Mangara Tabu Mangara (kulia) na kocha Tambwe Leya (kushoto) wakiwa na kombe la ubingwa wa ligi mwaka 1974. Wengine pichani ni viongozi na wanachama wa Yanga.
NA DANIEL MBEGA
WENGI
wamekuwa na maelezo tofauti kuhusu chanzo cha mgogoro wa Yanga kilichozaa timu
ya Pan African mwaka 1977. Wapo wanaosema kwamba kupoteza ubingwa wa Afrika
Mashariki na Kati mwaka 1976 ndiko kulikosababisha kutokea mgawanyiko. Lakini
maelezo hayo si sahihi, kwani wakati ubingwa huo unatoweka Jannuari 1976 mjini
Mombasa, Kenya, tayari kulikuwa na mgawanyiko wa Yanga-Raizoni na Yanga-Kandambili,
na zaidi tayari uchaguzi mkuu ulikuwa umefanyika (Desemba 1975) na Mangara Tabu
Mangara kudondoshwa kwenye uchaguzi huo.
Kwanza
kabla ya kuingia kwa undani kuhusu mgogoro huo ni vyema mtu akaielewa kwa
undani historia ya Yanga kuanzia mwaka 1968. Wengi wanasema kwamba Mangara Tabu
ndiye aliyefanikisha ujenzi wa jingo la Yanga la Jangwani. Si kweli! Suala la
ujenzi wa jingo lile lilianza tangu mwaka 1968, kweli, lakini kwanza
lilitanguliwa na uandaaji wa Katiba ya kwanza ya Yanga.
Katiba
hiyo ilianzaliwa na kasha kuchapishwa mwaka huo, lakini ndani yake kulikuwa na
vipengele ambavyo baadaye vikaja kuonekana vinawabana baadhi ya watu. Mojawapo
ya vipengele hivyo ni kile kilichoelezea kuhusu udhamini wa jingo la klabu
lililokuwa linatarajiwa kujengwa, ambacho kilisema kwamba, mdhamini ni lazima
awe na nyumba iliyojengwa kwa usimamizi au utaratibu wa serikali na pia awe na
pato la Shs. 1,500 kwa mwezi.
Rais
wa Yanga wa wakati huo, Kondo Kipwata ndiye aliyestahili sifa zote za maendeleo
ya klabu hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jingo hilo lenye ghorofa tatu,
pamoja na ujenzi wa uwanja wa Kaunda. Vyote hivi vilijengwa kutokana na
michango mbalimbali ya wananchi, serikali (ya Muungano na ile ya Mapinduzi
Zanzibar) na taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Wazo
la ujenzi lilipotolewa Mzee Kondo Kipwata alikuwa na nyumba zake, lakini
kutokana na kutokuwa na hati za kiserikali na kutokuwa na kazi, kipato chake
hakikuwa kile kilichoainishwa kwenye Katiba, hivyo kunuwia vigumu kuwa mmoja wa
wadhamini wa jingo hilo. Wakati huo Makamu wa Rais, Mangara Tabu, alikuwa Mpiga
Chapa Mkuu wa Serikali na kipato chake kwa mwezi kilikuwa Shs. 1,500. Yeye
ndiye aliyeandaa Katiba hiyo na kuichapa, hivyo ilikuwa rahisi kwake kuweka
kipengele hicho.
Lakini
tayari Mangara alikuwa kipingwa na wanachama wengine kama Mathew Kashindye na
David Mwambungu. Hali hiyo ikamfanya Mangara kutafuta njia ya kumwezesha kuwa
mmoja wa wadhamini wa jingo hilo, na kwa vile alikuwa na nyumba Mtaa wa Swahili
na pia alikuwa na kazi ya mashahara, wana-Yanga wakaamua kumweka kuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi.
