawaelewani mara kadhaa, licha ya kuwa walikuwa wakichezesha pamoja mechi za kimataifa kwa miaka mingi nyuma.
Kuna wakati Mapunda alinyoosha kibendera cha kuotea kwa upande wa Simba, lakini Taji alimwacha Mogella aelekee golini mpaka Nemes akaunyakua mpira huo. Halafu mara mbili Taji alimkatisha Mapunda upande wa kutupa mpira; kwanza Mapunda alikuwa amenyoosha kibendera mpira utupwe kuelekea Simba, lakini Taji akaelekeza Yanga, halafu wakati mwingine tena kuelekea na mwisho wa mchezo, Mapunda alinyoosha kiendera mpira utupwe kuelekea Yanga, lakini Taji akaelekeza Simba.

Shaffi Bora aonyesha vidole vitatu, njiwa ashindwa kuruka
Kama ilivyo kawaida ya mechi za Simba na Yanga, siku hiyo pia vilikuwepo vituko vingi kabla ya pambano hilo la watani wa jadi katika Uwanja wa Taifa. Pamoja na rabsha rabsha zilizojitokeza kuhusu mahali tiketi zilipokuwa zinauzwa, lakini baadaye watu wengi walijazana katika uwanja huo kuanzia mapema siku hiyo, na kwa vile watu hukaa muda mrefu uwanjani siku ya mechi hiyo kubwa kabla ya jioni kufika, basi vituko vingi hutokea hapa na pale.
Lakini mashabiki waliokuwa na makeke zaidi walikuwa wa Simba, ambao ni kawaida yao kuwazidi Yanga kwa mbwembwe uwanjani. Mashabiki wa Simba walikuwa na bendera, ambapo bendera mbili kubwa zilikuwa na maandishi ya SIMBA TAIFA KUBWA.
Timu ya Simba iliingia uwanjani saa 9.35 katika msafara wa magari nane, ambapo njiwa aliyekuwa katika gari la wachezaji, alitolewa na kurushwa, lakini njiwa huyo mweupe alishindwa kuruka mara mbili na kujibanza katika mlingoti wa umeme na kutoweka baadaye wakati mechi inachezwa huku Yanga ikiongoza kwa goli 1-0.
Kabla ya timu ya Simba kuingia, Mkurugenzi wa timu hiyo, Shaffi Bora, aliingia uwanjani kwa makeke akiwa katika gari la kifahari aina ya Mercedes Benz likiendeshwa na mdogo wake, Ahmed Bora. Shaffi alipokuwa katika gari hilo alionyesha vidole vitatu na kushangiliwa na mashabiki wa Simba, pengine alikuwa akimaanisha 'magoli matatu' dhidi ya Yanga.
Yanga waliingia uwanjani saa 10.02 pia kwa mbwembwe, ambapo wachezaji na viongozi waliruka waya wa seng'enge upande wa kusini. Aliyetangulia kuruka alikuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Syllersaid Mziray. Halafu walifuatia wachezaji na viongozi, akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi ya Yanga, Mohammed Fazal Viran 'Babu'.
Wachezaji wa Yanga walikimbia kuuzunguka uwanja na Mziray alikatisha katikati, ambako wachezaji wa Simba walikuwa wamekatisha kuja kwenye vyumba vya kukaguliwa. Wakati wachezaji wa Yanga walipokuwa wakielekea kwenye vyumba vya kukaguliwa baada ya kukimbia kuzunguka uwanja, wachezaji wa Simba walichomoka kutoka vyumbani kuelekea uwanjani na lango la kuingilia ndilo lilikuwa njia panda, ambako walipishania huku mashabiki wakishangilia.

