Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema
MWENYEKITI wa Chama cha TLP, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo mkoani Kilimanjaro, Dkt. Agustino Mrema amesema hakuna kiongozi wala kijana yeyote atakayemng'oa kwenye kiti chake cha ubunge.
Kwa madai kuwa, kazi ya ubunge si kubeba zege bali ni kuwatumikia wananchi.
Akizungumza hayo jana Dar es Salaam,Mrema alisema bado wananchi wa jimbo lake wanamhitaji kuwatetea haki zao hivyo kwa wale wanaosema yeye ni mzee wakae wakijua atagombea kwa matakwa ya wananchi wake.
Alisema, masuala ya kutetea wananchi si kazi inayofanywa na kila mtu; bali ni ushupavu wa kujitoa kusaidia matatizo mbalimbali wanayokabiliana nayo.
"Mtu anayeniambia mimi ni mzee, mimi sibebi zege, bali ubunge ni kuwakilisha watu na kuwatumikia ipasavyo, nina miaka 71 hivyo mimi bado dogodogo...sitaki watu wanisingizie watakaoniona mimi ni mzee waniache, wananchi wangu wa Vunjo bado wananihitaji," alisema.
Alisema, mwaka 1995 aliwahi kumpeleka,Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia kugombea kwa heshima yake ambapo wananchi walimpa ubunge wa Vunjo kwa muda wa miaka mitano na ilipofika mwaka 2000 wananchi walimkataa hivyo jamii iondoe mitazamo isiyofaha ya kusema mtu akiwa kijana anaweza kutumikia wananchi hiyo si hoja.
"Mimi nimekuwa Mbunge wa Moshi Vijijini miaka 10, nilienda Temeke nikapata nikarudi Vunjo nikapata, hakuna mtu wa kunitoa mimi katika jimbo langu," alisema Mrema.
Akizungumzia juu ya afya yake, Mrema alisema watu walimzushia kuwa yeye ana maambukizo ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) jambo ambalo si kweli, kwani anaugua kisukari tangu mwaka 1982 ambapo Rais Jakaya Kikwete aliweza kumsaidia kumpeleka India mwaka 2009.
Alisema, cheti chake kinaonyesha yeye kapona kwani tayari ameshapimwa na kugundulika amepona na afya yake imeanza kuwa nzuri si kama zamani, hivyo watu wanaosema kuwa afya haimruhusu kugombea ubunge wamekosea, watafute hoja nyingine.
CREDIT: MAJIRA
No comments:
Post a Comment