Hata
Rais Julius Kambarage Nyerere alipotembelea ujenzi huo mwaka 1970 alikuta
Mangara ndiye msimamizi mkuu. Wakati huo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia
klabu ya Wananchi (zamani ikijulikana kama African Sports), chini ya Sheikh
Abeid Amani Karume, ilikuwa imetoa Shs. 2 milioni kwa ajili ya kufanikisha
ujenzi huo. Jiwe la Msingi liliwekwa na Sheikh Karume mwaka 1971.
Pamoja
na hayo, bado kuliendelea kuwepo na migogoro. Mwanzoni mwa mwaka 1973 Mzee
Kondo Kipwata alifariki dunia, na kwa mujibu wa Katiba, Maka wake, Mangara
Tabu, ndiye aliyekaimu nafasi yake. Lakini katika mechi ya kwanza chini yake
dhidi ya Simba mwaka huo 1973, Yanga ilichapwa bao 1-0 na kisha kuvuliwa
ubingwa wa Taifa ilioushikilia kwa miaka mitano mfululizo (1968-1972). Kipigo
kile kikachochea kabisa mgogoro uliokuwa unazidi kukomaa, hivyo wanachama
wakaamua kumshinikiza Mangara kuhakikisha kwamba timu inaandaliwa vya kutosha
kwa ajili ya michuano ya Ubingwa wa Taifa wa mwaka 1974.
Ndipo
mwaka 1974 Yanga ikaendea kuzuru Brazil kwa ajili ya kujiandaa na ligi hiyo
iliyofanyika Mwanza. baada ya kurejea Yanga ilikuwa inatisha na ipoingia
fainali ikakumbana na Simba Agosti 10, ambapo iliweza kushinda kwa mabao 2-1.
Mapema mwaka 1975 ikaivua tena Simba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mjini
Zanzibar kwa kuifunga mabao 2-0.
Pamoja
na mafanikio hayo, bado wanachama waliendelea na mgogoro huo na walionyesha
dhahiri kutokuwa na imani na Mangara hasa kutokana na ikushindwa kujengwa kwa
viti (jukwaa) kwenye uwanja wa Kaunda ingawa wanachama walikuwa wamechangishwa
fedha kwa ajili hiyo. Mpaka leo haijulikani fedha zile ziliingia wapi.
Mangara
alikuwa ametengeneza sefu ya fedha kwenye klabu ya yanga pale Jangwani na
nyingine, kwa mujibu wa waliokuwepo, aliiweka nyumbani kwake. Wachezaji au
wanachama walipokuwa na shida ya fedha walikwenda kupanga foleni pale nyumbani
kwake. Kitendo hicho kilikuwa kinapingwa sana na kocha Tambwe Leya, ambaye
alikuwa akiidhinisha fedha kwa wachezaji wenye matatizo. Wale wanachama
waliokuwa wakimuunga mkono Mangara walikuwa wakijiita ‘Raizoni’, yaani watoto
wa mjini wanaojua kuvaa, na wale wengine waliokuwa wakimpinga walionekana
makabwera tu. Ni katika mgawanyiko huo, ambapo siku moja baada ya timu kumaliza
mazoezi pale Kaunda, wanachama fulani wakamzonga golikipa chipukizi Juma
Pondamali ‘Mensah’ na kuanza kumshambulia kwa maneno, lakini kipa huyo akasema,
‘Yaani hata nyie mnaovaa kandambili mnaweza kusema mbele ya wenye fedha?!’ Hapo
ndipo lilipoanzia neon ‘Yanga Kandambili!’
Wakati
huo Yanga ilikuwa inamiliki magari matano. Kulikuwa na Isuzu iliyokuwa na uwezo
wa kubeba abiria 65, Isuzu nyingine ya kubeba watu 30, Ford ya kubeba watu 35,
Pundamilia Isuzu ya kubeba watu 18, ambayo mara nyingi ilikuwa ikibeba
wachezaji wanapoingia uwanjani, na gari aina ya Honda iliyokuwa ikitumiwa na
kocha Tabwe Leya.