Kajura aeleza utabiri ulivyoharibika
Mtabiri mashuhuri wa nyota Jijini Dar es Salaam, Dk. Philip Kajura, alisema baada ya mechi kuwa, utabiri wake aliutoa mapema mno kiasi kwamba watu wengine walianza kutia changamoto ili aonekane hajui.
Kajura, aliyetabiri tangu Jumatano, Mei 15 kuwa Simba ingeifunga Yanga Mei 18 kwa sababu nyota yake ilikuwa kali sana siku hiyo, alisema bila shaka kuna watu ambao walimwingilia ili kumvurugia utabiri wake.
"Utakumbuka kwamba, hapa katikati kulikuwa na siku tatu nzima, ndiyo maana wengine nao walijitokeza kutabiri tofauti ili wanipe changamoto," alisema Kajura Jumapili, Mei 19 alipokuwa akihojiwa kwenye hoteli ya Internationale ya Mnazi Mmoja alikokuwa akiishi. Alipoulizwa kama alikuwa anajisikia vibaya kutokana na utabiri wake kuharibika, Kajura alisema hajisikii vibaya.
Hata hivyo, mara baada ya mechi hiyo, mashabiki kadhaa wa Simba walimfuata na kutaka kumpiga kutokana na kuwadanganya, lakini akafanikiwa kuokolewa kwa kujificha hotelini na walinzi wa hoteli hiyo wakakataza mtu yeyote kuingia ndani.
Timu zilipangwa kama ifuatavyo: Yanga: Stephen Nemes, Selemani Mkati/Freddy Felix 'Minziro', Kenneth Mkapa, Godwin Aswile, Salum Kabunda, Jumanne Shango, Abubakar Salum, Athumani China, Said Sued 'Scud', Issa Athumani (nahodha), Sanifu Lazaro.  Kocha: Syllersaid Mziray.
Simba: Iddi Pazi, Raphael Paul, Twaha Hamidu, Method Mogella, Frank Kassanga 'Bwalya', Iddi Selemani, Itutu Kigi/Jamhuri Kihwelu, Khalfan Ngassa, Bakari Iddi/Issa Kihange, Hamisi Gaga, Zamoyoni Mogella. Kocha: Abdallah Kibadeni.

Orodha nne
Kufungwa kwa Simba kulikuja kuelezwa baadaye na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni, kwamba kulitokana na kutokuelewana baina ya viongozi wa timu hiyo katika upangaji wa orodha ya wachezaji ambao wangecheza siku hiyo.
Kwa kawaida kocha ndiye mwenye jukumu la kupanga wachezaji kwenye mechi kutokana na kuangalia uwezo wao, lakini kwa Simba siku hiyo ilikuwa tofauti kabisa; kocha alikuwa na orodha yake, Mwenyekiti Juma Salum alikuja na orodha yake, Katibu Mkuu Abdul Yusuf Hazali alikuwa na orodha yake na Katibu Mkuu Msaidizi, Hamisi Mapande alikuwa na orodha yake!!!
Orodha ya wachezaji 11 wa kwanza iliyopendekezwa na Mwenyekiti ilikuwa kama ifuatavyo: Iddi Pazi, Raphael Paul, Twaha Hamidu, Method Mogella, Frank Kassanga 'Bwalya', Iddi Selemani, Issa Kihange, Khalfan Ngassa, Zamoyoni Mogella, Malota Soma na Bakari Iddi. Wachezaji wa akiba ni Mackenzie Ramadhani, Mavumbi Omari, Jamhuri Kihwelu, Hassan Affif na Hamisi Gaga au Itutu Kigi.
Orodha iliyopendekezwa na Katibu Mkuu ilikuwa kama ifuatavyo: Pazi, Mavumbi, Twaha, Method, Bwalya, Iddi Selemani, Kihange, Ngassa, Gaga, Zamoyoni na Bakari Iddi, na wachezaji wa akiba ni Mackenzie, Raphael Paul, Jamhuri, Malota na Affif.
Orodha ya Katibu Mkuu Msaidizi ilikuwa kama ifuatavyo: Pazi, Raphael Paul, Twaha, Jamhuri, Bwalya, Iddi Selemani, Kihange, Method, Bakari Iddi, Zamoyoni na Itutu Kigi. Wachezaji wa akiba walikuwa Mackenzie, Mavumbi, Alli Machella na Ayoub Mzee.
Orodha ya makocha ilikuwa: Pazi, Raphael, Twaha, Method, Bwalya, Iddi Selemani, Kihange, Ngassa, Ayoub Mzee, Gaga na Zamoyoni, na wale wa akiba walikuwa Mackenzie, Aziz Nyoni, Jamhuri, Malota na Affif.
Baada ya mjadala mrefu baina ya viongozi na makocha huku kila mmoja akitoa sababu zake za kupanga orodha hiyo hatimaye ikapendekezwa orodha nyingine ya tano, ambapo wachezaji Hassan Affif, Issa Kihange, Ayoub Mzee na Aziz Nyoni walikatwa katika orodha ya makocha na kuingizwa Itutu Kigi, Bakari Iddi na Mavumbi Omari kutoka kwenye orodha ya viongozi, ndipo ikapatikana orodha hiyo hapo juu, ambayo ilionekana uwanjani.
Pamoja na kufanya marekebisho makubwa, Simba ilijikuta ikipokea kipigo kama hicho kutoka kwa Yanga Agosti 31 kwa goli lililofungwa na Said Sued kwa mara nyingine.

WASILIANA NAMI SIMU/WHATSAPP/TELEGRAM 0656 331974


No comments:

Post a Comment