Wakati
Mangara alikuwa kaimu Rais wa klabu, mdogo
wake Mtaruke Mangara alikuwa Makamu wa Rais, Katibu Mkuu alikuwa David
Mwambungu, Katibu Msaidizi alikuwa Mohammed Misanga, Mweka Hazina alikuwa
Ngakonda, Mweka Hazina Msaidizi alikuwa Punzi, Abdul Masoud (mtangazaji wa
Radio Tanzania Dar es Salaam –RTD) alikuwa Katibu Mwenezi na Mathew Kashindye
alikuwa Katibu Mipango.
Lakini
baada ya kutwaa ubingwa kule Nyamagana mwaka 1974 mgogoro ukazidi na wanachama
wakashinikiza uchaguzi ufanyike. Serikali ikaona kwamba hali hiyo ingeweza
kuvuruga Amani nchini hasa katika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwaka 1975,
hivyo ikaamua kuwafungia Mwambungu na Kashindye kutojishughulisha na michezo
maisha.
Tamko
hilo la serikali halikuwakatisha tamaa wanachama, ambapo mwaka 1975 wakaamua
kufanya mapinduzi baridi kwa kuchagua viongizi wa muda uliokuwa chini ya
uenyekiti wa Omar Mussa Chitenje pamoja na Mohammed Misanga (Katibu Mkuu),
Punzi (Mweka Hazina), Edson Mwandemane (Katibu Mipango), na Abdul Masoud
(Katibu Mwenezi). Hatua hiyo ya kufanya mapinduzi baridi ilifuatia kutolewa kwa
Yanga na Enugu Rangers ya Nigeria katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika mnamo
Juni 1975. Katika mchezo wa kwanza huko Lagos timu hizo zilitoka suluhu, lakini
ziliporudiana mjini Dar es Salaam zikafungana 1-1, hivyo Wanigeria wakapata
ushindi wa sheria ya bao la ugenini.
Wanachama
wa Yanga walimtuma Hamad Abdallah Kiluvia kwenda kuipokea timu ya Enugu, ambapo
inasemekana alipewa ‘vitu’ kama mbinu ya ushindi. Alipofika Uwanja wa Ndege
alianza kusalimiana na golikipa wa Enugu, Emmanuel Okala, kipa mrefu sana
ambaye pia alikuwa akiidakia timu ya taifa, Green Eagles, wakati huo.
Lakini
upande wa Mangara inasemekana haukuwa radhi kuona Yanga inashinda, hivyo baadhi
ya waliokuwa wakimuunga mkono wakawashawishi wachezaji wa Yanga wacheze chini
ya kiwango. Wachezaji hao wakasikika wakisema kwamba, siku hiyo ya mchezo
hakuna mtu kufunga goli. Maneno hayo yalitamkwa wakati wako ndani ya gari
wakienda uwanjani siku hiyo ya mchezo, lakini viongozi hawakujua. Hata kocha
Tambwe Leya hakuwa na habari.
Baada
ya kuingia uwanjani, Enugu ndio walianza kupata bao, lakini baadaye Kitwana
Manara akasawazisha, hali iliyosababisha kutokee ugomvi mkubwa hapo uwanjani
baina ya kambi ya Mangara, ambao walikuwa wakilaumu kwa nini Kitwana alifunga
bao hilo. Hata hivyo, matokeo yakabaki 1-1 na Yanga ikawa imetolewa.
Baada
ya wanachama kugundua njama hizo, ndipo walipofanya uchaguzi Julai 1975 na
Mwenyekiti akawa Omar Mussa Chitenje. Hata hivyo, serikali ikaingilia kati na
kusema kwamba uchaguzi huo ulikuwa batili kwa sababu walichofanya wanachama ni
kama kuteua Kamati ya Muda tu kinyume na Katiba. Lakini mgogoro huo
ulipoendelea ikabidi serikali iridhie kufanyika kwa uchaguzi wa Yanga mnamo
Desemba 28, 1975, Jumapili, chini ya usimamizi wa Umoja wa Vijana wa TANU
(TLY). Ndipo kwa mara nyingine akachaguliwa Omar Mussa kuwa Mwenyekiti, Makamu
Mwenyekiti alikuwa Juma Shamte, Katibu Mkuu alikuwa Mohammed Misanga, Katibu
Msaidizi Hassan Lupindo, Katibu Mwenezi Abdul Masoud, Katibu Mipango Kennedy
Kanyanka, Mweka Hazina Kanduru Msusa, Mweka Hazina Msaidizi Edson Mwandemane.
Unaweza
kuona kwamba mpaka wakati huo tayari kulikuwa na makundi mawili; Kundi la
Mangara na kundi la wanachama wengine, wakiwemo na wale waliochaguliwa kushika
uongozi. Lakini kundi la Mangara lilikuwa linaungwa mkono na serikali, ndiyo
maana hata baada ya Yanga kuvuliwa ubingwa wa Afrika Mashariki na kati mjini
Mombasa, Kenya mwaka 1976, baada ya ungozi kupeleka basi la kukodi (UDA-Ikarus
Kumbakumba) kule Uwanja wa Ndege ili kuwapokea wachezaji, wachezaji hao wote
hawakuingia kwenye basi hilo na badala yake wakaingia kwenye magari ya
mawaziri, mkuu wa mkoa, RPC na magari mengineyo ya serikali. Kitendo hicho
kilizidisha hasira za wanachama, ambapo wakaazimia kuwafukuza wote na kuanza
kuunda kikosi kipya.
Serikali
ikatoa amri ya kutoruhusu uandikishwaji wa klabu ya michezo kutokana na
migogoro. Wachezaji wale walioondoka awali walitaka kujiunga na klabu moja pale
Manzese, lakini kutokana na amri hiyo ya serikali, ikabidi watimkie Morogoro
walikojiunga na timu ya Nyota Afrika iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Taifa.
Viongozi
wa serikali waliokuwa nyuma ya Mangara, Mshindo Mkeynge na Shiraz Shariff,
walikuwa Waziri wa Michezo, Utamaduni wa Taifa na Vijana Mrisho Sam Hagai
Sarakikya, Mkuu wa Mkoa wa Pwani (wakati huo) Clement Rwegasira, Katibu Mkuu wa
Rais Sammy Mdee, Mkurugenzi wa Radio Tanzania Dar es Salaam Paul Andrea
Sozigwa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani (Dar) Ismail Lazaro, ambao waliona
Mangara alikuwa ameonewa tu na wanachama hao.
Baada
ya kutimuliwa kwa wachezaji hao, Yanga haikuwa na kikosi kibaya sana, ingawa
mwaka huo 1976 walifungwa na Simba 2-1. Hali hiyo ikawashangaza hata wapinzani
wao, na hata serikali nayo ikachanganyikiwa kuona timu iliyokuwa na migogoro
mingi kama Yanga iliweza kuunda kikosi imara katika muda mfupi. Hii ilitokana
na kuwa na kocha mzuri, Tambwe Leya, ambaye aliamini vijana ndio walikuwa nguzo
imara.
Ndipo
likatolewa agizo la kuwataka Tambwe Leya na kocha wa Simba wa wakati huo, Nabby
Camara kutoka Guinea, kuondoka nchini haraka sana kwa madai kwamba walikuwa
makachero wa Shirika la Kijasusi la Marekani (Central Intelligence Agency –
CIA). Mwaka 1977 ndipo ikazaliwa Pan African baada ya wachezaji wale kurejea
kutoka Morogoro na pia ndio mwaka ambao Yanga ilichabangwa na Simba mabao 6-0.
Daniel mbega ni
mwandishi mwandamizi wa habari za uchunguzi na mtafiti ambaye anapatikana kwa
simu/whatsapp/telegram 0656 331974. Hii ni sehemu ya muswada wake wa HISTORIA
YA YANGA.

No comments:
Post a Comment